Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema ikiwa tafsiri na maana ya Demokrasia kwa Upinzani ni kuona CCM ikishindwa Uchaguzi, kupoteza Viti vya Udiwani, Ubunge na Uwakilishi, hiyo si tafsiri wala mantiki sahihi ya neno Demokrasia.
Aidha, CCM kimeapa hakiwezi kushindwa na Vyama vilivyoundwa kuanzia Mwaka 1992, kwa kudhani tayari viwe na nguvu za kukishinda chama kilichoshika Madaraka Miaka zaidi ya Sitini.
Matamshi hayo yametamkwa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis, alipozumgumza na Waandishi wa Habari ofisini kwake Kisiwandui Kisiwani Unguja.
Mbeto alisema, nguvu za chama chochote cha siasa duniani, ni umri na uimara wa chama hicho, Rasilimali Watu na Fedha, Mitaji na Vitega Uchumi, Sera makini, Oganaizesheni ilioshamiri na mtandao madhubuti wa kisiasa
Alisema, CCM ni chama kilichojijenga kimtandao kipo kila kona Tanzania, kina Rasilimali Watu, Mitaji na Vitega Uchumi, hivyo si jambo rahisi kudondoshwa na Vyama viliundwa Mwaka 1992.
“Ni ajabu kusikia Upinzani ukidai kura zake zinaibiwa. Vyama hivyo bado vichanga Kisiasa havina ubavu wa kushindana na CCM. Hata timu changa za Soka hazihimili mikiki mikiki dhidi ya Simba au Yanga Uwanjani,” alisema Mbeto.
Aidha, alisema bila kukitaja jina chama kimoja cha upinzani, alidai kimeweza kununua jengo jipya la Ofisi zake baada ya kulipwa ruzuku kutoka katika Serikali za CCM, huku chama hicho kikijigamba kina uwezo wa kuidondosha CCM.
Alipoulizwa iwapo Serikali za CCM zipo tayari kufanya mabadiliko ya Katiba, mifumo ya Uchaguzi, kitaasisi na sheria ya Uchaguzi, Mbeto alijibu kipo tayari ingawaje kusitokane na shindikizo au kwa vitisho.
“Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameahidi kabla hajaondoka madarakani mwaka 2030 Tanzania itapata Katiba mpya. Lakini hata ikipatikana Katiba, mabadaliko ya mifumo na sheria, upinzani haujapata na uwezo wa kuishinda CCM,” alieleza.
Katibu huyo Mwenezi alisema ikiwa neno Demokrasia kwa tafsiri ya upinzani hadi pale kishindwe uchaguzi, vyama hivyo vitasubiri kwa miaka mingi kwakuwa CCM bado kitaendelea kuungwa mkono wananchi na kuongoza dola.
“Nimemsikia Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Othman Masuoud Othmam akidai CCM kimejiweka madarakani. Muulizeni kimejiweka kivipi. Je, Uchaguzi haukufanyika? Vyama havikushuriki Uchaguzi, Tume ya Uchaguzi huikumtangaza mshindi ?,” alihoji Mwenezi huyo.
Mbeto alimtaja Mgombea huyo wa Urais Zanzibar kupitia ACT Wazalendo, hajawa na sifa za kumshinda Mgombea Urais wa CCM Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi, cha ajabu amekuwa akisimama na kudai ameibiwa kura.
“Ni kura zipi hizo alizoibiwa Othman. Yeye alikuwa wapi wakati kura zikiibiwa. Ziko wapi na kwanini hakuwakamata walioiba? Kama kuiba Kura jambo rahisi yeye na chama chake walishindwaje kuiba!,” alishangaa.
Hata hivyo, Mwenezi huyo alisema kwa nafasi ya Urais Zanzibar, alimtaja Othman kuwa Mwanasiasa mpya asiye na umaarufu ndani na nje ya ACT, kwa asili na historia ya Siasa za Zanzibar, si mtu anayetambulika na kukubalika.