Na Mwandishi Wetu
WANANCHI wanaojihusisha na uchimbaji wa mchanga kiholela kwenye mito iliyopo jijini Dar es Salaam wametakiwa kuacha mtindo huo kwani wanasababisha athari kubwa kwa jamii.
Hayo yamesemwa Septemba 18, 2026 na Elibariki Mmassy, Mkurugenzi wa Bodi ya Maji Bonde la Wami Ruvu, wakati wa kikao kilichohusisha kikosi kazi cha Mkoa wa Dar es Salaam na wadau wasafisha mito.
Mmasy alisema, wanafahamu kwamba kuna shughuli zinafanyika nyakati za usiku za uchimbaji wa mchanga kwa kutumia machepe na magari maalumu, jambo ambalo harihusiwi na kuitaka jamii inayozunguka miti hiyo kutoa ushirikiano ili kudhibiti vitendo hivyo.
Alisema, wananchi hawapaswi kukaa kimya wanapoona kuna shughuli zinaendelea ikiwemo uchimbaji wa mchanga na wana jukumu la kuhoji kama watu hao wana vibali, kwani kuacha uharibifu kwenye maeneo husika, kunaleta athari kwa jamii kubwa.

Mkurugenzi huyo alisema, shughuli hizo zimeruhusiwa kwenye maeneo maalumu kwa ajili ya kusafisha mito kwa kuondoa mchanga na takataka ili maji yaweze kupita urahisi.
Alisema, jijini Dar es Salaam taasisi yao wanasimamia mito kadhaa ambayo imekuwa ikitupwa takataka na wakati mwingine imekuwa ikijaa mchanga kutokana na shughuli ambazo zinafanyika milimani, hivyo mvua zinaponyesha, kingo cha mto zinakuwa dhaifu na mto unakuwa umepunguza kina na kusababisha maji kuingia kwenye makazi ya watu.
Mmasy alisema, ili kuepukana na changamoto hiyo na ikizingatiwa kuna uwezekano wa kuwepo kwa mvua kubwa za El Nino, inafanyika tathimini na kutolewa kwa vibali kwa taasisi zinazojihusisha nna usafishaji wa mito na kufnaya usafi.
Alisema, hivi sasa wameanza zoezi hilo la kusafisha mito kwa kushirikiana na wadau wakiwemo vijana ambao wana umoja wao unaotambulika sambamba na wakandarasi na kuwataka wananchi wengine ambao hawajaruhusiwa kufanya shughuli hizo za usafi kutoingia kwenye mito hiyo.

“Haturuhusu watu kuingia kwenye mito kiholela bila kufuata taratibu,” alisisitiza Mmassy na kuongeza kuwa, wamejipanga kwa ajili ya kufanya doria ili kudhibiti vitendo hivyo.
Aidha, alitoa wito kwa wananchi wanaoishi jirani na vyanzo vya maji na mito kuchukua tahadhari, kulingana na utabiri uliotolewa na Mamlaka ya Hali ya uwezekano wa kuwepo kwa mvua kubwa na kusababisha madhara.
Kwa upande wake Mhandishi Amani Mafuru, Katibu Tawala Msaidizi anayesimamia Miundombinu, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam alisema, kikao hicho muhimu, kimelenga kujipanga kufanya maandalizi ya kukabiliana na mvua za El Nino.
Alisema, katika kuongeza nguvu, wameamua kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo Wami/Ruvu ambao kwenye kikao hicho walitoa tathmini ya hali ya mito ilivyo kwasasa na wamepokea maoni ya wadau wakiwemo wakandarasi na vikundi vya vijana maarufu wanaoitwa ‘machepe.’

Alisema, maoni hayo yatawasaidia kwenye shughuli za kila siku za Kikosi Kazi kinachoratibu zoezi la usafishaji wa mito ya jijini Dar es Salaam.
Naye, Athumani Kambi, Katibu wa Chama cha Machepe (Chawamada), alisema wanafurahishwa na jinsi Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anavyopambana kuhakikisha Tanzania inakuwa ya kijani, na wameahidi watalinda mazingira ili kuunga mkono jitihada hizo.
Akizungumza kwa niaba ya wakandarasi wanaojihusisha na usafishaji wa mito, Shani Ngwanda alisema, kikao walichofanya kimekuwa na tija, ambapo wamejadiliana namna ya kukabiliana na mvua za El Nino.
Alisema, baada ya majadiliano ya kina, kinachofuata ni utekelezaji kwa vitendo kwa ajili ya kuokoa mazingira yanayoizunguka jamii hususani wakati huu ambapo kumetolewa tahadhari ya kuwepo kwa mvua hizo.
