Masauni: Serikali inatambua mchango wa dini zote

0

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhandisi Hamad Yusuf Masauni amesema, Serikali inatambua na kuthamini mchango wa Dini zote katika kujenga maadili mema ndani ya jamii ya Watanzania.

Alisema, vijana wakifundishwa mila na desturi sahihi na kushika mafundisho ya dini, na wakawa na hofu ya Mwenyezi Mungu, maovu mengi yatapungua hapa nchini kwani mustakabali wa taifa unaujengwa na watanzania wenyewe kwa kusaidiana kuilea jamii katika maadili mema hasa kwa vijana ambao ndio viongozi watarajiwa.

Waziri Masauni ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Kikwajuni, Zanzibar, ameyasema hayo katika mahafali ya Chuo cha Kislamu cha MPF Zanzibar Februari 22, 2025 ambapo alikuwa mgeni rasmi katika mahafali ya kwanza ya chuo hicho.

“Kuifundisha jamii ni jambo la kuenziwa kwa vile umma wa sasa umekumbwa na vishawishi vibaya ambavyo kwa njia moja ama nyingine huwatoa watu kwenye mwelekeo.

Vishawishi vibaya vinaonekana dhahiri katika jamii. Sasa tunaposimama kuichunga jamii, yote kiujumla na mmomonyoko wa maadili si tu tunawasaidia wao waweze kutimiza ndoto zao bali ni kwa ustawi wa taifa letu kwa ujumla ili kufikia malengo tuliojiwekea.

“Kipekee nitumie nafasi hii kuwashukuru viongozi wetu wakuu, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa miongozo na maelekezo mbalimbali wanayotupatia ambayo yameendelea kuleta mafanikio ya maisha bora kwetu Watanzania.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here