Uchumi wa China utashinda uchumi
wa Marekani itakapofika 2028?

0

Na Igamanywa Laiton

MNAMO Oktoba 1934 maelfu ya waume kwa wake, wanajeshi, wakulima na walalahoi kutoka China Kaskazini, kati na Kusini waliungana na kuanza safari. Ni safari ya maumivu ambayo iliwalazimu wakatishe katika mito hatari na mikubwa yenye upana wa makumi ya Kilometa.

Ni safari ambayo ilikuwa ikiwalazimu kupita katika sehemu zenye watu wenye chuki dhidi yao, safari ambayo iliwalazimu kukatiza katika milima mirefu yenye baridi kali na waliianza wakiwa tayari dhaifu; walikuwa hohe hahe bila chakula cha kutosha, madawa, nguo na viatu vya kuwasaidia njiani dhidi ya mazingira ambayo si rafiki.

Ilikuwa ni safari ya Kimapinduzi na kihistoria ambayo ilianza Oktoba 16, 1934 huko katika jimbo la Jiangxi chini ya Bo Gu na Otto Braun na watu 160,000, kabla ya kuungana na msafara mwingine ulioanzia katika jimbo la Hunam chini ya Mao ze Dong.

Mapinduzi haya yalianza baada ya wakulima waliokuwa wamechoshwa na utawala unaotajwa wa kidhalimu wa Kai Sheki Cheng. Utawala ambao uliwapa mgongo wananchi masikini na kuwageukia mabepari. Mambo hayo yalichochea ugumu wa maisha na kusababisha kudorora kwa uchumi, utawala bora na ustawi wa kijamii.

Wakiwa wamechoka, wananchi kutoka katika vijiji mbalimbali walianza safari iliyokuja kuzaa kile kilichokuja kujulikana kama ‘Maandamano Marefu/Makubwa ya China.’ Kati ya watu 160,000 waliotoka Jangxi na kuungana na maelfu wengine waliotoka Hunam, ni 20,000 pekee ndiyo waliofika mwisho wa safari, wengine waliuawa ama kupoteza maisha kwa njaa ama kwa sababu nyingine.

Inasemekana, wakiwa njiani mke wa Mao alifikia katika kilele cha uchungu na kujifungua, lakini kwa kuwa safari ilikuwa haijafika mwisho, iliwabidi wamuache mtoto akiwa na siku kadhaa katika kijiji kwa mwanakijiji wasiyemfahamu. Inasemekana Mao hakuwahi kuonana tena na huyo mtoto wake. Katika safari hiyo, Mao mwenyewe alivunja rekodi ya kuogelea kwa kuvuka mto wenye urefu wa zaidi ya Kilometa 14.

Mwaka 1935 Mao aliandika: “Maandamano Marefu yametuzalia Azimio ambalo ni msingi wa Taifa letu, maandamano haya yameionesha dunia kuwa Jeshi letu (Red Army) ni jeshi imara na ni njia pekee inayoelekea katika Ukombozi.”

Safari hii ya maandamano iliishia kwa kuleta Mapinduzi katika nchi ya China kwa mkulima na mlalahoi kupewa heshima yao iliyokuwa imepotea baada ya kuwa wametupwa na serikali iliyopita ya Komitang kwa muda mrefu. Mapinduzi haya yalizaa Chama tawala imara cha Watu wa China (CPP), chama kilichoasisi falsafa ya ujenzi wa Taifa la China ya sasa, na ni chama pekee kilichodumu madarakani hadi leo hii.

Kwa sasa China ni Mtawala mwenye nguvu ajaye baada ya Marekani na Uingereza. Katika mwaka 2017 Uchina ilikuwa ya pili kwa kuwa na viwango vya juu vya utiririkaji wa soko la mtaji la uwekezaji nyuma ya Marekani. Leo hii China inasimama kama nchi mfano wa mafanikio. Mafanikio ambayo yalianza kwa uchungu na kujitoa mhanga kwa makabwela na walalahoi wakulima na wafanyakazi wa hali ya chini.

Afrika ni bara ambalo linategemea biashara na China. Ni nchi moja tu ambayo haina ushirikiano wa kibiashara na China ambayo ni eSwatini (zamani Swaziland). China ndiyo Taifa lenye ushawishi mkubwa kibiashara Afrika baada ya kuipiku Marekani zaidi ya miaka 10 iliyopita.

Kwa ujumla, thamani ya biashara baina ya China na Afrika kwa mwaka 2017 ilifikia kiasi cha Dola Bilioni 170 kutoka Dola Bilioni 10 mwaka 2000.

Taarifa kutoka mtandao wa CRI zinaonyesha kuwa, barani Afrika, China kwa sasa ni mfadhili mkubwa wa miradi ya miundombinu, mingi imekamilika, na mingine inaendelea na miradi mingi zaidi imepangwa. Miradi hii inaweza tu kuendelezwa ikiwa misingi ya kiuchumi ya Beijing yatabaki imara.

Umuhimu wa Pendekezo la ‘Ukanda Mmoja, Njia Moja’ kwa Afrika ni wazi kwa wote, kwani hadi sasa nchi 42 za Afrika zimejiunga na pendekezo hilo. Huu ni ushuhuda tosha kwamba, Mataifa mengi ya Afrika yanaona haja ya miundombinu bora, ambayo bado inaonekana kama kikwazo kikubwa cha maendeleo katika eneo hilo.

