Na Mwandishi Wetu
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) jana iliwasilisha Bungeni taarifa yake kuhusu mwenendo wa uwekezaji wa mitaji ya umma kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na kutaka thamani ya hisa katika mitaji ya umma iendane na ukubwa wa gawio.
Akiwasilisha taarifa ya PIC Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Ojambi Masaburi ambaye pia ni Mbunge wa Kivule, jijini Dar esSalaam, alisema Kamati imebaini kuwa licha ya thamani ya hisa kuongezeka, uwiano wa gawio dhidi ya thamani ya uwekezaji bado ni mdogo.
Alisema Kwa taasisi zenye hisa chache, ni taasisi 18 tu kati ya 56 zilizotoa gawio mwaka 2024/2025, na uwiano wa gawio umeshuka kutoka asilimia 13 (2022/2023) hadi asilimia 8.9 (2024/2025).
Akionyesha thamani ya jumla ya mitaji ya umma iliyowekezwa katika taasisi, mashirika ya umma na kampuni ambazo Serikali ina hisa Masaburi alisema imefikia shilingi trilioni 92.275 na
kwamba Kiasi hicho ni ongezeko la takribani asilimia 20.3 ikilinganishwa na shilingi trilioni 76.708 zilizokuwa zimewekwa mwaka 2022/2023.
”Katika kipindi hicho, Mfuko Mkuu wa Serikali ulipokea jumla ya shilingi trilioni 1.028 kutokana na michango mbalimbali ya taasisi na mashirika,” alisema.
Aliongeza kati ya fedha hizo shilingi bilioni 612.4 ni mchango wa asilimia 15 ya mapato ghafi, shilingi bilioni 333.97 ziada na michango mengineyo, shilingi bilioni 58.8 Riba na marejesho ya mikopo, shilingi bilioni 20.3 michango ya TTMS shilingi bilioni 3.07
“Uwekezaji katika taasisi ambazo Serikali ina hisa nyingi (asilimia 51 au zaidi) ulifikia takribani shilingi trilioni 89.01, huku uwekezaji katika taasisi zenye hisa chache ukifikia shilingi trilioni 3.267 hili ni ongezeko la asilimia 52.2 ikilinganishwa na mwaka uliopita,” alisema.
Kufuatia hali hiyo PIC ilitoa maoni na mapendekezo 12 kwa Bunge. Miongoni mwa masuala yaliyozingatiwa ni uwiano mdogo kati ya ongezeko la uwekezaji na rejesho linalopatikana, Umuhimu wa kuongeza mtaji katika taasisi ambazo Serikali ina hisa chache ili kuongeza tija.
Pia, ilitaka kutumia zaidi ushirikiano wa sekta binafsi (PPP) katika miradi yenye fursa ili kupunguza utegemezi wa fedha za serikali.
Aidha, katika mapendekezo hayo PIC ilitaka kulipwa madeni ya Mamlaka ya Mbolea (TFRA) na
kutenga bajeti ya kutosha ya ruzuku ili kuepuka madeni mapya,Kuboresha usimamizi wa
rasilimali za NARCO na Kutathmini na kuboresha utendaji wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege
(TAA) pamoja na Kupunguza utegemezi mkubwa wa ruzuku katika mishahara na uendeshaji wa baadhi ya taasisi.