Na Mwandishi Wetu
HISTORIA inaonyesha kuwa Mataifa yanayofanikiwa si yale yasiyokuwa na tofauti za kisiasa, bali ni yale yanayoweza kuzisimamia tofauti hizo kwa njia ya mazungumzo, kuheshimiana na kuweka mbele maslahi ya wananchi.
Kwa muda mrefu, Zanzibar imepitia vipindi vya ushindani wa kisiasa vilivyoambatana na mafanikio na changamoto mbalimbali ambazo zimesababisha mgawanyiko mkubwa kwenye jamii hiyo.
Upo ushahidi wa ndugu, majirani au marafiki kususia sherehe, misiba au biashara za mtu ambaye wana itikadi tofauti za vyama na hali ikafika pabaya zaidi kwa watu kusababishiana majeraha, vifo na hasara ya mali kwa kuchomeana nyumba kwa sababu ya uhasama wa kisiasa.
Hata hivyo, zimefanyika jitihada mbalimbali za mazungumzo kwa muda mrefu kuhakikisha hali hiyo inatoweka visiwani hapo na watu wanaishi kwa amani; kwani uzoefu umeonyesha kuwa, mazungumzo na maridhiano vinaweza kusaidia kupunguza misuguano na kujenga mazingira bora ya ushirikiano.

Jana, Julai 9, 2026 kwenye viwanja vya Ikulu, Visiwani Zanzibar, liliwasilishwa tamko la pamoja kati ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha ACT Wazalendo, ikiwa ni mwelekeo wa kujenga Mustakabali mpya Visiwani humo.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, kwenye hotuba yake aliyoitoa baada ya kusainiwa wa tamko hilo anasema, hiyo ni hatua muhimu inayofungua njia ya utekelezaji wa uundaji wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Vile vile, Rais Dkt. Mwinyi anasema, tukio hilo muhimu ni njia ya kuelekea kuimarisha amani, umoja, mshikamano na mustakabali mwema wa Zanzibar.
Wadau wengine walioshiriki kwenye hafla hiyo wanasema, tamko la pamoja linaweza kuwa ishara ya dhamira ya kutafuta mwafaka kupitia njia za amani na wamesisitiza hatua hiyo ina faida kubwa kwa wananchi wa Zanzibar.
Wanasema, itasaidia kuimarika kwa utulivu wa kisiasa ambao utaziwezesha Taasisi za Serikali kufanya kazi kwa ufanisi na wananchi kuendelea na shughuli zao za kila siku kwa utulivu; Mazingira hayo pia huongeza imani ya wananchi katika mifumo ya utawala na demokrasia.
Katibu wa Kamati Maalum NEC Zanzibar Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis katika kusisitiza hilo anasema, Serikali nzuri ni ile ambayo ina ridhaa ya wananchi wote.
“Tukifikia mahala pazuri, kasi itaongezeka, Serikali nzuri ni ile inayopata ridhaa ya wananchi wote; kwanza itatuliza siasa zetu, itawapa matumaini ya maendeleo wananchi wetu, Wazanzibar na watanzania wanataka maendeleo, hawahitaji malumbano yetu ya Kisiasa,” anasema Mbeto.

Faida nyingine ni kukuza uchumi. Zanzibar inategemea kwa kiwango kikubwa sekta za utalii, biashara na uwekezaji, ambapo inaelezwa kuwa, Utalii ndio uti wa mgongo wa uchumi wa Visiwa hivyo.
Taarifa zinaonyesha kuwa, Utalii unachangia zaidi ya asilimia 30 ya Pato la Taifa (GDP), zaidi ya asilimia 80 ya mapato ya kigeni, na kutoa ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja kwa maelfu ya wananchi, hususan vijana na wanawake.
Aidha, kasi ya ukuaji wa uwekezaji Visiwani Zanzibar imeongezeka, ambapo taarifa ya karibu inaonyesha zaidi ya miradi 485 yenye thamani ya Dola za Kimarekani Bilioni 6.2 imesajiliwa na Mamlaka ya Vitegauchumi Zanzibar (ZIPA), inayotarajiwa kuzalisha ajira 25,470.
Kwa maana hiyo, mazingira ya amani na utulivu, huongeza imani ya wawekezaji na kuwavutia watalii, jambo linaloweza kuongeza zaidi mapato, ajira na fursa za maendeleo kwa wananchi.
Pia, maridhiano yanaweza kuimarisha mshikamano wa kijamii. Tofauti za kisiasa zisipopewa nafasi ya kugawa jamii, wananchi huendelea kuishi kwa kuheshimiana na kushirikiana katika kujenga maendeleo ya maeneo yao. Ushindani wa kisiasa hubaki kuwa wa sera na hoja badala ya kuwa chanzo cha migawanyiko.

Vile vile, maridhiano yanaweza kuchochea utamaduni wa mazungumzo na utatuzi wa migogoro kwa njia za Kikatiba na kisheria, hali hiyo huongeza imani ya wananchi katika mchakato wa uchaguzi na taasisi zinazosimamia haki na utawala wa sheria.
Hata hivyo, mafanikio ya tamko lolote la pamoja yatategemea utekelezaji wake. Kauli zinapaswa kuambatana na vitendo vinavyoonyesha uwazi, kuheshimiana, uwajibikaji na kujali maslahi ya wananchi. Maridhiano yanakuwa na maana zaidi pale yanapoleta matokeo yanayoonekana katika maisha ya watu.
Katika kusimamia hilo, Rais Dkt. Hussein Mwinyi amewahakikishia viongozi wa vyama vya siasa na wananchi wa Zanzibar kuwa yuko tayari kushirikiana na viongozi wenzake kuyaendeleza kwa dhati maridhiano hayo, kwa lengo la kuhakikisha Zanzibar inaendelea kuwa na amani, umoja, mshikamano na utulivu.
Rais Dkt. Mwinyi amesema, Zanzibar inahitaji kuendelea kuimarisha misingi ya kuaminiana, kuvumiliana, kuheshimiana na kushirikiana, kwa kuwa mambo hayo ni nguzo muhimu katika kulinda amani, kukuza maendeleo na kuiwezesha Zanzibar kufikia malengo yake ya muda mrefu.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amepongeza hatua hiyo na kueleza kuwa, maridhiano yaliyofikiwa yanafungua ukurasa mpya wa kuimarisha umoja, utulivu na mshikamano miongoni mwa Wazanzibari.
Aidha, amesema hatua hiyo ni ishara ya ukomavu wa kisiasa na uthibitisho wa dhamira ya viongozi pamoja na wadau wa siasa katika kujenga mazingira ya amani, ushirikiano na maendeleo endelevu kwa Zanzibar na Taifa kwa ujumla.
Kama wanavyosisitiza viongozi hao wakuu, tamko la pamoja ambalo limesainiwa na kuelekea kwenye hatua ya maridhiano na uundwaji wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, ni msingi wa kujenga Zanzibar yenye amani ya kudumu, uchumi unaokua na demokrasia inayozidi kuimarika.