Hali ngumu ya maisha ilimfundisha Xi Jinping kuwa ‘imara kama mlima’

0

BEIJING, China

RAIS Xi Jinping alizaliwa Beijing mwaka wa 1953. Kama vijana wengi wa zama zake, ambao familia zao zilikuwa wapinzani wa serikali, Xi alifanya kazi katika mashamba ya nafaka.

Hali ngumu ya maisha ilimfundisha Xi kuwa “imara kama mlima”. Kwa muda, alikuwa akilala kwenye ghala usiku na kufanya kazi vijijini wakati wa mchana. Leo, ghala hili limekuwa moja ya vivutio vya utalii vya China. Wakati huo huo, picha ya Xi imewekwa kwenye ghala moja, ambayo inaonyesha kuwa kiongozi huyo wa China alikuwa akisoma kitabu baada ya kazi ngumu.

Xi Jinping ni mmoja wa wanamapinduzi wakongwe na waasisi wa Chama cha Kikomunisti cha nchi hiyo. Baba yake alikuwa mmoja wa mashujaa wa mapinduzi na kizazi cha kwanza cha viongozi wa kikomunisti wa China.

Hivi karibuni, chama cha Kikomunisti cha China (CPC) kimemchagua Xi Jinping kuendelea kuwa Katibu wake Mkuu kwa muhula wa tatu katika kikao kilichomalizika Jumamosi na hivyo kumuidhinisha kuendelea kuwa rais wa China.

Mtandao wa ‘Pars today’ unaripoti kuwa, kikao cha 20 cha Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China kilifanyika Jumamosi chini ya uwenyekiti wa Xi. Wanachama pia walimchagua Xi kuwa Mwenyekiti wa Tume Kuu ya Kijeshi ya CPC.

Akizungumza katika kongamano la wawakilishi na wajumbe 2,338 walioalikwa kwenye kikao cha mwisho cha kongamano katika Ukumbi Mkuu wa Wananchi wa Beijing, Xi Jinping amesema, Kongamano la Chama cha Kikomunisti cha China limefikia malengo yake ambayo ni umoja wa fikra, kujiimarisha, kujiamini, kupanga njia na kuimarisha motisha.

Xi alidokeza kuwa, chama kinaendelea kwenye njia ya malengo yake baada ya karne moja ya jitihada.

Aliongeza kuwa: Tuna uhakika na uwezo wa kuumba miujiza mipya na mikubwa zaidi katika safari mpya ya enzi mpya, miujiza ambayo itaushangaza ulimwengu.

Kuchaguliwa kwa Xi Jinping kwa muhula wa tatu mfululizo tangu mwaka 2012 kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Kikomunisti cha China, cheo ambacho kinamhakikishia nafasi yake kwa muhula mwingine wa miaka mitano mfululizo kama rais wa nchi hiyo, ni ishara ya umaarufu wa Xi miongoni mwa viongozi wakuu wa chama wawawakilishi walioshiriki kwenye Kongamano la Chama cha Kikomunisti, ambalo hufanyika kila baada ya miaka mitano.

Kuamua mwelekeo wa kati na wa muda mrefu wa China katika nyanja za sera ya ndani na nje ni moja ya majukumu muhimu ya Kongamano la Chama cha Kikomunisti cha China. Aidha, uchaguzi wa Katibu Mkuu mpya wa Chama cha Kikomunisti kama mkuu wa chama tawala cha China ni hatua nyingine muhimu katika kongamano hilo.

Katika miaka kumi iliyopita, wakati Xi Jinping akiwa mkuu wa Chama cha Kikomunisti na pia kama Rais wa China, mwelekeo muhimu zaidi wa Beijing umekuwa katika sekta ya uchumi, ambao umeifanya nchi hii kuwa injini ya uzalishaji bidhaa duniani kote.

Rais Xi Jinping akihutubia kikao cha Chama cha Kikomunisti cha China. Sisitizo la Xi kuhusu uzalishaji unaozingatia mauzo ya nje na uendelezaji wa soko lengwa la bidhaa za China katika sehemu zote za dunia umepelekea wahusika wa taasisi zote za kifedha na kiuchumi za China kuzingatia kikamilifu mkakati huo.

Mnamo 2007, Xi alichukua nafasi ya Chen Lianglu, Katibu wa zamani wa chama huko Shanghai, kwa sababu ya ufisadi wa kifedha, na wakati huo huo akateuliwa kuwa mjumbe wa kudumu wa Ofisi ya Kisiasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti.

Mwaka 2012, Chama cha Kikomunisti cha China kilimchagua Xi Jinping kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Kikomunisti cha China na kisha akachukua nafasi ya Rais Hu Jintao tarehe 15 Novemba mwaka huo.

Mnamo mwaka wa 2018, Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China ilipiga kura ya kuondoa ukomo wa mihula miwili ya urais wa nchi hiyo, na kumruhusu Xi kubaki kubakia madarakani.

Bila shaka, ikumbukwe kuwa Xi ni mtu mwenye ushawishi mkubwa katika Chama cha Kikomunisti cha China, hivyo mwaka 2017, Kamati Kuu ya chama hicho ilipiga kura ya kujumuisha maoni na mitazamo yake katika katiba ya nchi.

Katika historia ya China ya kisasa maoni pekee yaliyowahi kuwekwa katika katiba ya nchi ni ya mwanzilishi wa Chama cha Kikomunisti Mao Zedong na Deng Xiaoping, ambaye alianzisha mageuzi ya kiuchumi katika miaka ya 1980.

Katika zama za uongozi wa Xi, China imeweza kuwa na uchumi wa pili kwa ukubwa duniani na amefanya mageuzi makubwa, ikiwa ni pamoja na kupunguza viwanda vya serikali visivyo na faida, kupunguza uchafuzi wa mazingira, pamoja na mpango wa miundombinu wa “Ukanda Mmoja, Njia Moja” wa mabilioni ya dola unaolenga kupanua uhusiano wa kibiashara wa China na dunia.

Wakati wa utawala wa Xi Jinping, China imeibuka kama dola linalojiamini zaidi katika upeo wa dunia. Maonyesho ya nguvu kubwa katika Bahari ya China Kusini, kukabiliana vilivyo na jitihada za kisiwa cha Taiwan kujitangazia uhuru pamoja na kutumia nguvu laini kupitia mabilioni ya dola za uwekezaji katika nchi za Asia na Afrika kwa lengo la kupanua ushawishi wa nchi hiyo duniani, ni miongoni mwa mafanikio ya utawala wa Xi.

Janga la virusi vya corona limeathiri uchumi wa China kama ulivyo uchumi wa nchi nyingine, lakini nchi hiyo inajaribu haraka kufidia mdororo wa ukuaji wa uchumi uliosababishwa na janga hilo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here