RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amelivunja rasmi Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mujibu wa masharti ya Ibara ya 90(2)(a) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.
Uamuzi huu unatoa fursa kwa uteuzi wa wagombea wa Uchaguzi Mkuu pamoja na kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wenyewe.
Baada ya hatua hii, Bunge halitaruhusiwa kuketi tena hadi baada ya Uchaguzi Mkuu na baada ya kuapishwa kwa wabunge wapya, isipokuwa kwa masharti ya Ibara ya 90(4) ya Katiba hiyo hiyo, ambayo inampa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mamlaka ya kutoa Taarifa Maalum ya kuitisha Mkutano wa Bunge na kuagiza kwamba Spika pamoja na wote waliokuwa wabunge mara tu kabla ya kuvunjwa kwa Bunge, wahudhurie Mkutano huo iwapo kutatokea hali ya hatari (vita, majanga au maafa makubwa) inayohitaji Bunge kukutana.
Kuvunjwa rasmi kwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni hatua ya mwanzo kuelekea Uchaguzi Mkuu ulioandaliwa kufanyika tarehe 29 Oktoba, 2025 kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Tume ya Uchaguzi (INEC).
Baraza la Mawaziri litaendelea kuwepo na kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa masharti ya Ibara ya 55(5) na Ibara ya 57(2)(b) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.