CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimeridhishwa na maendeleo ya mradi wa soko lililopo Fungurefu ambao umefikia asilimia 86 na kupongeza Serikali ya Wilaya pamoja na wasimamizi wa mradi kwa usimamizi mzuri wa utekelezaji wake.
Akizungumza katika ziara yake inayoendelea katika Mkoa wa Kaskazini Unguja, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Abdi Mahmoud Abdi, amesema maendeleo ya mradi huo yanaonesha kuwa utekelezaji wake unaenda vizuri kwa mujibu wa mkataba na unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Oktoba mwaka huu.
Alisema, kukamilika kwa mradi huo kutasaidia kuondoa changamoto iliyokusudiwa kutatuliwa kupitia ujenzi wake, hivyo ni muhimu kuhakikisha miundombinu hiyo inatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.
Aidha, ameitaka Baraza la Mji kuanza mapema maandalizi ya matumizi ya majengo hayo, ikiwemo mipango ya biashara, mikataba na namna wafanyabiashara watakavyotumia maeneo hayo kabla ya mradi kukabidhiwa rasmi.
Alisema wafanyabiashara waliokuwa wakitoa huduma katika eneo hilo wanapaswa kupewa kipaumbele katika maduka yatakayopatikana, kwa kuwa tayari wana uzoefu wa kufanya biashara katika eneo hilo.
“Wasubiri mpaka mwezi wa kumi wanakabidhiwa ndipo waweke mpango wa kutumia majengo haya. Sasa hivi ndiyo muda wa kuweka mpango kwamba tukimaliza tufanye biashara fulani na fulani,” amesema.
Pamoja na hayo, ameitaka Serikali ya Wilaya na Baraza la Mji kuweka mpango wa matumizi ya maeneo ya nje ya soko ili kuzuia ujenzi holela wa vibanda na maduka yasiyokidhi viwango.
Hata hivyo, alisema, eneo hilo linapaswa kuwekewa utaratibu unaoonesha aina ya majengo na biashara zinazoweza kuanzishwa ili kuendana na mabadiliko ya Zanzibar na miradi mikubwa ya kisasa inayotekelezwa.
Alisema Serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi kujenga miundombinu ya kisasa huku maeneo ya nje yakiendelea kuwa na majengo yasiyo na hadhi na yasiyoendana na mazingira ya sasa.
Aidha, amepongeza ongezeko la maduka 40 katika mradi huo, akisema hatua hiyo itasaidia kuongeza uwezo wa soko kutoa huduma na kutatua changamoto zilizokuwa zimeainishwa awali.
Alisema utekelezaji wa miradi mikubwa ya kisasa ni sehemu ya juhudi za kuboresha huduma kwa wananchi na kuimarisha mazingira ya biashara, hivyo ni muhimu kuhakikisha miradi hiyo inatumika ipasavyo baada ya kukamilika.
Kwa upande wake, muhandisi wa mradi huo Hamid Katwe amesema mradi umefikia hatua ya finishing, huku hali ya kifedha ikiwa si changamoto kubwa kutokana na kuimarika kwa mtiririko wa fedha.
Alisema mradi huo ulikabiliwa na changamoto katika hatua za awali, ikiwemo ujenzi wa misingi kutokana na eneo kuwa karibu na bahari, pamoja na upatikanaji wa vifaa vya ujenzi vya ndani, hususan mawe yaliyotumika katika kuimarisha eneo la mradi.
Hata hivyo, alisema kwa mujibu wa mkataba, mradi unatarajiwa kukamilika ifikapo Oktoba 30, 2026, huku maeneo makuu pamoja na vifaa muhimu, ikiwemo courtroom na mashine ya kutengeneza barafu, vikitarajiwa kukamilika au kuwasili ifikapo Oktoba Mosi mwaka huu.
Hata hivyo, amesema changamoto iliyopo kwa sasa ni ujenzi wa maduka 40 yaliyoongezwa katika mradi huo, lakini anaamini sehemu kubwa ya mradi uliopangwa awali itakamilika kwa wakati, huku akitarajia ufunguzi rasmi wa mradi huo kufanyika wakati wa sherehe za Mapinduzi.