Trilioni 1.2 kutumika kuboresha elimu ya Sekondari

0

Na Angela Msimbira, URAMBO

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za` Mikoa na Serikali za Mitaa Angellah Kairuki amesema, Serikali itatumia takribani Shilingi Trilioni 1.2 katika kuboresha elimu ya sekondari nchini.

Kairuki ameyasema hayo wakati wa kuzungumza na wananchi wa Kata ya Kasisi, Halmashauri ya Wilaya ya Urambo mara baada kukagua ujenzi wa shule ya Sekondari ya Kasisi unaogharimu Shilingi Milioni 470.

Alisema, kiasi hicho cha fedha kitatumika ndani ya miaka mitano ya utekelezaji wa Mradi wa Kuboresha Elimu ya Sekondari (SEQUIP).

Kairuki alisema, Serikali imefanya tathmini ya shule Kongwe za msingi kwa ajili ya kuongezwa madarasa kukarabatiwa na kujengwa upya.

Alisema, kwa kutambua umuhimu wa elimu hasa katika maeneo ya pembezoni ambapo watoto wanatembea umbali mrefu kufuata elimu, Serikali imeweka mkakati wa kusogeza huduma hiyo karibu na wananchi. Pia, kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia nchini kwa kujenga miundombinu ya elimu.

“Tabora pia kuna Watanzania, kuna watoto wanaohitaji huduma, hivi kama atatembea umbali mrefu sana atakuwa na kiwango cha ufaulu unaotakiwa, hivyo kwa kutambua hilo tunasogeza huduma ya elimu karibu na wananchi,” alisema Kairuki.

Alisema, lengo la Serikali ni kuhakikisha hakuna kata inakosa shule ya sekondari ili kuhakikisha kila mtoto wa kitanzania anapata fursa ya upata elimu.

Aidha, Kairuki alitoa rai kwa wananchi kujitoa katika kusaidia shughuli za maendeleo ili kuunga mkono juhudi za Serikali na kuwataka wananchi kuhakikisha wanafanya kazi kwa bidii na kuzalisha ili Serikali iweze kukusanya mapato kwa ajili ya kuendeelea kuboresha huduma kwa jamii.

Kairuki aliwaomba wazazi kuwahimiza watoto wao kujikita katika masomo na kuhakikisha wanatoa muda kwa ajili ya kujisomea ili wanachofundishwa waweze kukielewa na kukitumia baadaye na kuwa na kizazi cha wasomi na wanaojitambua.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here