Jukumu la kijana katika kujiandaa kuwa na uzee mwema

0

Na Lion Mangole

BAADA ya wazazi kumlea mtoto hadi kufikia umri wa ujana, jukumu la kutambua na kusimamia misingi mizuri ya kufikia ndoto za kuwa na uzee mwema litakuwa ni jukumu lake mtoto/ Kijana. Kijana anatakiwa ajenge maisha yake kwa kutazama misingi aliyowekewa na wazazi wake, mara nyingi vijana wanafanya makosa makubwa kwa kudharau misingi mizuri waliyowekewa na wazazi wao.

Kujenga nje ya msingi wa wazazi ni jambo linaloweza kumgharimu kijana katika maisha yake ya baadae. Inawezekana wazazi wamemlea kijana katika mazingira mema sana, lakini baadae kijana akayaharibu yeye mwenyewe. Ujana ni nafasi nyingine adimu ambayo mtu anatakiwa aitumie vizuri ili kuamua hatima ya uzee wake. Vijana wengi wanasahau kama siku moja watazeeka, na ndio maana huishi maisha ya kushangaza na ya hatari sana.

Aidha, kuyatumia vibaya maisha ya ujana wao, ikiwa ni pamoja na kutumia fedha vibaya pamoja na afya zao kuzihatarisha kutokana na aina ya maisha wanayoishi. Kwa mfano uvutaji wa sigara, bangi, na madawa ya kulevya unywaji wa pombe umalaya na uasherati kwa ujumla, pamoja na maisha ya anasa yaliyopitiliza.

Yote haya yanamuhatarisha kijana. Wito wangu kwa vijana ni huu, mnatakiwa kujua kuwa, ujana ni wakati muhimu sana wa kuamua hatima ya uzeeni, hivyo msiutumie ujana wenu vibaya maana mtakuja kuujutia baadae.

Ndoa; Hii ni hatua inayotakiwa kufuatwa kwa umakini sana na kijana. Ndoa ni moja ya jambo muhimu sana linaloambatana na uzee, aidha mwema au mbaya. Watu wengi wanafanya makosa makubwa hasa pale wanapofikia kuamua kuingia katika maisha ya ndoa.

Hakuna kazi ngumu kama ya kuchagua mtu atakayeingia katika maisha ya ndoa na wewe. Mwenzi wa ndoa ni sehemu ya maisha yako, hivyo unapoamua vibaya kuhusu nani atakuwa mwenzi wako katika ndoa, unafanya kosa litakalochangia uufikie uzee mbaya.

Aina ya kazi; Katika vitu vinavyoweza kuchangia maisha yetu ya uzee kuwa mema au mabaya ni aina ya kazi. Ijapokuwa kazi ni muhimu sana katika maisha yetu, lakini ni vema tujue sio kila kazi inaweza kuwa rafiki katika maisha yetu hasa kiafya.

Mtu anaweza kujitahidi sana ili awe na maisha mazuri yatakayo mfikisha katika uzee mwema, lakini maamuzi ya kazi gani atafanya nayo inaweza kuwa ni tatizo jingine.

Mara nyingine watu wengi wanalazimika kufanya kazi za hatari au zinazoweza kuchangia kuyaharibu maisha yao, lakini kwa kuwa hawajaweza kuona kazi nyingine au hawakupata kazi nyingine baada ya kutafuta sana, hivyo wanaamua kufanya kazi yoyote.

Utafiti wangu umebaini, karibu asilimia 90 ya watu, wanafanyakazi ambazo hawakupanga kama wangezifanya, bali maisha yanawalazimisha kufanya hizo kazi. Sisemi usifanye kazi, bali mada hii ikusaidie kujua mambo yanayochangia kuharibu maisha yako ya uzeeni.

PONDA MALI KUFA KWAJA! AU UZEE WAJA?

Kuna msemo uliosikika kwa miaka mingi sana ukisemwa na watu wengi wasio na ufahamu. Mara nyingi husema “ponda mali kufa kwaja” au utasikia wakisema hivi “vunja mifupa wakati meno ipo” Misemo hii ina maanisha kuwa uzee haupo ila kuna kifo tu, jambo ambalo si kweli.

Watu wengi wanasahau kama kuna uzee, ila wanakumbuka kifo tu, aidha naweza kusema hivi watu wengi wanaogopa kufa zaidi kuliko kuogopa uzee. Kijana mwenye busara anastahili kuogopa sana uzee mbaya, kuliko hata kifo. Ni lazima kijana afanye jitihada kuhakikisha anapozeheka, basi awe amejiandaa vizuri ili asiteseke.

