AICC na mikakati ya kunufaika na ‘Uchumi wa Mikutano’

0
Mkurugenzi Mtendaji wa AICC, Ephraim Mafuru, akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari kuhusu shughuli za taasisi yake.

Na Iddy Mkwama

“Utajiri wa miaka 45 ya historia ya AICC pamoja na wito wa ‘We Bring the World to Tanzania’ (Tunaileta Dunia Tanzania), unakwenda kudhihirishwa na mkakati tuliojiwekea wa kuhakikisha tunaandaa Mikutano ya Kimataifa ambayo imekuwa ikiitangaza Tanzania katika ramani ya dunia,”

“Tunajivunia na kujisikia fahari kwa kuendesha shughuli mikubwa (mikutano), tuna vifaa vya kisasa na tunaweza kutafsiri lugha tano, tuna kumbi kubwa na ndogo…sisi ni wenyeji wa diplomasia ya uchumi wa mikutano.”

Hiyo ni kauli ya Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC), Ephraim Mafuru, ambaye anasema kwa sasa wageni wengi wanaipenda Tanzania na wanatarajia siku zijazo kupokea mikutano mikubwa ya Mashirika na Taasisi mbalimbali kutoka nje ya nchi.

Mafuru anasema, kwa sasa Tanzania inashika nafasi ya tano kwenye orodha ya nchi ambazo zinapokea wageni kwa ajili ya kufanya utalii wa mikutano, lakini lengo lao ni kupanda kwenye nafasi ya tatu na ikibidi kuwa kinara na tayari jitihada za kufikia malengo hayo zimeanza.

Anasema, wanaandaa mpango ambao utawaelekeza wawekeze wapi na watafanya ukarabati na kuboresha kumbi zake ukiwemo Ukumbi wa Mwalimu Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam ambao unasimamiwa na AICC.

Ukumbi huo mbali na maboresho madogo yaliyofanyika, wanatarajia kuongeza eneo ili waweze kupokea mikutano mikubwa zaidi kama ambao umemalizika hivi karibuni wa Mifumo ya Chakula Afrika (AGRF – Afrika Food System Summit).

Kwenye mkutano huo ambao ulikutanisha wageni zaidi ya 5400, Mafuru anasema walifanikiwa kuwapatia huduma kwa siku sita walizokaa nchini na wamefikia malengo. “wageni wamefikia malengo na sisi tumeitangaza nchi yetu.”

Vile vile, wanaangalia uwezekano wa kujenga ukumbi mkubwa zaidi wa mikutano jijini Arusha, hoteli za hadhi ya nyota tano, maduka makubwa na hata nyumba za kupangisha.

“Tuna hekari 90 ambazo tupo kwenye mchakato wa kujenga Kituo kikubwa na cha kisasa cha mikutano ambacho kitabeba watu wengi zaidi ya AICC,” anasema.

Mafuru anasema, kituo hicho kitajulikana kama “Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Kilimanjaro,” kitakuwa na huduma mbalimbali ambazo zitamfanya mgeni kufurahia uwepo wake Arusha na Tanzania kwa ujumla na kuiingizia nchi mapato.

Mafuru anasema, mbali na kujenga kituo hicho cha kisasa, wanatarajia kuboresha hospitali inayomilikiwa na Kituo hicho ambayo ina vitanda 32, na wana vifaa vya uchunguzi vya maabara vya kompyuta; ikiwemo mashine ya Kisasa ya X- Ray, kiti cha Meno na Kliniki ya tiba ya mwili.

“Hospitali hii inahudumia wakazi wa Arusha na wajumbe wa mikutano, baadhi kutoka UN, EAC, wafanyakazi wa AU, watalii, wafanyabiashara pamoja na wateja wa ndani,” anasema na kuongeza kuwa, kwasasa ina uwezo wa kuhudumia wagonjwa zaidi ya 7,000 kwa mwezi, ambapo lengo ni kufanya kuwa ya kisasa ili kuhudumia wagonjwa wengi zaidi.

