Na Cecilia Mwashihava
UTALII wa kutembelea hifadhi mbalimbali Duniani, ni njia pekee ya kuzitambulisha na kuwa moja ya njia kuu za ongezeko la Pato la Taifa husika. Nchini Tanzania tuna utajiri mkubwa wa vivutio vya utalii zikiwemo mbuga za wanyama na hifadhi tengwa za Taifa.
Hifadhi ya Tarangire ni moja ya Hifadhi kubwa inayoendelea kuipaisha Tanzania katika ramani za utalii na kutembelewa na watalii toka nchi mbalimbali Duniani. Uzuri wa Tarangire ndio unaofanya nitamani na wewe ujifunze leo kupitia makala hii ya kuhamasisha na kutambua utajiri mkubwa tulionao.
Hifadhi ya Taifa ya Tarangire inapatikana katika mkoa wa Manyara. Mkoa wa Manyara unapakana na Arusha, Shinyanga na eneo karibu na mipaka ya Kenya. Mbali na sifa ya uwepo wa ziwa Manyara, lakini ina sifa kubwa ya uwepo wa hifadhi kubwa ya Tarangire. Hifadhi hii ina ukubwa wa Kilometa za mraba zipatazo 2850.
Pengine watu wengi hawafahamu asili ya jina ‘Tarangire’ limetokana na nini? Jina hili Tarangire limezaliwa kutokana na mto Tarangire. Mto huu Tarangire ni mto unaopita kati kati ya hifadhi hii na unayo sifa ya kutokauka kipindi chote cha majira ya mwaka.
Pili, ni mto unaotoa chanzo kikuu cha maji kwa viumbe waishio. Wanyamapori na mimea hifadhini inafaidika na uwepo wa huu mto. Asili ya mto huu ni Nyanda za Juu za mto Kondoa ulio katika jiji la Dodoma ulio na urefu wa Kilomita zipatazo 120 na humwaga maji yake katika ziwa Burunge.
Hifadhi ya Tarangire ina muda mrefu toka kuanzishwa kwake. Hifadhi ya Tarangire ilianzishwa toka mwaka 1970 na kutambulishwa rasmi kama Hifadhi ya Taifa mwaka huo huo. Lakini, kabla ya mwaka 1970 hifadhi hii ilitambulika kama “Pori la Akiba la Wanyamapori”.
Kutambulishwa kwake kama Tarangire, kumeipa sifa kubwa hii hifadhi nchi nyingi Duniani. Soko la nyama wa pori hufanyika Duniani kote kwa vibali maalumu ili kuepusha ujangili unaoweza kupoteza au kuleta utowekaji wa baadhi ya wanyama walio hatarini kupotea Duniani.
Jiografia ya hifadhi ya Tarangire ina maumbile yenye mvuto wa pekee. Hifadhi inajumuisha uwepo wa Mto Tarangire, Kanda za Uoto wa asili, Maeneo yenye ardhi oevu, Vilima, Majabari ya mawe, miti mingi na Mibuyu mikubwa yenye kuvutia hifadhini kwa maumbo yake makubwa ya kustajaabisha.
Hifadhi hii imesheni vivutio vikuu kama chatu wenye sifa ya pekee. Chatu hawa ni wale chatu wapandao juu ya miti. Vivutio vingine ni Migunga mwamvuli, Makundi makubwa ya Tembo, Mibuyu mikubwa, aina za ndege mbalimbali na wanyama mbalimbali kama vile; Pundamilia, nyati, swala, twiga, nyani, ngedere, kuro, Kongano, pofu, digidigi na wengine wengi.
Hifadhi ya Taifa ya Tarangire inasifika maeneo mengi Duniani kuwa moja ya hifadhi yenye makundi makubwa na mengi ya Tembo kuliko hifadhi nyingine zote Tanzania nap engine maeneo mengine Duniani. Idadi ya tembo wanaopatikana katika hifadhi hii ni kubwa kwa uwiano na eneo la hifadhi.
Tembo hawa huishi kwa makundi makundi (familia) hivyo ufikapo hifadhi ya Tarangire utaona makundi mengi ya tembo hao na utafurahishwa na jinsi waishivyo. Ajabu jingine ni kujionea tembo aliyezaa mapacha (wawili) na tembo wadogo hao wamekua vizuri.
Hifadhi ya Tarangire ina miti mingi na mikubwa ya mibuyu. Mibuyu hii inasadikika kuwa na umri wa miaka ipitayo zaidi ya elfu nane (8000). Mibuyu hii husaidia si tembo pekee ila wanyama wengine wote kujipatia maji kipindi cha kiangazi au ukame. Wanyama hujipatia hifadhi ya maji kupitia magome ya mibuyu hii.
Mto Tarangire ndio chanzo pekee kikubwa na cha uhakika cha maji kwa wanyamapori ndani hifadhini. Mto huu hutiririsha maji yake kwa kipindi chote cha mwaka. Hivyo katika kipindi cha kiangazi hupelekea mahamisho ‘long term migration’ ya wanyama kama pundamilia na nyumbu ndani ya hifadhi kutoka maeneo mbalimbali.
Katika kipindi cha masika maji huwa mengi, hivyo kupelekea wanyama kutoka kama nyumbu na pundamilia kutoka na kwenda maeneo mengine kujipatia chakula na maji. Hifadhi ya Taifa ya Tarangire ni hifadhi nzuri sana na yenye mandhari inayovutia watalii nje na ndani.
Pia, ina wanyama wengi sana pamoja na ‘The Big four’ ambao ni Simba, chui, Nyati (mbogo) pamoja na tembo. Hifadhi hii inapambwa na ndege wazuri wa aina mbalimbali zaidi ya makundi 550 ambao huburudisha kwa nyimbo zao nzuri ufikapo hifadhini. Unasubiri nini kufaidi yote haya? Karibu sana hifadhi ya Tarangire ujifunze mengi na uburudike pia na utajiri huu wa wanyama pori na mazingira ya hifadhi ya asili.
*Mwandishi wa Makala hii ni Mhifadhi wa wanyama pori, anapatikana kwa namba 0747 268 217, barua pepe; mwashihavacecilia@gmail.com.