Pale mtu anapoponda mali katika ujana wake bila kujiwekea malengo ya uzeeni, anajitengenezea jehanamu ya nje. Lakini pia tunapaswa kujiuliza hivi, iweje watu wanasahau, au wapuuze uzee na kuona kama haupo ila kujihami kwa ajili ya kifo tu? Tunagundua kuwa ni ujinga ndio unaowadanganya.

Msemo wa ponda mali kufa kwaja, ni msemo unaowapofusha macho au fikira zao ili wasiweze kuwa na tahadhari katika kutumia vizuri mali au fedha zao, hatimaye hujikuta wamemaliza fedha na mali zote na maisha bado yanaendelea na uzee umewakuta watupu. Mimi nataka kumalizia kwa wito huu kwa vijana wote, wabadilishe msemo huo na sasa wase hivi “tunza mali/fedha na afya yako maana uzee upo.

TAKWIMU ZA MAUAJI YA VIKONGWE, NA UKATIRI

Idadi ya Vikongwe Wanaouawa kila mwaka nchini sasa yafikia 500….TANZANIA inatajwa kuwa nchi ya pili kati ya mataifa 91 duniani yanayodaiwa kuongoza kwa usalama duni wa maisha ya Wazee. Hii inatokana na kile kinachodaiwa kuwa nchi yenye mbinu hafifu katika kudhibiti uharamia huo.

Nchi inayoifuata baada ya Tanzania kiudhaifu ni Pakistan. Inaelezwa kwamba Pakistan ni moja ya Mataifa ambayo kwa kiasi kikubwa sera zake za kiuchumi na kijamii, zimeathiriwa mno na migogoro ya kivita. Utafiti unaonyesha kwamba nchi ya Sweden ndiyo inayoongoza kati ya nchi hizo 91 duniani kwa kulinda usalama wa wazee.

Hii inatokana na usimamizi thabiti wa sheria zake kama nchi. Ikumbukwe kwamba Desemba 10, 1948, Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa, lilipitisha Kanuni za Kulinda Haki za Binadamu ambazo kila nchi inalazimika kuzitekeleza kwa ajili ya usalama wa raia wake, wakiwemo wazee.

Nchini Tanzania, inaelezwa kwamba zaidi ya wazee vikongwe 500 huuawa kikatili kwa kukatwa mapanga na silaha nyingine za jadi kila mwaka. Licha ya kwamba mauaji ya aina yoyote dhidi ya binadamu hayakubaliki, lakini idadi ya wazee 500 wanaouawa, ni sawa na wastani wa wazee 41 wanauawa kila mwezi nchini.

Serikali inaonekana kupata kigugumizi cha kutungwa kwa Sheria ya Wazee, licha ya kuwepo kwa Sera ya Wazee iliyopitishwa mwaka 2003. Hata hivyo, inaeleweka kwamba sera ni sera tu, haiwezi kuwa sheria. Ndiyo maana nchi yoyote haiwezi kuongozwa kwa sera bila kuwa na sheria.

Katika Mkoa wa Mwanza kwa mfano, mauaji ya wazee vikongwe yamekithiri zaidi katika Wilaya ya Magu. Serikali katika wilaya hii imeshindwa kabisa kudhibiti vitendo hivyo vya kikatili na kinyama kutokana na baadhi ya wananchi wake kuamini katika imani za kishirikina Takwimu na taarifa ya utafiti uliofanywa na Shirika la Kutetea Haki za Wazee la Maperece, lenye Makao makuu yake wilayani Magu, zinaonyesha kwamba kati ya mwaka 1998 na 2001 kulikuwepo na matukio ya kikatili 17,220 dhidi ya Wazee.

Kati ya matukio hayo, Wazee 1,746 waliuawa. Hii ni hali isiyokubalika. Ni hali inayopaswa kulaaniwa na jamii nzima ya Watanzania. Kwa upande wake, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), katika Ripoti yake ya mwaka 2009, inaonyesha kwamba wanawake vikongwe takriban 2,583 waliuawa katika mikoa minane hapa nchini, ikiwa ni wastani wa mauaji ya vikongwe 517 kila mwaka.

Kwa mujibu wa Ripoti hiyo ya LHRC, mikoa inayoongoza kwa mauaji hayo ni pamoja na Mwanza, Shinyanga, Mara na Kagera, huku kwa Mkoa wa Shinyanga pekee, ikidaiwa kwamba vikongwe wanawake takriban 241waliuawa kati ya Januari 2010 na Juni 2011.

Mkurugenzi Mkuu, Ofisi ya Takwimu Tanzania, DkT. Albina Chuwa amewahi kukaririwa na vyombo vya habari akibainisha kwamba, asilimia 5.6 ya watu wote nchini ni Wazee. Kwa mujibu wa Dkt. Chuwa, asilimia kubwa ya jamii hiyo ya Wazee inapatikana katika Mikoa ya Kilimanjaro, Mtwara, Lindi na Pwani, huku mikoa ya Dar es Salaam na Mjini Magharibi Unguja, ikiwa ndiyo mikoa pekee nchini yenye asilimia ndogo ya wazee wenye umri wa zaidi ya miaka 60.

