CCM yatoa onyo kwa wagombea wanaotumia majina ya viongozi kujinadi

0

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

CHAMA Cha Mapinduzi(CCM) kimewaonya wanachama wake wanaopitapita majimboni kabla ya wakati huku wakitumia majina ya viongozi wa juu na kudai wametumwa kwenda kugombea waache mara moja kufanya hivyo.

Pia, CCM kimesisitiza na kuwaasa makatibu wa Wadi, Majimbo, wilaya na Mikoa, kuwatendea haki wagombea wote bila kufanya upendeleo wowote.

Msimamo huo umetolewa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamisi Mbeto Khamis, aliyesema kila kiongozi asimamie katiba, kanuni na taratibu za uchaguzi kwa njia ya usawa, haki na uwazi.

Mbeto alisema, kuna baadhi ya wanachama wa CCM wameanza kutumia majina ya viongozi na kuanza kujinadi kuwa wametumwa kwenda kugombea Udiwani, Ubunge na Uwakilishi wakati si jambo la kweli.

Alisema, hakuna kiongozi yeyote anayeweza kumtuma mwanachama akagombee wadhifa wowote wa kisiasa au wa kiserikali, kwani kwa kufanya hivyo ni kukiuka kwa taratibu za uchaguzi na matakwa ya kikatiba ya chama.

“Wanachama wote wana haki sawa mbele ya katiba, kanuni na taratibu za chama chetu. Kila mwenye uwezo , ushawishi na kukidhi vigezo vya kisiasa ana haki ya kugombea nafasi yoyote ndani ya chama na ngazi za dola,” alieleza.

Aidha, Katibu huyo Mwenezi alisema CCM ni chama kinachoongozwa kwa mujibu wa taratibu zake zilizojiwekea hivyo ni lazima kila wanachama, mgombea na watendaji wa CCM wafuate matakwa ya katiba ya chama.

“Kila mwanachama atumie ushawishi wake kisiasa kupitia vikao vya wanachama. Ajieleze hadi wapiga kura waridhike na kumchagua. Rushwa ndani ya CCM ni adui wa haki. Kila mwanachama na mtendaji ajiweke mbali na kupokea au kuomba rushwa,” alisema Mbeto.

Hata hivyo, alisema CCM kitaendelea kuwa chama cha kidemokrasia, kisicho na sera za ubaguzi wa rangi, ukabila wala ukanda au asili ya mtu.

“Kila mwanachama atakaegombea nafasi za kuwania ngazi za dola atapimwa kutokana na vigezo na sifa vilizowekwa na chama si vinginevyo,” alieleza.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here