Buenos Aires, ARGENTINA
TOFAUTI na matarajio ya watu wengi Lionel Messi amesema, ataendelea kucheza soka ya Kimataifa baada ya kuongoza Argentina kutawazwa mabingwa wa Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 36 akiwa nahodha.
Nyota huyo wa Paris Saint – Germain (PSG) aliweka wazi hayo wakati alipofanya mahojiano na kituo cha Televisheni ha Tyc Sports, kilichopo nchini Argentina.
Messi atakayefikisha umri wa miaka 36 mwaka ujao, anaamini kuwa bado mchango wake unahitajika uwanjani akiwa na jezi ya Argentina.
“Napenda soka. Ndicho kitu ninachofanya. Nafurahia kuwa sehemu ya timu ya Taifa na natamani kuendelea kucheza mechi kadhaa za Kimataifa nikiwa mshindi wa Kombe la Dunia,” alisema Messi ambaye ndiye aliibuka mchezaji bora wa makala ya 22 ya fainali za Kombe la Dunia mwaka huu baada ya kupachika wavuni mabao saba na kuchangia krosi tatu zilizozaa mabao.
Aidha, Messi atakuwa na umri wa miaka 39 fainali zijazo za Kombe la Dunia zitakapofanyika nchini Amerika, Canada na Mexico, ambapo kocha wa timu ya Taifa ya Argentina alisema, angependa Messi awe sehemu ya kikosi chake wakati wa fainali hizo za dunia mnamo 2026.
“Kwanza kabisa, tunahitaji kumhakikishia nafasi katika kikosi kitakachowakilisha Argentina kwenye makala yajayo ya fainali za Kombe la Dunia,” alisema Scaloni.
“Iwapo anataka kuendelea kucheza, basi atakuwa pamoja nasi. Ndiye mwenye usemi wa mwisho kuhusu mustakabali wake kitaaluma. Ataamua iwapo atasalia kuwa mchezaji wa Argentina au la,” alisema.