Na Mwandishi Wetu
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amechangia Shilingi Milioni 70 kwa Doris Mollel Foundation, ambapo Shilingi Milioni 20 ameitoa kuwasaidia watoto njiti kupitia Shirika hilo lisilo la Kiserikali na pia amenunua vifaa tiba vya kuwasaidia Watoto hao vyenye thamani ya Shilingi Milioni 50.
Akiongea katika tukio hilo, Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel amemshukuru Rais kwa kuchangia fedha hizo ambazo amezitoa mwenyewe kutoka kwenye mshahara wake, huku akiweka wazi kuwa, Serikali kupitia Wizara ya Afya itaendelea kuwasaidia Watoto njiti na Wanawake wanaojifungua Watoto hao.
Nae, Mkurugenzi wa Doris Mollel Foundation ambaye pia alizaliwa Mtoto njiti, Doris Mollel amemshukuru Rais kwa msaada huo ambapo alisema, ameutoa katika siku mwafaka, ambapo Doris Mollel Foundation iliitumia siku hiyo kutoa misaada mbalimbali.
Doris Mollel Foundation huadhimisha Siku ya Mtoto Njiti Duniani ambayo kwa kawaida huadhimishwa mnamo Novemba 17 kila mwaka, Shirika la Doris Mollel Foundation liliadhimisha kilele cha siku hiyo November 20, 2022 ambayo ilikutwa Siku ya Mtoto Duniani na yalifanyika katika viwanja vya Robanda, vilivyopo katika Wilaya ya Serengeti, Mkoani Mara.