Serikali kupambana na wachimbaji wasio na leseni

0

Na Albert Kawogo, Dodoma

SERIKALI kupitia tume ya madini itaanza kampeni kupambana na wachimbaji madini wasio na leseni ambao wamekuwa wakivamia maeneo yenye leseni na kuchimba bila ridhaa ya wamiliki.

Mpango huo wa Serikali utatekelezwa kupitia kikosi kazi maalum kitakachoundwa hivi karibuni na Wizara ya Madini.

Akizungumza katika Mkutano na waandishi wa habari mjini Dodoma Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini Mhandisi Ramadhani Lwamo alisema, Serikali inapoteza mapato kutokana na wachimbaji madini wasio na leseni na akasisitiza kuwa, chini ya kikosi kazi kitakachoundwa wanaamini jambo hilo litakwisha.

Akijibu maswali ya waandishi wa habari waliotaka kufahamu ni lini Serikali itawakabili wachimbaji haramu hasa katika mikoa inayozalisha dhahabu kwa wingi Mhandisi Lwamo alisema, wakati mwingine ni udhaifu wa maafisa madini wa maeneo hayo wasio waaminifu ambao wamekuwa wakishirikiana na wahalifu kufanya uhalifu wa kuvamia maeneo yanayomilikiwa kihalali.

Aidha, kupitia Mkutano huo Mhandisi Lwamo alisema kiwango cha makusanyo ya maduhuli ya Serikali kimepanda kutoka Shilingi Bilioni 624.61 zilizokusanywa mwaka wa fedha 2021/2022 hadi kufikia Shilingi Bilioni 753.82 mwaka wa fedha 2023/2024

Alisema, mchango wa sekta ya madini kwenye Pato la Taifa umeongezeka kutoka asilimia 7.2 mwaka 2021 hadi asilimia 9 mwaka 2023 kutokana na kuimarika kwa usimamizi wa shughuli mbalimbali za madini.

Kwa upande wa ukuaji wa sekta ya madini alisema umeongezeka kutoka asilimia 9.4 mwaka 2021 hadi kufikia asilimia 11.3 mwaka 2023.

Pia, amefafanua kuwa ukuaji wa sekta ya madini na mchango wake katika Pato la Taifa unatarajiwa kufikia asilimia 10 na zaidi ifikapo mwaka 2025.

Mhandisi Lwamo aliueleza Mkutano huo kuwa kuanzia mwaka wa fedha 2021/2022 mauzo ya madini katika masoko na vituo vya ununuzi wa madini yameendelea kuongezeka kutoka Shilingi Bilioni 2.361.80 hadi Shilingi Bilioni 2,597.18 kwa mwaka 2023/2024.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here