Na Eleuteri Mangi
WATANZANIA na Afrika Kusini wanajukumu la kuwa vinara katika sekta za uchumi ili kuenzi historia ya nchi hizo mbili zilizoasisiwa na Viongozi wa Mataifa hayo; Mwalimu Julius Nyerere kwa upande wa Tanzania na Nelson Mandela kwa upande wa Afrika Kusini wakati wa harakati za ukombozi wa Afrika Kusini.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Utamaduni Dkt. Emanuel Temu, jijini Dodoma alipomwakilisha Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mohamed Mchengerwa katika Tamasha la Msimu wa Utamaduni wa Afrika Kusini na Tanzania ambalo limefanyika jijini humo likiwa na dhamira ya kuimarisha uhusiano na ushirikiano baina ya nchi hizo mbili.
“Mpaka mwaka 1994 tunajua kwamba nchi zote za Afrika zilikuwa zimepata uhuru tayari, na nchi yetu ilitoa mchango mkubwa sana katika kuhakikisha nchi hizi zinapata uhuru. Kufanyika kwa Tamasha la Msimu wa Utamaduni linakumbusha na kuwafundisha vijana wetu kufahamu historia halisi ya tulipotoka na namna gani tulishirikiana katika kupata uhuru wa nchi zetu,” alisema Dkt. Temu.
Dkt. Temu alisisitiza kuwa, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere aliamini kuwa hatuwezi kuwa huru peke yetu bila wenzetu kuwa huru, huo utakuwa uhuru wa mashaka.
Aidha, aliongeza kuwa wananchi wa nchi hizo mbili wanajukumu la kuendeleza mahusiano baina yao na amani iendelee kushamiri kwa kuwa walikuwa vinara katika harakati za ukombozi wa Bara la Afrika, sasa wananchi wa mataifa haya mawili wanajukumu la kuwa vinara katika sekta za uchumi kwa kuwa wanarasilimali za kutosha, nia wanayo, uwezo wanao na jukumu lilipo ni kutekeleza azma hiyo.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Utamaduni wa Afrika Kusini, Mcawe Mafu alisema Afrika Kusini wameanzisha tamasha hilo kwa lengo la kuwafundisha vijana historia ya nchi yao na kuwa Tanzania ni nchi yao kwa kuwa wapigania uhuru wa nchi yao walikaa hapa hadi walipopata uhuru na kuanza kurudi kwao miaka ya 1991 na 1992.
“Waafrika Kusini wanaijua nchi hii vizuri, Morogoro tulipewa ardhi bure Mazimbu na Dakawa na hapa Dodoma tulipewa ardhi Kongwa na Magagao Iringa, Waafrika Kusini waliishi nchi hii hadi miaka ya 1991 na 1992 ndipo tulipoanza kurudi nyumbani. Nawaambia Waafrika Kusini wanasema asante sana kwa ukarimu wenu,” alisema Mcawe Mafu.
Naibu Waziri huyo aliongeza kuwa, vitu vyote walivyojenga hapa Tanzania waliamua kuviacha kama shukrani zao kwa nchi hii ambapo ametolea mfano maeneo ya Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine Morogoro Kampasi ya Solmon Mahlangu (Mazimbu), Chuo cha ufundi Dakawa, shule ya sekondari ya Dakawa, hospitali pamoja na Shule ya Sekondari ya Kongwa iliyopo mkoa wa Dodoma.
Tamasha la Msimu wa Utamaduni wa Afrika Kusini na Tanzania linafanyika hapa nchini katika maeneo manne ikiwemo Dar es Salaam, Dodoma, Morogoro na Zanzibar na linafanyika kuanzia Novemba 17 hadi Desemba 4, 2022.