Na Mwandishi Wetu
OKTOBA mwaka huu 2025 tunatarajia kuingia kwenye Uchaguzi Mkuu wa rais, wabunge na madiwani, na tayari vyama vinajipanga kulingana na upepo wa kisiasa unavyokwenda.
Kilichopo madarakani kinatathmini utekelezaji wa Ilani yake katika kuwaletea maendeleo wananchi wake. Vyama vya upinzani vinatafuta namna ya kushinda katika maeneo tofauti kulingana na udhaifu wa waliopo madarakani.
Nchini kuna vyama 19 vya kisiasa, vilivyo sajiliwa vyenye haki ya kusimamisha wagombea katika ngazi zote. Pia, wanachama wake wenye sifa, wana haki ya kupiga kura kwa mgombea yeyote wanayemtaka.
Kwa mantiki hiyo, uchaguzi ni mchakato na unaanzia kwa chama husika kuhamasisha wanachama wake kujiandikisha na wengine kurekebisha taarifa zao katika daftari la kudumu la wapiga kura. Wanasiasa wengi wanaelewa hivyo, kupishana na mchakato huo na mingine ni kukigharimu chama.
Inapotokea chama cha upinzani kupishana na mchakato au kuona wamepoteza au hawana ushawishi, kuna hatua huchukua ikiwa ni pamoja na kutafuta ushirika na vyama vingine kama walivyofanya ACT Wazalendo.
Hatua nyingine ni kutafuta sababu ya kukimbia uchaguzi ili kukwepa aibu ambayo inaweza kukifanya chama kupoteza ushawishi na kufa au kubaki jina Ofisi za Msajili wa vyama vya siasa.
Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu na Makamu wake, John Heche wakaamua kuliko aibu, bora wasishiriki.
Chadema muda mwingi wameutumia katika kuhubiri No reform No election na kushindwa kuwashawishi wanachama wao kuhusu daftari la wapiga kura kiasi kwamba, hata wanachodai kikifanyika hawajawaandaa wanachama wao kupiga kura.
Hatua hiyo ni kupishana na mchakato na kukubali kuingia katika Uchaguzi Mkuu ni kutaka kuvuna aibu. Kwa kutambua misingi ya demokrasia, wenzao ndani ya chama wakagoma kwa kujiorodhesha na kueleza isivyo haki kutoshiriki uchaguzi, wakaitwa G -55.
ACT Wazalendo kiliona yote hayo na kwa busara za viongozi wao, wakatafuta vyama shirika waunganishe nguvu.
Kulingana na Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Bara, Isihaka Mchinjita, mara baada ya kuchukua fomu ya kuwania Ubunge jimbo la Lindi Mjini, anasema walitaka ushirikiano na vyama vingine ili kuing’oa CCM madarakani.
Anasema waliviandikia barua vyama vya siasa vikubwa vya upinzani vyenye ushawishi karibu vyote kuomba ushirika lakini hawakujibiwa.
Wakawatembelea ofisini kwao, lakini hakuna lolote la maana na hadi hivi sasa kimya. ACT Wazalendo baada ya kukataliwa na wenzao, wameamua kupambana wenyewe.
Chama hicho kinajipanga huku kukiwa na tetesi za baadhi ya wanachama wao kutaka kurudi na wengine kutimkia Chama cha Wananchi (CUF).
Mara kadhaa Mwenyekiti wa CUF, Prof. Ibrahim Lipumba anasema, kuna vijana walikuwa katika chama hicho wanataka kurudi (waliounda ACT Wazalendo wengi walitoka CUF).
Mwenyekiti huyo anasema, yupo tayari kuwapokea wagombee nafasi wanazotaka ili kuwatumikia wananchi.
Pia, Prof. Lipumba anabainisha kuwa yupo tayari kumuachia kijana mwenye uwezo, madhubuti na mwenye msimamo kuwania Urais kupitia chama hicho.
Kampeni za Urais ni mzunguko mkubwa unaohitaji kijana mwenye nguvu za kutosha na yeye ingawa bado ‘ngangari’ lakini anakiri umri umeenda.
Wimbi la kuhama viongozi wa ACT Wazalendo Pemba hivi karibuni, kwenda CCM ni jambo jingine linalofanya viongozi wa chama hicho waone umbali uliopo kutoka walipo hadi kiti cha Urais iwe Jamhuri ya Muungano au ya Umoja wa Kitaifa, Zanzibar.
Katibu Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo Khamis Mbeto Khamis anasema ACT Wazalendo hawana hoja, Zanzibar.
Anasema maendeleo makubwa yaliyofanywa na Rais Dkt. Hussein Mwinyi hata kipofu anayaona.
Ukweli huo ndio ambao si Mwenyekiti wa chama hicho, Zanzibar Othman Masoud Othman ‘OMO’ wala Makamu wake, Zanzibar Ismail Jussa Ladhu wanataka kuusikia.