MENEJA wa Mkoa wa Mtwara wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Joseph John Mwabusila, ameeleza kuwa miradi inayoendelea kutekelezwa na Shirika hilo katika mikoa ya Mtwara na Lindi itakuwa chachu kubwa ya kukuza mapato ya Shirika.
Akizungumza wakati akiikaribisha Bodi ya Wakurugenzi ya NHC iliyoanza ziara ya kutembelea miradi hiyo, Mwabusila alisema kuwa ujenzi wa maghala ya mazao pamoja na mradi wa biashara wa Masasi unatarajiwa kuongeza mapato ya Shirika katika Mkoa wa Mtwara kwa asilimia 100.
“Kwa sasa tunakusanya wastani wa Shilingi Milioni 80 kwa mwezi, lakini kukamilika kwa miradi hii kutaleta ongezeko kubwa la mapato na kuinua mchango wa Mkoa katika pato la Shirika,” alisema Bw. Mwabusila.
Bodi hiyo, inayoendelea na ziara katika mikoa ya Ruvuma, Njombe, Iringa, Morogoro na Dodoma, inalenga kujionea namna NHC inavyotekeleza miradi ya kimkakati itakayoongeza tija, ajira, na mapato ya ndani ya Shirika.
Wajumbe wa Bodi wamepongeza hatua za ubunifu zinazochukuliwa na Menejimenti ya NHC, wakisisitiza umuhimu wa mikoa yote kubuni miradi yenye tija, kuhakikisha uwiano kati ya mapato na gharama za uendeshaji, na kukusanya kodi kikamilifu.
“Tunapongeza Mkoa wa Mtwara kwa ukusanyaji mzuri wa kodi na tunataka ubunifu huu uenezwe kote nchini,” walisema wajumbe wa Bodi.
Ziara hii ni sehemu ya mikakati ya NHC kuhakikisha kila mkoa unachangia kikamilifu katika kukuza mapato ya Shirika, sambamba na azma ya Serikali ya kujenga uchumi imara unaotegemea uwekezaji wa ndani.