Mwitikio wa uwekezaji hatifungani za SUKUK ni pigo kwa Jussa wa ACT Wazalendo

0

Mwandishi Wetu, Zanzibar


MWITIKIO wa uwekezaji katika hatifungani za SUKUK, uliozinduliwa rasmi mwishoni mwa wiki, umefungua ukurasa mpya katika mageuzi ya kifedha Zanzibar.

Uwekezaji huu unatarajiwa kuongeza na kuiimarisha kifedha Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) tofauti na propaganda za mwanasiasa Jussa Ismail Ladhu ambaye awali alidai kuwa benki hiyo inaenda kuuzwa.

Ukweli wa jambo hilo ulionekana wazi kwa mamia ya watu kujitokeza na kufanya uwekezaji siku hiyo kwa kununua hatifungani hizo wakati wa uzinduzi wa mpango huo ambao upo chini ya Hazina ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na kuondoa madai ya Jussa na wenzake.

Katika uzinduzi huo Mfuko wa Hifadhi ya Taifa ya Jamii (ZFF), wamewekeza Shilingi Bilioni 30 achilia mbali watu binafsi ambao wamewekeza kati ya Shilingi Milioni 5 hadi Shilingi Milioni 70 na wawekezaji hao ni wale walioalikwa tofauti na waliokuwa wanafuatilia na kununua kwenye mfumo wakati wa uzinduzi huo.

Msingi wa Hatifungani hizo ambazo zinafuata sharia ya Kiislamu, ni wa kwanza kwa nchi za Afrika Mashariki na umekuwa na tija kubwa kwa nchi zinazoutumia ikiwemo Malaysia na Nigeria.

Kupitia hatifungani hizo, wafanyabiashara na Serikali wataweza kupata mikopo mikubwa isiyo na riba nchini mwao badala ya kutegemea kutoka nje ambayo kwa siku za karibuni imekuwa na changamoto nyingi achilia mbali riba zinazotozwa ambazo ni za kiwango kikubwa na zinazokinzana na imani ya dini.

Kupitia uwekezaji huo, mtu binafsi au taasisi inaweza kuanza kuwekeza kiwango cha kuanzia ni Shilingi Milioni 1, na kuiwezesha benki ya PBZ ambayo awali ilikuwa inatoa mikopo kwa wafanyabishara wadogo kutokana na ukosefu wa fedha za kutosha, sasa inaenda kutoa mikopo kwa ajili ya miradi mikubwa inayohitaji fedha nyingi.

Watu wengi wenye uwezo kifedha Zanzibar walikuwa wanashindwa kuwekeza kwa kuwa taasisi nyingi zinatoza riba, jambo ambalo linakwaza imani yao, hivyo kuanzishwa kwa hatifungani hizo kutawafanya wapate sehemu ya kuwekeza fedha zao na kupata faida badala ya riba.

Chini ya utaratibu huo fedha ambazo Serikali itakopa kwa ajili ya miradi mikubwa inayotekelezwa hivi sasa, hazitaingia katika deni litakalokatwa kwenye Pato la Taifa (GDP) tofauti na madeni mengine na milango ipo wazi kwa makampuni, wizara, watu wa dini mbalimbali kuwekeza katika Hatifungani hizo.

Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dkt. Hussein Mwinyi anasema, nchi hiyo hivi sasa inatekeleza miradi mikubwa na makampuni makubwa yanayokuja Zanzibar, hivyo yatahitaji kukopa, kwahiyo wanahitaji kufanyakazi na taasisi ambayo ipo imara kifedha.

Pia, kutokana na Hatifungani hizo ambazo faida hutolewa asilimia 10 kwa mwaka mara mbili na baada ya miaka saba aliyewekeza anaweza kutoa amana yake, zinakuja kuleta mapinduzi ya kifedha Zanzibar na wale wanaopotosha kuwa PBZ inauzwa wanahitaji kuelimishwa kama kweli hawajui.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango. Dkt. Saada Mkuya anasema, mipango mingi ya maendeleo inahitaji fedha katika mfumo na ushirikishaji wa wananchi kupitia uwekezaji wa hatifungani ndio njia ya kufikia lengo.

Anasema, Hatifungani ni uwanja mpana kwa serikali kupata fedha kwa ajili ya miradi badala ya kutegemea mikopo yenye riba isiyo rafiki na vyanzo vingine kwani taasisi, sekta binafsi na Serikali zina mahitaji makubwa ya fedha na kuwekeza kwenye hatifungani kutatatua changamoto hiyo.

Pamoja na kuwekeza kupitia mfumo wa Kielektroniki na kupata risiti ya kiasi cha fedha walichowekeza, pia watendaji wa SUKUK watawafuata wawekezaji hao walipo kwa ajili ya kusaini fomu maalum ya uthibitisho zaidi, na ni fursa adhimu kwa watu wote kuwa sehemu ya miradi ya maendeleo inayotekelezwa Zanzibar.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here