CCM kuanzisha tume ya maridhiano

0

Na Albert Kawogo

MGOMBEA Mwenza kwa nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Emmanuel Nchimbi amesema, iwapo watapewa ridhaa, moja ya mambo ya kipaumbele kwenye siku 100 za mwanzo ni kuanzisha Tume ya Maridhiano ili kuhakikisha Watanzania wote wanasikilizwa na kuishi kwa umoja na mshikamano.

Dkt. Nchimbi amesema hayo leo Septemba 3, 2025, katika Uwanja wa Lalago wilayani Maswa, Simiyu, katika kampeni za uchaguzi mkuu wa madiwani, wabunge na Rais utafaofanyika Jumatano ya Oktoba 29, 2025.

Alisema, tume hiyo inalenga kujenga Tanzania yenye umoja, maridhiano na mshikamano wa kitaifa.

“Tunataka nchi iwe na watu wanaosikilizana na kuelewana. Wale wengi wasikilizwe, na wale wachache wasinyamazishwe. Tanzania yetu itabaki imara ikiwa Watanzania wote watashirikishwa,” alisema Nchimbi.

Mbali na suala hilo la maridhiano, Dkt. Nchimbi alisema, Serikali ya awamu ijayo itatekeleza miradi ya kijamii ikiwemo ujenzi wa zahanati 10, madarasa 100 ya shule za msingi, madarasa 200 ya sekondari, na vyumba 75 vya maabara.

Aidha, alisema mtandao wa maji utaboreshwa katika vijiji vya Mogwa na Isulile, huku eneo la umwagiliaji likiongezeka hadi kufikia hekta 500 kupitia skimu mpya za umwagiliaji.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here