Na Dkt. Raymond Mgeni
MAPINDUZI makubwa ya teknolojia ya mawasiliano na mifumo ya kidijitali imeubadilisha ulimwengu kabisa. Kama ingetokea watu waliokufa miaka ya 1960 au 70 wangeona dunia ya sasa ilivyo, basi wangestaajabishwa na uwepo wa mitandao ya kijamii. Wakati huo hapakuwepo na mitandao ya kijamii kama ilivyo sasa.
Zama tunazoishi sasa pana uwepo wa mitandao ya kijamii mfano “Whatsapp”, “Facebook”, “Instagram”, “tiktok” na “Clubhouse” kwa kutaja kwa uchache. Tunafikia kuona ile tafsiri ya kuwa dunia imekuwa kama kijiji basi ni dhahiri sasa katika zama hizi dunia ndipo inakoelekea.
Maisha ya watu sasa huwezi kuyatenganisha na mitandao ya kijamii inayofikiwa kwa urahisi kwa watu wengi. Watu wengi wana uwezo wa kumiliki simu au chombo kama komputa kinachoruhusu mtu kufanya mawasiliano ya sauti, kuandika au kwa kuona ona kama “zoom” au “webinar”.
Hili linaonesha idadi kubwa ya watu ni watumizi wa interneti na watumiaji wa mojawapo ya mitandao ya kijamii katika kuwasiliana au kufuatilia kinachoendelea mtandaoni.
Ukipita njiani au maeneo mbalimbali iwe ofisini, hospitalini, nyumba za ibada utaona namna kila mtu kainama akitumia simu kuwasiliana katika mitandao ya kijamii. Watu wengi huingiwa hata na hofu au wasiwasi wanapoona simu zao zipo kukaribia kuisha chaji au kuishiwa kifurushi cha kuperuzi mitandaoni.
Mtu anaumia moyo hali hizi zinapojitokeza kwa kuhofia kuwa atapitwa na mambo mengi yanayoendelea mitandaoni. Mfano mtandao wa kijamii wa “Tiktok” au “Instagram” ambapo mtu huruhusiwa kutuma picha au vidio fupi fupi imekuwa maarufu na makundi mbalimbali ya watu hususani vijana yanapenda kujiunga na kufuatilia yanayoendelea. Si ajabu kuona mtu ametumia zaidi ya masaa akiwa anatoka mtandao mmoja na mwingine kusoma maoni ya wafuasi wengine wa hiyo mitandao.
Licha kuwa mitandao ya kijamii imerahisisha watu kufanya mawasiliano, kutangaza biashara, kupata huduma za kielimu au mafunzo na kupata taarifa mbalimbali pia imekuja kuleta changamoto nyingi zinazogusa hali ya hatari katika afya ya akili ya watumiaji wa mitandao ya kijamii.
Uraibu wa mitandao ya kijamii, sonona na magonjwa ya wasiwasi yanaonekana kuja kwa kasi zaidi kutokana na kutumia mitandao ya kijamii kupitiliza. Unaweza kujiuliza ni kwa namna gani mitandao hii inachangia sonona, wasiwasi au uraibu?
Mwanya wa mitandao ya kijamii ni kuwa imempa kila mtu uhuru kutuma kitu anachoona anaweza kusambaza hata wakati mwingine watu hutuma picha au vitu visivyo na maadili. Mtu anaweza kutuma namna maisha yake yalivyo mazuri licha uhalisia wa maisha nje na mitandao si halisi.
Wafuasi au wale wanaofuatilia watu wenye ushawishi ni rahisi mno kufanya mambo yanayowazidi ili kujionesha nao wana maisha mazuri. Wapo wanaoingia katika matumizi ya vilevi, madeni ili tu kuonesha wengine wao ni watu wa hadhi fulani.
Hili limechangia kundi la vijana wengi kuingia katika maisha ya kuigiza ambayo yamesababisha waingie katika hali za mfadhaiko, wasiwasi endapo yale wanayoyafanya mitandaoni si sawa na uhalisia wa maisha yao ya kila siku mitaani.
Kujilinganisha, hofu ya kupitwa na matukio na kutafuta maoni kupitia mtandaoni kumechangia kuwepo na visa vingi vinavyojitokeza vya watu kupata sonona, msongo wa mawazo na hali za wasiwasi kutokana na mitandao.
Ni mambo haya matatu ndiyo yanayochangia kwa asilimia kubwa watu wapate hali za mfadhaiko, wasiwasi na kupata msongo wa mawazo wakiwa ni watumizi wa mitandao ya kijamii, wafuasi na wategemezi wa mitandao ya kijamii.
Mitandao ya kijamii imeongeza ushindani wa watu kutuma picha au vidio za kujilinganisha sababu ya watu wengine kufanya kitu fulani cha hadhi za juu dhidi ya wengine. Watu wengi husukumwa kuonesha maisha yasiyo halisi ili wale wanaofuatilia maisha yao kupitia kurasa za kijamii waone ni watu wa maisha mazuri kumbe si hivyo.
Si wote ambao wanaofuatilia hufurahia kuona hivyo. Wengi hupata hali za mfadhaiko kuona mbona wao maisha ni magumu na wengine maisha yao mazuri. Zipo picha nyingi za watu wakionesha maeneo ya kifahari waliyopo, pesa wakizitumia kwa kuonesha au hata sehemu wanazokula. Hili linachangia sana wanaofuatilia kupata hali za kusononeka wanapojilinganisha na maisha yao.
Hofu ya kupitwa na kutafuta maoni ya kile mtu amekifanya vinachangia sana watu waingiwe na wasiwasi na mfadhaiko. Watu hutuma picha au matukio ya maisha yao ili waone wengine watasemaje?, ikitokea katuma picha na haina mrejesho wowote wengi hupata hali za mfadhaiko na kujawa na maswali mengi.
Wengi hujiona huenda picha waloiweka ni mbaya au haijafurahiwa na wengine. Waathirika wakubwa hapa ni wanawake hasa wanapotuma picha na hakuna anayeisemea kwa chochote. Sambamba na hapo wengi hujawa na hali za wasiwasi au hali ya kimsongo wa mawazo wa kupitwa na habari au mambo ya mtandaoni pindi wanapokuwa wameharibikiwa simu, bando limeisha au chaji imeisha.
Jambo muhimu la kuzingatia ili kuondokana na hali za mfadhaiko, wasiwasi na msongo wa mawazo kupitia mitandao ya kijamii ni kutochukulia kila kinachotumwa mtandaoni ni halisi.
Pili, ni kujiepusha na kutekwa muda wote kuwa mtandaoni ili kujipa muda nje na mitandao ya kutathimini maisha binafsi na tatu ni kuchuja taarifa, picha au chochote kinachokuwa kinasambazwa kupitia mitandao ya kijamii.
*Mwandishi wa makala hii ni Mtaalamu wa Idara ya Afya ya Akili, Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya. Anapatikana kwa Simu:- 0676 559 211. Barua Pepe;-raymondpoet@yahoo.com.