NAIBU Waziri, Ofisi ya Rais-TAMISEMI (Afya) Dkt. Festo Dugange, amezitaka halmashauri zenye uwezo wa kiuchumi kuajiri watumishi wa mikataba ili kutatua changamoto ya upungufu wa watumishi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Dkt. Dugange ametoa maelekezo hayo kwa wakurugenzi wa halmashauri nchini, wakati akifunga mkutano wa 15 wa Taasisi ya Maboresho ya Mamlaka za Serikali za Mitaa (TOA) uliofanyika kwa siku mbili katika Ukumbi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma uliopo kwenye Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma.
“Ofisi ya Rais-TAMISEMI ilitoa mwongozo maalum wa namna ya kuajiri watumishi wa mikataba na hususani wa sekta ya elimu na afya, hivyo Makatibu Tawala wa Mikoa kawasimamieni Wakurugenzi wa Halmashauri kutekeleza mwongozo huo,” Dkt. Dugange alisisitiza.
Dkt. Dugange alisema, Serikali imeleta fedha nyingi katika halmashauri ambazo zimejenga zahanati, vituo vya afya, hospitali za wilaya na shule na inaendelea kuajiri kwa awamu, hivyo halmashauri zinazokusanya mapato ya kutosha zinapaswa kuajiri watumishi wa mikataba ili waweze kutoa huduma kwa wananchi kupitia mbiundombinu hiyo iliyojengwa na Serikali.
Aidha, Dkt. Dugange amehimiza kuwa, siku zote Ofisi ya Rais-TAMISEMI inaamini watumishi wote waliochini ya TAMISEMI wakifanya kazi kwa bidii na ufanisi, ni dhahiri kwamba kiwango cha utendaji kazi wa Serikali kitakuwa ni zaidi ya asilimia tisini kwani majukumu yanayotekezlezwa na TAMISEMI yanawagusa wa Tanzania wengi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Tawala za Mikoa wa Ofisi ya Rais-TAMISEMI Beatrice Kimoleta amesema kuwa, TAMISEMI itaendelea kushirikiana na Taasisi ya Maboresho ya Mamlaka za Serikali za Mitaa (TOA) ili iweze kuwa imara na kutekeleza majukumu yake kikamilifu.