IMEELEZWA kuwa, chanjo ya ugonjwa wa Covid 19 ambazo zimethibitishwa na kuanza kutumika nchini ni salama, hivyo wananchi waendelee kujitokeza kupata chanjo hizo ili kujikinga na ugonjwa huo.
Itakumbukwa kwamba, chanjo ambazo zimethibitishwa na zinazotumika hapa nchini ni Moderna, Pfizer, Sinopharm, Sinovac na Jensen (JJ) na zilianza kutolewa baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuzindua rasmi kampeni ya Kitaifa ya zoezi la chanjo Julai 28, 2021.
Akizungumza kwenye semina iliyoandaliwa na Chama cha waandishi wa habari Mkoa wa Dar es Salaam (DCPC) kwa kushirikiana na Shirika la Inter News kupitia mradi wa ‘boresha habari,’ Afisa Afya wa Mkoa wa Dar es Salaam Enezael Ayo alisema, licha ya changamoto ya uwepo wa taarifa za upotoshaji kuhusu chanjo ya ugonjwa wa Covid 19, lakini wananchi wanaendelea kujitokeza kupata chanjo.
Alisema, wakati wanaanza zoezi la kutoa chanjo hiyo, jijini Dar es Salaam kulikuwa na vituo vitatu, baadae vikaongezeka hadi 15, lakini baada ya kuona mwitikio unakuwa mdogo, waliongeza na hivi sasa vimefika vituo 318 na zoezi linakwenda vizuri.
“Mbali na kuongeza vituo hivyo, tulianzisha huduma ya Mkoba ambayo imewafikia watu wengi zaidi; kuanzia ngazi ya familia, mtu mmoja mmoja na kwenye mikusanyiko ya watu, na bado tunaendelea kutoa chanjo na wadau wanaendelea kujitokeza,” alisema Enezael huku akiwashukuru wadau wa maendeleo waliopo Dar es Salaam ambao wanawaunga mkono.
Alisema, kwa kiasi kikubwa huduma ya Mkoba imesaidia kuwafikia watu wengi hususani mitaani, ambapo wahudumu waliwafuata wananchi kwenye maeneo yao wanayoishi na kwenye maeneo ya kazi, na mafanikio yaliyopatikana yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na Wenyeviti wa Serikali za Mitaa ambao wanashirikiana vizuri na watoa huduma.
“Wenyeviti wa Serikali za Mitaa walishirikishwa na walisaidia kuhamasisha kuhusu umuhimu wa kuchanja, walikuwa wanapita na watoa huduma kwenye maeneo yao, tunashukuru wametusaidia sana,” alisema.
Aidha, Enezael alisema licha ya mafanikio waliyoyapata ikiwemo kuongezeka kwa idadi ya watu waliopata chanjo hiyo, bado kuna wananchi wengine hawajajua umuhimu wa chanjo, na hali hiyo imechangiwa kwa kiasi kikubwa na upotoshaji ambao umekithiri kwenye jamii kuhusu chanjo ya Covid 19.
“Kuna baadhi ya watu wanaipinga chanjo hii na kudai ina madhara, kibaya zaidi wakati tunatoa chanjo ya Polio kwa watoto, wakaendelea na upotoshaji na kudai kwamba, Serikali imeona chanjo ya Covid imeshindikana kwa wakubwa, wameamua kuhamishia kwa watoto, jambo ambalo halina ukweli,” alisema.
Alisema, chanjo hizo za watoto zimekuwepo kwa miaka mingi, na kama kuna hali inajitokeza ni maudhi ya kawaida yanayotokana na kuingia kwa kitu kipya mwilini.
“Baada ya chanjo wananchi waliambiwa wakisikia hali tofauti warudi kwenye vituo na kweli wapo waliorudi na waliripoti maumivu ya kichwa na homa; ambayo ni maudhi madogo madogo na kawaida pale kitu kipya kinapoingia mwilini, ila hakuna taarifa ya vifo,” alisema.
Aliendelea kusema: “kuna waliodai ukipata chanjo unabadilika, hadi leo hakuna kilichotokea, watu wanaendelea na maisha, sote tumeona hadi viongozi wa nchi wamechanja, tuelewe kwamba viongozi wetu hawawezi kuua watu wao, watu ni utajiri.”
Kwa upande wake mmoja wa watoa mada kwenye semina hiyo Dkt. Christina Mdingi ambaye ni mtaalamu wa masuala ya afya alisema, chanjo hiyo ni salama na inafaa kwa matumizi ya binadamu hivyo, aliwaomba waandishi wa habari waendelee kuwahamasisha wananchi wajitokeze kuchanja.
“Waandishi wa habari ni watu muhimu sana kwenye suala hili, wao wakielewa kuhusu umuhimu wa chanjo hii, jamii nzima itaelewa, na itahamasika kwa haraka, tujifunze, tuchukue tahadhari, chanjo ni salama wataalamu wamethibitisha na rais amethibitisha,” alisisitiza Dkt. Christina ambaye alitoa mada kuhusu nafasi ya vyombo vya habari katika kuhamasisha chanjo ya Covid 19.