BANDARI imetajwa kuwa ni chanzo kingine cha mapato yanayotokana na Biashara ya Kaboni.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mkuu wa Bandari ya Oslo iliyopo nchini Norway Ingvar Mathisen wakati Ujumbe wa Tanzania ulipotembelea bandari hiyo hivi karibuni.
Ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Waziri wa nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhandisi Hamad Yussuf Masauni ulitembelea bandari hiyo kwa lengo la kujifunza namna inavyohifadhi mazingira na kuzuia uzalishaji wa gesijoto.
Akizungumza na ujumbe huo, Mkurugenzi Mkuu Mathisen alisema, Bandari ya Oslo ni mtambuka na haizalishi gesijoto na kuwa ni ya tatu kwa ukubwa duniani kwa kuwa na teknolojia janja ya bahari.
Aliongeza kuwa, lengo kuu la bandari hiyo ni kuhakikisha inapunguza jesi joto kwa asilimia 85 ifikapo mwaka 2030 hivyo, Serikali ya nchi hiyo imeazimia kufikia lengo hilo kwa kutumia teknolojia.
Kwa mujibu wa Mathisen, kuanzia mwaka 2018 Bandari ya Oslo imeacha kupokea na kuendesha meli zake kwa kutumia mafuta, badala yake meli zao iwe za kisafirisha abiria, mizigo au starehe zote zinatumia umeme.
Hivyo, alisema kwa vyombo vyote ambavyo havitumii teknolojia hiyo, bandari ya Oslo hutoza ada ya uzalishaji gesi joto-‘ Emission Fees’( inayojumishwa kwenye mpango wa biashara ya kaboni).
Itakumbukwa kuwa, Tanzania ni nchi ambayo upande wake wa mashariki una pwani ndefu ya Bahari ya Hindi ambayo ina Bandari kubwa ya Dar es Salaam, Mtwara na Tanga na pia kuna bandari ndogo zinazohudumia Lindi, Kilwa Masoko, Mafia, Pangani na Kwale.
Vilevile, bandari zote hizi hutumia vyombo vya usafirishaji hivyo, kwa kuwa na teknolojia ya kutambua kila chombo huzalisha kiasi gani cha gesi joto, Mamlaka husika kwa kushirikiana na Kituo cha Ufuatiliaji wa Kaboni (NCMC) zinaweza kufanya biashara hiyo kwa kudai ada ya uzalishaji gesi joto.
Kupitia ziara hiyo Tanzania imebainisha fursa mbalimbali za uhifadhi na usimamizi wa Mazingira kupitia Uchumi wa Buluu na Biashara ya Kaboni.