Na Mwandishi Wetu
CHAMA cha Muungamo wa Wakulima (AAFP)kimezishauri Serikali za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT)na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kuzuia uuzaji nafaka nje ya nchi ili kukabiliana na tishio la njaa.
Ushauri na tahadhari hiyo imetolewa hivi karibuni na Mwenyekiti wa AAFP Said Soud Said alipozumgumza na waandishi wa habari nje ya ukumbi wa Chuo cha Utalii mara baada ya kuhudhuria Mkutano Jijini Dar es Salaam.
Soud alisema, licha ya chama chake kutetea maslahi ya Wakulima, anazishauri Serikali kuweka mkakati maalum wa kuzuia uuzaji mahindi, mtama na mupunga nje kufuatia kuzuka kwa ukame katika pembe ya Afrika na upungufu wa chakula.
Alisema, Wakulima wana haki ya kuuza mazao mahali popote baada ya kuvuna mazao yao wanapopata bei nono lakini akashauri kutokana na hali ilivyo ipo haja ya kuchukua tahadhari zaidi.
“Ukiacha nchi za pembe ya Afrika kuzuka njaa janga ukame na mabadiliko ya hali ya hewa pia misimu ya mvua haieleweki. Wakulima wanalima kwa bahati nasibu, Mito, vijito na mabwawa inakauka. Bahari na maziwa yanaimeza nchi kavu,” alisema Soud.
Aidha, alitaja kuzuka ukame, kuwepo kwa mvua za nadra, mabadiliko ya tabia nchi na kukosekana mavuno ya kutosha. “Isionekane ni siasa huo ndio ukweli . Vyama vya siasa , NGOs, Vyama vya Kijamii, Jumuiya za Kikanda na za Kimataifa huu ni wakati wa kushikamana”
Pia, Mwenyekiti huyo amezishauri Serikali zianze kuweka msukumo wa makusudi katika sekta ya kilimo ili wakulima walime mashamba makubwa ya umwagiliaji na kuvunwa mazao nyakati zote.
“Serikali izidi kuvutia wawekezaji wa nje na ndani wawekeze katika kilimo. Tanzania bado ina ardhi kubwa yenye rutuba kwa kilimo hususan cha umwagiliaji . Bila kutoa mikopo na ruzuku wakulima wadogo, wakati na wakubwa njaa itaitatatiza nchi,” alisisitiza.
Mwenyekiti huyo wa AAFP alisema, benki ya wakulima itoe mikopo kwa wakulima wakubwa ili wajue zana za kilimo za kisasa zitakazowafanya kulima mashamba makubwa ya mahindi, mpunga, pamba na alzeti.
Mazao mengine alitaja, dengu , kahawa, chai , ngano, korosho, karafuu, kunde, maharage, soya, viazi vitamu, mbaazi na choroko
“Wakulima wetu walime jadi ekari mia tano na kuendelea. Wakopeshwe fedha ili wanunua zana za kilimo bora. Kilimo cha kutegemea mvua na kijembe cha mkono hakina tija wala manufaa kwa maendeleo,” alieleza,
Hata hivyo, Soud alishauri kuwe na mpango mkakati maalum utakaowajengea uelewa wakulima kuhusu kilimo bora na kutambua kuna wimbi la mabadiliko ya tabia nchi kwani baadhi yao hawajawa na uelewa wa kuridhisha.