Nadharia za Kimagharibi haziwezi kufanyiwa majaribio Afrika

0

Na Emmaculate Mwalwego, OUT

TANGU kurejea kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa kwenye nchi zilizopo Kusini mwa Jangwa la Sahara mwanzoni mwa miaka ya 1990, hamasa za kisiasa kwa vyama vya upinzani kushika dola imekuwa ikishuka kwenye nchi nyingi.

Kwa maneno mengine, nguvu ya vyama vya pinzani ni dhaifu hata katika nchi ambazo haki za kisiasa zimeenda sambamba na kuheshimu uhuru wa raia katika kuchagua. 

Hata hivyo kumekuwa na mjadala kwa wasomi. Baadhi huamini kwamba kuzorota kwa vyama vya upinzani kunachangiwa kwa kiasi kikubwa na udhibiti wa viongozi waliopo madarakani. Wapo wanazuoni wanaoamini viongozi wengi waliopo madarakani hudhibiti taasisi za Serikali na mtiririko wa ufadhili.

Hali hiyo ya udhibiti imetoa upendeleo kwa vyama vinavyotawala na hivyo kusababisha nchi nyingi kutokuwa na mabadiliko. Wanazuoni wengine wenye mtazamo wa Kimagharibi huamini nadharia ya kwamba, rais anayeondoka madarakani ushindi wa chama tawala huwa kiduchu.

Bila shaka nadharia nyingi zimebuniwa Ulaya na zinafanya kazi kwa mazingira ya huko. Napenda niweke sawa kwamba, kwa kusema hivyo sina maana nadharia zote zinazobuniwa Ulaya haziwezi kutumika katika mazingira ya Kiafrika. Jambo la msingi nikujua kwamba, nadharia nyingi hazina nafasi katika kufanyiwa majaribio kwenye bara la Afrika.

Mathalani nadharia niliyoibainisha hapo awali kwamba, ushindi wa kiongozi fulani hutoa matokeo dhaifu kwa chama tawala endapo tu kiongozi huyo ataondoka madarakani kwa ukomo, kuzorota kwa afya, kwa mujibu wa sheria za chama chake.

Upo ushahidi wa dhahiri kwamba, baadhi ya nchi kiongozi anapong’atuka madarakani kwa sababu ya ukomo ulioainishwa katika katiba za nchi, hakuna athari inayosababisha chama husika kukosa fursa ya kuendelea kutawala kwa sababu tu kimesimamisha mgombea mwingine. Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeshiriki chaguzi sita zilizohusisha vyama vingi vya siasa.

Kati ya hizo, chaguzi tatu CCM imeingia kwenye mchakato wa kinyang’anyiro ikiwa na wagombea wapya. Mfano, uchaguzi wa mwaka 1995, CCM ilimsimamisha kwa mara ya kwanza hayati mzee Benjamin William Mkapa. Uchaguzi huo mzee Mkapa alishinda kwa kishindo na kumbwaga kwa kura nyingi mpinzani wake mkuu, Hayati Augustino Lyatonga Mrema kutoka NCCR Mageuzi.

Uchaguzi mwingine ni ule wa mwaka 2005, ambapo CCM ilimsimamisha mgombea mpya, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete aliyechuana vikali na Prof. Ibrahimu Lipumba kutoka Chama cha Wananchi (CUF). Katika uchaguzi huo Dkt. Kikwete alipata ushindi wa asilimia 80.28, Lipumba wa (CUF) alipata asilimia 11.68 na Freeman Mbowe wa Chadema alipata asilimia 5.88 ya kura zilizopigwa.

Uchaguzi wa mwaka 2015, CCM ilimsimamisha Hayati Dkt. John Pombe Magufuli na kupata ushindi wa asilimia 58.46, dhidi ya Edward Lowassa aliyepata asilimia 39.97 ya kura zote.
  

Matokeo haya yanatoa picha kwamba, ukomo wa kiongozi bado hauwezi kuwa sababu ya chama tawala kushindwa uchaguzi. Zipo sababu nyingine kama vile chama tawala kuingia katika uchaguzi mkuu kikiwa katika mgawanyiko.