“Tunataka kuiboresha na kuwa na huduma za Kisasa ili hata kama mgeni amekuja kwenye mkutano na amepata changamoto ya afya, anapata huduma kwenye hospitali yetu,” anasema Mafuru.

Hata hivyo, licha ya mafanikio yaliyopatikana na mipango iliyopo, Mafuru alitaja baadhi ya changamoto ambazo zinawakabili ikiwemo uchakavu wa miundombinu ya kumbi zao, ingawa aliweka wazi kwamba, tayari wameanza kulifanyia kazi suala hilo na wameanzia kwenye ukumbi wa JNICC.

Mbali na hilo, anasema wanakabiliwa na ugumu wa wateja wao kulipa madeni hususani Taasisi na Mashirika ya umma, ambapo kwasasa wanadai zaidi ya Bilioni 7 na ameomba wadaiwa hao kuwalipa ili waweze kujiendesha.

“Tutaomba kibali cha Msajili wa Hazina kwamba ili tukuruhusu kutumia kumbi zetu kwa taasisi za umma ni lazima ulipe kabisa. Kwa maana sasa kuna madeni ambayo tunadai yanafikia kiasi cha Shilingi Bilioni 7,”

“Unakuta Taasisi imejitangazia kuingiza faida na inatoa gawio, lakini inadaiwa, tutaomba kibali kabla ya kusoma faida za hesabu zako kwanza lipa deni letu,” anasema Mafuru.

Anaendelea kusema: “Jumla ya deni ni Shilingi Bilioni 7.4 kati ya hao wadaiwa 17 hadi 20 ni Taasisi za Serikali ambapo ni sawa na asilimia 65 ya deni lote ambalo ni sawa na Shilingi Bilioni 4.76 zinazodaiwa na Taasisi za Serikali.”

Aidha, Mkurugenzi Mtendaji huyo wa AICC anasema, wana mikakati mingi wameiweka ambayo ina lengo la kuchangia zaidi uchumi wa nchi sambamba na kuimarisha akiba ya fedha za kigeni nchini.

“Mheshimiwa Gavana hiki (AICC) ndiyo kituo cha kukupa Dola za Kimarekani. Tumejipanga kwa umakini mwaka huu tutaliingizia Taifa zaidi ya Dola za Kimarekani Milioni 48,” anasema Mafuru.

“Pia tuna mikakati tunayokwenda kuifanya, tunaamini tuna uwezo wa kufanya zaidi ndani ya miaka mitano ijayo, tumejiwekea malengo ya kuwa na mikutano kuanzia 30 hadi 50 ya watu 2000,” anasema Mafuru huku akisisitiza, Tanzania ina uwezo wa kuteka uchumi wa mikutano kwa sababu ina kila kitu.

“Tanzania ina kila kitu kinachoifanya kuwa kinara wa kuendesha uchumi wa mikutano, wengine wana ‘facilities tu,’ hivyo nasisi tunajipanga kuhakikisha tunaweka mazingira mazuri ya kuwakarimu wageni ili tuwe bora zaidi,” anasema Ephraim Mafuru.

Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) kilianzishwa chini ya Sheria ya Mashirika ya Umma Na.17 ya mwaka 1969 kwa agizo la Rais kupitia tangazo la Serikali namba 115, lililochapishwa Agosti 25, 1978.

AICC kinamilikiwa na Serikali ya Tanzania na kinafanya kazi chini ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na kinafanya kazi kama Shirika kamili la kibiashara huku utoaji wa huduma za mkutano ndio biashara kuu.

Wachambuzi wa masuala ya uchumi wanasema, ‘uchumi wa mikutano’ duniani utaongezeka zaidi, ambapo kadri miundombinu na teknolojia ya upashanaji wa habari zinavyozidi kuboreshwa barani Afrika, ndivyo mikutano mingi zaidi ya Kimataifa itakavyofanyika, na Afrika inatazamiwa kunufaishwa zaidi kutokana na ongezeko hilo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here