Na Albert Kawogo
MATUMIZI ya teknolojia za kisasa katika shughuli za uhifadhi yameongeza ufanisi wa ulinzi wa wanyamapori, huku yakichangia ongezeko la watalii na mapato ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA).
TASWIRA ya uhifadhi wa wanyamapori nchini Tanzania inaendelea kubadilika kadiri teknolojia za kisasa zinavyotumika kulinda rasilimali za taifa.
Kutoka kwenye ndege zisizo na rubani (drones) hadi mifumo ya GPS, TANAPA imeendelea kutumia teknolojia kuimarisha uhifadhi na kuongeza ufanisi wa shughuli zake.
Hatua hiyo imekuwa na mchango mkubwa katika kudhibiti ujangili, kupunguza migogoro kati ya binadamu na wanyamapori na kuboresha mazingira ya hifadhi. Sambamba na mafanikio hayo, shirika limepiga hatua katika kukuza utalii na kuongeza mapato.
Katika mwaka wa fedha 2025/2026, TANAPA imekusanya Sh bilioni 534.09, kutoka Sh bilioni 174.71 zilizokusanywa mwaka 2021/2022. Hili ni ongezeko la zaidi ya mara tatu ndani ya kipindi hicho.
Vilevile, idadi ya watalii waliotembelea hifadhi za taifa imeongezeka kutoka 708,319 hadi 1,559,641.
Ukuaji huo unaonesha mchango wa uhifadhi na utalii katika kukuza uchumi wa taifa.
Akizungumza katika kikao kazi na wahariri wa vyombo vya habari kilichoandaliwa kwa ushirikiano na Ofisi ya Msajili wa Hazina (OTR), jijini Dar es Salaam, Kamishna Mkuu wa Uhifadhi wa TANAPA, Massana Gibril Mwishawa, amesema mafanikio hayo yametokana na kuimarika kwa shughuli za uhifadhi na utalii.
Amesema hatua hizo ni sehemu ya utekelezaji wa mipango ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kulinda rasilimali za taifa na kukuza sekta ya utalii.
Katika mapambano dhidi ya ujangili, teknolojia imekuwa nyenzo muhimu inayowezesha askari wa wanyamapori kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.
TANAPA imepata ndege zisizo na rubani 40 zinazotumika kufanya doria za angani, kufuatilia mienendo ya wanyamapori na kubaini maeneo yenye viashiria vya uhalifu.
Pia, mifumo ya GPS imewekwa kwa baadhi ya wanyamapori ili kufuatilia mienendo yao na kutoa taarifa wanapokaribia maeneo yanayokaliwa na wananchi. Hatua hiyo inalenga kupunguza migogoro na madhara yanayotokana na wanyama kuingia katika makazi ya watu.
Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, shirika limefanya doria 31,314, na kukamata watuhumiwa 385 wa ujangili, silaha 105 na kutibua mitego 1,971. Aidha, limekamata mifugo 65,600 iliyoingia ndani ya hifadhi kinyume cha sheria.
Katika kuimarisha mawasiliano na usalama, TANAPA imejenga vituo vitatu vya kisasa vya mawasiliano katika Hifadhi za Taifa za Serengeti na Nyerere.
Shirika pia linaendelea kuboresha mifumo ya redio katika hifadhi za Serengeti, Ziwa Manyara, Tarangire, Mkomazi na Nyerere ili kurahisisha mawasiliano kati ya askari wa wanyamapori na vyombo vingine vya usalama.
Mbali na kudhibiti ujangili, TANAPA imeendelea kurejesha mazingira yaliyoharibika ili kuhakikisha wanyamapori wanapata makazi na chakula cha kutosha.
Katika hatua hiyo, shirika limedhibiti mimea vamizi katika hekta 984.2 kwenye hifadhi 15. Pia limesafisha hekta 1,546 zilizokuwa zimeathiriwa na vichaka katika Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara.
Juhudi hizo zinalenga kurejesha maeneo ya malisho na kupunguza uwezekano wa wanyamapori kutoka nje ya hifadhi kutafuta chakula.
Aidha, TANAPA imefanikiwa kurejesha ukanda wa ikolojia unaounganisha Hifadhi za Taifa za Katavi na Milima Mahale kwa kushirikiana na wananchi. Hatua hiyo inasaidia kulinda misitu ya asili na kuwezesha wanyamapori kuhama kati ya maeneo hayo.
Ushirikiano huo pia umefungua fursa za kiuchumi kwa wananchi kupitia shughuli mbalimbali, ikiwemo biashara ya hewa ukaa na mikataba inayosaidia kupata mapato kwa ajili ya kuendeleza uhifadhi.
Faida za uhifadhi zinaonekana pia katika maisha ya wananchi wanaozunguka hifadhi. Kupitia miradi ya uwajibikaji kwa jamii, TANAPA imekuwa ikichangia ujenzi wa zahanati, madarasa, nyumba za walimu, miundombinu ya maji na barabara.
Shirika pia linaendelea kutoa ajira kwa Watanzania, hususan vijana wanaotoka katika jamii zinazozunguka hifadhi. Vilevile, linaweka mazingira rafiki kwa wawekezaji wa sekta ya utalii ili kuongeza fursa za ajira katika hoteli, usafirishaji na huduma nyingine.
Kwa Tanzania yenye hifadhi 21 za taifa zenye jumla ya eneo la kilomita za mraba 95,338.48, uwekezaji katika teknolojia na uhifadhi una nafasi kubwa katika kulinda urithi wa asili.
Hifadhi ya Nyerere ndiyo kubwa zaidi ikiwa na kilomita za mraba 29,276, ikifuatiwa na Ruaha yenye kilomita za mraba 19,822 na Serengeti yenye kilomita za mraba 14,763.
Pamoja na mafanikio hayo, changamoto za migogoro kati ya binadamu na wanyamapori, ujangili, uingizaji wa mifugo hifadhini, mimea vamizi na upungufu wa maji kwa wanyamapori bado zinahitaji mikakati endelevu.
Kwa msingi huo, matumizi ya teknolojia, ushirikiano na wananchi pamoja na uwekezaji katika miundombinu ya uhifadhi ni nguzo muhimu katika kuhakikisha rasilimali za taifa zinalindwa na kuendelea kutoa manufaa kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Mafanikio ya TANAPA yanaonesha kuwa uhifadhi si suala la kulinda wanyamapori pekee, bali pia ni uwekezaji katika uchumi, ajira, ustawi wa jamii na maendeleo ya taifa.