Ukichunguza data za marejeo ya uchaguzi, utabaini kwamba uchaguzi mwa mwaka 2015, ndiyo uliokuwa na ushindani mkali baina ya chama tawala cha CCM na Chadema.

Sababu ya CCM kushinda kwa alama hizo kilitokana na kuingia katika uchaguzi mkuu kikiwa katika mpasuko wa kisiasa. Umoja wa kitaasisi ndani ya chama cha siasa, uandaliwa kukidhi malengo ya pamoja ya chama ya kila wakati.  

Chama cha siasa huwa na muundo na usimamizi unaojenga uhusiano kati ya viongozi wa chama na wanachama. Uhusiano huo hauwezi kuwa wa moja kwa moja kati ya wanachama wa kawaida na Mwenyekiti wa Taifa wa chama, hivyo kati kuna viongozi waandamizi wa chama ambao wao husimama badala ya viongozi wa chama ngazi ya Taifa. Jukumu la msingi la viongozi hawa ni kuuunganisha wananchama wa chini na wale wa juu. 

Kama kundi hili la kati litapuuzia matatizo ya kundi la wanachama na kushindwa ama kuyafikisha kwa usahihi au kutoyafikisha kabisa, daraja la mahusiano hulegea. Athari ya kulegea kwa daraja hilo, ni kuanguka kwa chama.

Kwa maneno rahisi, chama cha siasa kinapokuwa na ushirikiano na mahusiano mazuri, huwa na nguvu kuanzia uongozi wa juu, wa kati hadi kwa wanachama wenyewe. Hivyo, kukosekana kwa umoja ndani ya CCM kulisababisha chama hicho tawala kuingia katika uchaguzi kikiwa katika migawanyiko. 

Huo ndio wakati ambao CCM ilikosa nguvu ya kisiasa. Chama kilikosa watu wa kuwashawishi wananchi kwa misingi ya ustadi wao binafsi wa kutumia maarifa, mawazo na hata utaalamu nakadhalika katika kuwajengea picha halisi wananchi kwa lengo la kuimarisha nguvu ya chama.

Baadhi ya viongozi wa wakati ule walipofanya mikutano ya hadhara walikuwa wakitumia muda mwingi kuwashambulia wanaCCM wenzao kutoka kundi jingine. Hivyo, taswira ya CCM kwa wananchi kwa wakati huo ilioonekana kuwa hasi. Kutokana na hilo, hoja kwamba ukomo wa uongozi husababisha kushuka kwa haiba ya chama kwa umma, haina ukweli. 

Kama nilivyodokeza hapo awali kwamba, baadhi ya wanazuoni wa kimagharibi huamini kwamba mabadiliko ya kisiasa lazima yaletwe kwa chama kinachotawala kuondoshwa madarakani. Mtazamo huu ni dhaifu. Ni dhaifu kwa sababu, wakati mwingine chama cha siasa hushindwa kutokana na udhaifu wa viongozi wa chama chenyewe.

Kwa mfano, wanasiasa wanapewa nafasi ya kuongoza, lakini badala ya kuwatumikia wale waliowapa nafasi ya kuwaongoza, hutumia muda mwingi kuhamasishana katika kususia mikutano ya bunge, kugomea bajeti za serikali. Kutumia muda mwingi kulumbana na wanasiasa wengine kwenye mitandao ya kijamii mfano wa waimba taarabu za mipasho.

Unapofika wakati wa uchaguzi mwingine, wananchi wanahoji kile ulichokifanya katika kipindi cha miaka mitano kuwahusu wao. Mgombea hana cha kujibu. Mgombea wa aina hii lazima atafute maneno ya kuhalalisha kushindwa kwake ili wakati mwingine apate nafasi ya kugombea tena. Kukubali kushindwa kuna maana kwamba haiba yake kisiasa imeshuka.

Hivyo, hoja ya kushindwa kwa vyama vya upinzani hutokana na ukandamizwaji wa demokrasia kunakofanywa na viongozi waliopo madarakani haina mashiko. Ukweli ni kwamba wakati mwingine huchangiwa na viongozi wa vyama husika wa vyama vya upinzani. 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here