Balozi Matinyi awasilisha hati za utambulisho kwa mfalme wa Sweden

0

BALOZI wa Tanzania nchini Sweden, Mobhare Matinyi, amewasilisha rasmi Hati za Utambulisho kwa Mfalme Carl XVI Gustaf, katika hafla maalum iliyofanyika Juni 12, 2025, katika Kasri la Mfalme wa Sweden, jijini Stockholm.

Baada ya mazungumzo mafupi kwenye Wizara ya Mambo ya Nje ya Ufalme wa Uswidi, Balozi Matinyi alisindikizwa kwa gwaride rasmi kuelekea kwenye Kasri la Kifalme na kuwasilisha hati hizo kwa Mfalme Carl XVI Gustaf, ikiwa ni ishara rasmi ya kuanza kazi yake kama mwakilishi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Sweden.

Katika mazungumzo yao mafupi, Balozi Matinyi alimfikishia Mfalme Carl XVI Gustaf salamu za Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwake yeye binafsi pamoja na serikali na watu wa Uswidi.

Balozi Matinyi alimwelezea pia Mfalme Carl XVI Gustaf dhamira ya Tanzania ya kuendeleza na kuimarisha uhusiano mzuri wa kidiplomasia uliopo baina ya nchi hizi mbili na nia ya kukuza ushirikiano katika utekelezaji wa diplomasia ya uchumi, hususani katika uwekezaji, biashara, utalii, elimu na mafunzo ya ufundi, afya, nishati, miundombinu, utunzaji mazingira, pamoja na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Kwa upande wake, Mfalme Carl XVI Gustaf alituma salamu za undugu na urafiki kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan; na kueleza kuwa nchi yake ya Uswidi itaendelea kushirikiana na Tanzania kwa manufaa ya mataifa yote mawili, hususani katika kuendeleza sekta za viwanda, nishati, madini, utalii na elimu.

Itakumbukwa kuwa, Matinyi aliteuliwa na Rais Dkt. Samia kuwa Balozi wa Tanzania nchini Uswidi mnamo Machi 25, 2025, ambapo pia atakuwa na jukumu la kuiwakilisha Tanzania katika nchi za Denmark, Finland, Iceland, Norway, Estonia, Latvia, Lithuania na Ukraine.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here