Na Mwandishi Wetu
MKUU wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), Prof. Preksedis Ndomba amezipongeza Kampuni mfano tano za wanafunzi zilizofanya vizuri na kupewa tuzo ya ubora.
Pongezi hizo amezitoa kwenye hafla ya kukabidhi tuzo hizo iliyofanyika leo, Mei 20, 2026 ambapo Mkuu huyo ameweka msisitizo kuwa, kila mwanafunzi ni lazima ashiriki na aandike andiko la mradi wa kuanzisha kampuni za mfano.
Prof. Ndomba amewataka wanafunzi hao kutumia fursa hiyo muhimu kwa wakati huu ambao wapo chuoni hapo kwa kuwa wapo na wataalam ambao watawaongoza na kuwasimamia, jambo ambalo litawasaidia baadae watakapohitimu masomo yao.
“Tumieni muda huu mliopo hapa DIT kuandika na kuanzisha Kampuni, mkishatoka hapa huwezi kupata mtu wa kukufundisha kama ambavyo unafundishwa hapa,” alisema Prof. Ndomba.
Aidha, alisisitiza kuwa, ni lazima DIT iwe na wanafunzi walioiva ndani ya taasisi na hii inafanikishwa kupitia dhana ya mafunzo viwandani, ambapo alisema tangu mwaka 2016 DIT iliamua kujikita kwenye dhana hiyo na matunda yake yanaonekana sasa.
Hata hivyo, Prof. Ndomba ameeleza mkakati wa taasisi wa kuatamia makampuni yanayofanya vizuri ambapo DIT imetenga jengo kwa ajili ya kuwapatia ofisi ya kufanyia kazi, pia watakuwa wanafanya kazi zao kupitia Kampuni Tanzu ya taasisi inayoitwa DIT Company Ltd ili waweze kukua na kuwa vizuri kabla hawajaanza kujitegemea.
Kwa upande wake Magdalena Michael, mwanafunzi wa DIT ambaye ni Mtendaji Mkuu wa ABIOS Company Ltd ameelezea furaha yake baada ya kupokea tuzo na ameipongeza dhana hiyo ya mafunzo viwandani kwa kuwa inaongeza ujasiri na kuwapa mwanga wa kujiajiri kuliko kutafuta ajira.
Naye, John Charles Njunwa, Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Civic Innovations ambao kampuni yao imeandika andiko na kubuni mchoro wa daraja la kuvukia watembea kwa miguu kutoka DIT Kampasi Kuu kwenda upande wa pili wa bara bara ya Bibi Titi, ameipongeza taasisi na kuwataka wanafunzi wengine waanze kuandika maandiko waweze kuongeza ujuzi.