Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
CHAMA cha Mapinduzi (CCM), kimewatoa hofu wenye nia ya kugombea nafasi mbalimbali katika uchaguzi ndani ya chama hicho unaotarajiwa kufanyika mapema mwakani 2027 kuwa wasijishughulishe na watu wanaopita pita na kutengeneza makundi kwa lengo la kuingilia uchaguzi.
Akizungumza na wanahabari kuhusiana na uchaguzi huo mjini Unguja Septemba 14, 2026, Katibu wa Kamati Maalum NEC Zanzibar Idara ya Itikadi Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis alisema, chama kipo makini na hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa watakaobainika.
“WanaCCM wasiwe na hofu na hao wanaojihangaisha kupanga safu makundi, kupanga watu, niwaambie na niwahakikishie kamati ya maadili na usalama ipo makini,” alisema na kuongeza kuwa, kila mwana CCM ana haki ya kugombea katika nafasi zilizo ainishwa na katiba ya CCM.
Mbeto alisema, chama kina uzoefu kinapoelekea chaguzi za dola na anakiri kuna makada wa CCM wana nia ya kurithi nafasi mbalimbali ikiwemo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Zanzibar ifikapo 2030 kutokana na ukweli kuwa huenda uongozi mzima ukabadilika na ili mgombea apate tiketi ya CCM lazima awe na wajumbe.
Alisema, kutokana na hali hiyo kuna watu wanataka kucheza karata zao ili wapange safu za watu ambao watakuja kuwaunga mkono, tayari wameunda makundi na kueleza kuwa Mwenyekiti wa kamati ya maadili na usalama, Mzee Steven Sato Wasira yupo, hivyo wajiandae.
Mwenezi huyo alisema, kitu ambacho ana uhakika nacho na anaweza kukithibitisha ni kuwa, chama kipo makini na wapo ambao wanatia mikono ili kupanga safu ya kuwaunga mkono.
“Wameanza michakato, wengine wameanza ziara sehemu mbalimbali kote huko kujitangaza kuweka mguu sawa, bahati nzuri CCM ni chama imara kinaongozwa na katiba, sheria na kanuni” alisema Komredi Mbeto.
Alisema, upo usalama wa kutosha na uchunguzi ukatapofanyika na yeyote akibainika jina lake litaondolewa na adhabu kali itatolewa kulingana na sheria za kamati ya usalama na maadili za CCM.
“Nisiwafiche kama kuna watu wanataka kufanya hivyo, chama kipo makini na kitachukua hatua, tutakuwa makini sana na hivi karibuni yalifanyika mapitio ya kanuni za maadili na usalama na sasa zimekuwa kali zaidi kwa watu watakaotaka kuingilia uchaguzi,” alisema.
CCM kulingana na katiba ya chama hicho 2027 kinaingia kwenye uchaguzi wa kupata viongozi wake katika ngazi mbalimbali isipokuwa nafasi ya Mwenyekiti na Makamu wawili.
Nafasi zingine ambazo hazitagombewa ni Sekretarieti kwa maana ya wakuu wa idara na wenyeviti na makatibu wa CCM wa wilaya na mikoa ambao mchakato wake huanzia Kamati Kuu Taifa na uteuzi kufanywa na Halmashauri Kuu Taifa.