Baadhi ya miradi ambayo imekamilika chini ya Pendekezo la Ukanda Mmoja, Njia Moja, ni pamoja na barabara kuu ya Cherchell Ring Expressway nchini Algeria, reli inayounganisha Addis-Ababa na Djibouti, Bandari ya Doraleh nchini Ethiopia, reli ya Mombasa – Nairobi ya Kenya, Daraja la Maputo – Katembe nchini Msumbiji, reli ya Lagos – Kano nchini Nigeria, na barabara kuu inayounganisha uwanja wa ndege wa Entebbe na mji wa Kampala nchini Uganda.

Ni muhimu kusema kuwa, uwekezaji wa China barani Afrika umeongezeka kwa kiasi kikubwa tangu pendekezo hilo lilipozinduliwa. Ripoti ya hivi karibuni ya kampuni ya McKinsey inakadiria kuwa, zaidi ya makampuni 10,000 ya China yanafanya kazi barani Afrika, na ripoti mbalimbali zinaonyesha uwekezaji huu umekuwa na matokeo mazuri barani humo.

Nchini Kenya, ujenzi wa barabara kuu inayounganisha Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta na sehemu za Magharibi mwa Nairobi unaendelea, na unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa 2021. Miradi hii michache ni baadhi ya maendeleo ya miundombinu inayojengwa kote barani, na inatoa fursa kubwa za uwekezaji.

Mambo haya yanafanyika wakati China imefichua kwamba, tayari imetoa robo tatu ya ahadi ya fedha iliyotolewa kwa Afrika mwaka 2018. Waziri msaidizi wa Mambo ya Nje wa China Deng Li amesema, zaidi ya asilimia 70 ya Dola za Marekani Bilioni 60 za msaada wa kifedha ulioahidiwa na China katika Mkutano wa FOCAC uliofanyika Beijing tayari zimewasilishwa au kupangwa kutolewa.

Kutokana na hali nzuri ya uchumi, Deng alibainisha kuwa China itatafuta njia mpya ya ushirikiano na Afrika inayolenga miradi ambayo itabadilisha hali ya maisha ya watu. Amesema China ina hamu ya kushiriki miradi ambayo “inazalisha mamilioni ya ajira, kuboresha maisha, kukuza uchumi wa kidijitali, kupunguza umaskini, na kuimarisha sekta ya viwanda.”

Huku ikiwa na watu Bilioni 1.4, China inajivunia asilimia 20 ya idadi ya watu duniani, na raia wake wanapoinuka kiuchumi, pia matumizi yao yanaongezeka, na makampuni yatajitahidi kuuza bidhaa zao kwenye soko hili, ambalo ni kubwa zaidi duniani. Nchi nyingi zinazoendelea bado ni wazalishaji wakuu wa bidhaa za kilimo na maliasili, na kuongezeka kwa mahitaji ya bidhaa hizi nchini China kutaboresha bei za bidhaa hizo.

Hivi sasa Afrika inahitaji kichocheo cha ukuaji, na kupitia kuendelezwa kwa sera imara ya kiuchumi, China inaweza kutoa msukumo huo kwa ukuaji wa uchumi wake. Je, unafahamu kuwa uchumi wa China unaelekea kuwa namba moja duniani katika miaka 8 ijayo?

Ripoti iliyotolewa na Kituo cha Utafiti wa Uchumi na Biashara CEBR inasema, uchumi wa China utashinda uchumi wa Marekani itakapofika mwaka 2028, miaka mitano kabla ya utabiri wa awali, kutokana na mgogoro wa uchumi unaosababishwa na janga la Corona. CEBR inasema, kando na China kushughulikia janga hilo kwa ufanisi zaidi kuliko Mataifa ya Magharibi, athari za ukuaji wa uchumi kwa nchi hizo zitadumu kwa muda mrefu.

Taarifa zilizotolewa na Umoja wa Mataifa mwanzoni mwa mwaka huu zinaonyesha kuwa, China imeipiku Marekani kama eneo linalolengwa na uwekezaji wa moja kwa moja wa kigeni. Nusu ya uwekezaji mpya nchini Marekani kutoka katika makampuni ya kigeni, ulishuka mwaka uliopita hatua iliyosababisha Taifa hilo kupoteza nafasi yake ya kwanza.

Kwa upande mwingine, takwimu hizo zinaonyesha uwekezaji wa moja kwa moja katika kampuni za Wachina uliongezeka kwa asilimia 4, na kulifanya Taifa hilo kuchukua nafasi ya kwanza duniani. Kupanda kwa China kunaonesha ushawishi wake katika sekta ya kiuchumi duniani. China ilijipatia kipato cha Dola Bilioni 163 mwaka uliopita, ikilinganishwa na Dola Bilioni 134 zilizoingia Marekani, Mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu Biashara na Maendeleo (UNCTAD) ulisema katika ripoti yake.

Mwaka 2019, Marekani ilipokea Dola Bilioni 251 kupitia uwekezaji wa moja kwa moja wa kigeni, huku China ikijipatia Dola Bilioni 140. Huku China ikiwa katika nafasi ya kwanza kwa uwekezaji mpya wa kigeni, Marekani bado inatawala katika uwekezaji wa jumla kutoka mataifa ya kigeni.

Hii inaonyesha miongo ambayo imetumia kama eneo la kuvutia zaidi kwa wafanyabiashara wa kigeni wanaotafuta kupanua biashara zao ng’ambo. Lakini, wataalamu wanasema takwimu hizo zinasisitiza hatua ya China kuelekea katikati mwa uchumi wa ulimwengu ambao kwa muda mrefu umetawaliwa na Marekani, Taifa lenye uchumi mkubwa zaidi duniani.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here