TPA yapongezwa kwa kuhudumia meli na shehena kwa kasi na ubora

0

WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Dkt. Selemani Jafo ameipongeza Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kwa kuboresha miundombinu ya kutolea huduma katika Bandari zake hali iliyoongeza kasi na ubora wa kuhudumia Meli na Shehena.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa maonyesho ya 19 ya Biashara ya Afrika Mashariki yaliyofanyika katika Viwanja vya Furahisha jijini Mwanza, Jafo alisema maboresho hayo yamezifanya Bandari za Tanzania kuwa katika viwango bora, kuvutia Wateja na Kampuni kubwa za Usafirishaji na kuhimili ushindani kutoka Bandari za Nchi jirani.

“Uwekezaji huu umepunguza muda wa kuhudumia Meli kutoka siku 7 hadi kufikia siku kati ya 3 mpaka 4 huku muda wa Meli kusubiri kuingia Bandarini ukipungua kutoka siku 5 hadi siku 3.

Akiongea kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Afisa Uhusiano Mwandamizi wa TPA, Leonard Magomba alisema, baada ya kupatikana kwa Wabia katika uendelezaji na uendeshajiwa Bandari ya DSM, TPA imejipanga kuimarisha Bandari zake nyingine kwa kuzifanyia upanuzi wa Miundombinu na uwekezaji wa Vitendea kazi na Wataalamu ili nazo zifikie Viwango vya kimataifa vya ubora wa huduma.

“Kwa sasa Bandari yetu ya DSM ina uwezo wa kuhudumia Meli kubwa zenye urefu wa hadi Mita 300, hii imewezekana baada kuongeza kina cha lango la kuingia Bandarini na eneo la kugeuzia Meli hali inayowezesha Meli kubwa kuingia bandarini kwa urahisi zaidi“, alisema.

Magomba ametumia fursa hiyo kuwakaribisha Wateja, Wadau na Umma kutembelea Banda la TPA katika maonesho hayo sambamba na kuendelea kutumia Bandari zetu katika shughuli za usafiri na usafirishaji ili kunufaika na fursa zilizopo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here