Mwambe mambo magumu jimboni Masasi

0

Na Mwandishi Wetu

WAKATI chama cha Mapinduzi (CCM) kikiwa kimetangaza kuanza kwa mchakato wa ndani wa uteuzi wa wagombea watakaowakilisha chama hicho kwenye Uchaguzi Mkuu unatarajia kufanyika Oktoba, mwaka huu joto la kisiasa limeanza kupanda kwa baadhi ya wabunge ambao hawajatimiza ahadi zao.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa CCM Dkt. Emmanuel Nchimbi, mchakato huo wa kupitisha wagombea kwa nafasi za ubunge, ujumbe wa Baraza la wawakilishi na udiwani utaanza rasmi Juni 28, 2025 na utakamilika Julai, 2025.

Uchunguzi uliofanywa na timu ya waandishi wa habari ambao wanafanya ziara ya kufuatilia hali ya kisiasa kwenye majimbo mbalimbali nchini, umebaini Geofrey Mwambe ambaye ni mbunge wa Masasi mjini, ni mmoja wa wabunge ambao wana wakati mgumu na ana uwezekano mdogo wa kurudi bungeni.

Kwasasa, upepo wa kisiasa kwa Mwambe haupo vizuri kutokana na kile kinachoelezwa ni kushindwa kutimiza ahadi zake alizozitoa wakati anaomba ridhaa ya kuwa mbunge wa jimbo hilo kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

Inaelezwa, Mwambe wakati wa kampeni aliahidi kuwasaidia kiuchumi na kuwatafutia fursa makundi mbalimbali kwenye jimbo hilo, lakini ameshindwa kutimiza ahadi zake na kwa muda uliobaki wanaamini hawezi kuzitimiza.

“Mbunge wetu amejitengenezea mazingira magumu sana ya kuaminiwa tena kwenye uchaguzi ujao, aliahidi kuwasaidia wafanyabiashara wa korosho kupata soko Kimataifa na kikubwa zaidi akawaambia atahakikisha kituo kikubwa cha mauzo ya Korosho kinakuwa Masasi,” alisema mmoja wa wafanyabiashara wa Korosho ambaye hakupenda jina lake liwekwe hadharani.

Mfanyabiashara huyo alidai, jambo kubwa zaidi ambalo limewakera zaidi wafanyabiashara wa korosho ni kitendo cha mbunge huyo kuwashawishi kununua magari kwa ajili ya kubebea korosho kwa ahadi ya kuwatafutia fursa za kusafirisha zao hilo.

“Kuna watu wamekopa fedha benki kwa ajili ya kununua maroli kwa kuamini ahadi ya mbunge kwamba atatufungulia fursa za kusafirisha korosho na kuifanya Masasi kuwa kituo kikuu cha zao hilo, lakini hadi leo hakuna dalili yoyote wanahangaika kulipa madeni, jambo la kusikitisha zaidi tunasikia biashara hiyo anaifanya mwenyewe,” alisema.

Mbali na kundi hilo la wafanyabiashara wa korosho, vijana wanaosafirisha abiria kwa pikipiki nao wanamlalamikia mbunge huyo kwa kushindwa kutimiza ahadi yake ya kuwapatia mikopo, ambapo aliwataka wajiunge kwenye vikundi.

“Tumejiunga kwenye vikundi lakini ahadi yake hajatimiza, sasa sijui akija tena atatuambia nini na tuseme wazi hatutamsikiliza tena, maana ameshindwa kutekeleza ahadi yake, hatutakubali aje na ahadi nyingine,” alisema kijana aliyejitambulisha kwa jina la Mustafa.

Aidha, wananchi wengine waliozungumza na waandishi wa habari waliokuwa kwenye ziara hiyo walisema, wanakabiliwa na changamoto kubwa ya kukosekana kwa huduma za kijamii ikiwemo maji, umeme wa uhakika na maji.

Walisema, wameshangazwa na kitendo cha mbunge wao kutoa magari kwa shule za sekondari wakati miundombinu ya barabara haipitiki kwa urahisi kwenye maeneo mengi ya jimbo hilo na kwamba alipaswa kwanza kushughulikia zipatikane barabara za uhakika kabla ya kutoa magari hayo.

“Magari aliyoyatoa hayatusaidii sisi wananchi wa kawaida ambao tunakabiliwa na changamoto nyingi. Tuna tatizo la barabara, umeme nao sio wa uhakika, maji nayo ni shida kubwa, lakini mbunge wetu kaona kipaumbele ni magari ya kifahari kwa shule za sekondari wakati sisi wananchi tunateseka na changamoto za huduma mbalimbali za kijamii,” alisema Maulid Mohamed, mkazi wa Masasi.

Kutokana na hali hiyo, wananchi hao wamesema watahakikisha kwenye uchaguzi ujao wanafanya maamuzi sahihi na kupata mwakilishi ambaye atawapigania ili kutatua changamoto zinazowakabili.

“Tumechoshwa na ahadi zisizotekelezwa, kwenye uchaguzi ujao hatutarudia tena makosa, tutachagua mbunge ambaye atatujali na kutupigania bungeni ili changamoto ambazo zinatukabili zipatiwe ufumbuzi,” alisisitiza mwananchi huyo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here