Na Mwandishi Wetu
CHAMA cha Mapinduzi (CCM), Zanzibar kimewaonya watia nia wa Ubunge, Uwakilishi na wapambe wao dhidi ya vitendo na kauli ambazo zinaenda kinyume na maadili, sheria na kanuni za uchaguzi ndani ya chama.
Akizungumza na wanahabari leo 27, Juni 2025, Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis alisema, kuna ushahidi wa video unaowaonyesha wapambe wakiwapigia debe watiania wao, huku wakiwaponda wengine.
“Kuna wapambe kwa kujua au kutokujua wanasema tunamtaka fulani na fulani hatumtaki, fulani hana nafasi hapa na maneno mengine ya kibaguzi,” alisema Mbeto na kubainisha kuwa, kila MwanaCCM anayejiona anatosha anaruhusiwa kuchukua fomu na kuwania uwakilishi au ubunge.
Mwenezi Mbeto alisema, ubaguzi na kuchafuana sio utaratibu wa chama, kwani hakina ubaguzi na amewataka watia nia kuzungumza na wapambe wao kuwatahadharisha juu ya matendo ya namna hiyo.
Alisema, vitendo vya kuchafuana, kuunda makundi na kutumia pesa kukashifu wengine havitavumiliwa na vinaweza kuwaondoa kwenye mchakato wa uchaguzi.
“CCM ni chama kikubwa na jambo kama hilo likitokea, lazima kitajua kwani chama ni kikubwa na jambo hilo haliwezi kufanywa chama kisijue na pia nawakumbusha katazo la CCM Taifa la shamra shamra shamra, misafara ya wapambe na heka heka zingine wakati wa kuanza zoezi hilo kesho 28 Juni hadi 2 Agosti mwaka huu 2025” alisema Mbeto.
Mbeto amewataka watia nia na wapambe wao wawe watulivu na kudumisha amani na mshikamano na kusubiri wakati mwafaka ukifika baada ya vikao vya uteuzi na mtia nia anaruhusiwa kuambtana na mkewe na familia na sio zaidi ya watu hao na hata wana habari wametakiwa kukaa mbali na ofisi za chama wilaya zinakotolewa fomu.
“Mtu alichopanda ndicho atakachovuna na chama kitawatendea haki sawa watia nia wote bila ubaguzi atakaepatikana kuwania iwe uwakilishi au ubunge itakuwa ni kwa mujibu wa utaratibu wa chama chetu” alisema Mbeto.