Aidha, baadhi ya Ripoti za Ofisi hiyo ya Takwimu nchini, zinaonyesha kwamba mwaka 2012/2013, idadi ya Wazee wenye umri wa zaidi ya miaka 60 walikuwa wanakadiriwa kufikia Milioni mbili, huku asilimia 82 kati ya Wazee wote hao wakiishi vijijini.

Shirika binafsi la Tanzania Mission to The Poor and Disabled (PADI), linalofanya shughuli zake mkoani Iringa, chini ya Mkurugenzi wake Isikaka Msigwa, linasema Serikali bado haijadhititi vya kutosha katika kudhibiti mauaji hayo ya Wazee kama ilivyo kwa baadhi ya nchi za Bara la Afrika.

Kwa mujibu wa baadhi ya taarifa za shirika hilo, baadhi ya Wazee nchini hufariki dunia kwa njaa pamoja na kukosa huduma za matibabu hospitalini, baada ya baadhi yao kupimwa na kisha kuambiwa na madaktari wao wakanunue dawa katika maduka ya dawa wakati hawana hata senti tano mifukoni mwao.

Kwa mfano, taarifa za PADI zinasema mwaka 2013 pekee, watu 17 waliripotiwa kuuawa kikatili kwa imani zinazoshabihiana na ushirikiana katika Wilaya za Ludewa, Wanging’ombe, Makete na Njombe. Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, Kanuni ya Adhabu, Ibara ya 24 inasema: “Pale mtu anapomshauri mtu mwingine kutenda kosa, na kosa likatendeka baada ya ushauri huo, mtu huyo aliotoa ushauri huo itachukuliwa kuwa yeye aliyetoa ushauri ndiye ametenda.

Kadhalika, Ibara ya 25 ya Sheria Na. 55 ya mwaka 1963, nyongeza ya 6 Na. 31 ya mwaka 1997, nyongeza Na. 9 ya mwaka 2002, miongoni mwa adhabu zinazotakiwa kuchukuliwa na Mahakama dhidi ya Mshauri wa Mauaji, ni pamoja na kunyongwa kwa kitanzi hadi kufa au kifungo cha maisha jela.

Aidha, Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, Sura ya 39, Ibara ya 60 (1), inasema: “Ofisa Polisi yeyote Msimamizi wa Kituo cha Polisi au Ofisa Polisi yeyote anayepeleleza kosa, anaweza kuendesha gwaride la utambulisho kwa madhumuni ya kuhakikisha kama shahidi anaweza kumtambua mtu anayetuhumiwa kutenda kosa.

Katika Sheria na Ibara hiyo ya 60, kifungu cha Nne (4), kinaeleza kwamba mtu yeyote ambaye bila sababu halali au za msingi, anakataa kuhudhuria na kushiriki katika gwaride la utambulisho, atakuwa na hatia ya kosa, na atawajibika akitiwa hatiani kwenda jela kwa kifungo kisichozidi miezi sita, kulipa faini au vyote viwili kwa pamoja.
mauaji haya ya kikatili kwa Wazee na Vikongwe wa nchi yangekomeshwa kabisa.

Wakati Serikali ya Tanzania ikiendelea na danadana kibao katika kutunga sheria kwa ajili ya kuwalinda na kuwatunza wazee, mataifa mengi ya Ulaya na baadhi ya Afrika, yamejipanga kila mwaka kuwekeza zaidi kwenye usalama wa Wazee.

Kutokana na hali hiyo, upo ulazima sasa kwa Serikali kuweka mikakati maalumu kwa ajili ya kutokomeza kabisa vitendo vya mauaji ya Wazee, pamoja na kutunga Sheria ya Wazee itakayoipa nguvu za kisheria Sera ya Wazee ya mwaka 2003, ambayo pamoja na mambo mengine, inamtaja mzee kama hazina ya hekima, nguzo ya malezi ya watoto na nguzo ya uchumi.

Kama hivyo ndivyo, basi Wazee wana kila sababu ya kuenziwa na kulindwa usalama na afya zao, kwa sababu Tanzania hii tunayojivunia kwa sasa, imefikishwa hapa ilipo kwa juhudi na michango ya kizalendo ya Wazee. Mwisho. Chanzo cha Taarifa ni: Idadi ya Vikongwe Wanaouawa kila mwaka nchini sasa yafikia 500…Fikra Pevu. http://www.fikrapevu.com/.

*Mwandishi wa Makala hii ni Mchungaji wa Kanisa la MGCT. Nyantira Kitunda Dar es salaam. Anapatikana kwa simu 0717528272. Email.kusomavitabu@gmail.com.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here