Na Albert Thomas Kawogo
LEO nataka kuzungumzia bandari saba za Dar es Salaam ambazo zimekuwa ni nguzo muhimu katika kuchangia mapato ya taifa letu tangu nchi ilipopata uhuru.
Naifahamu Bandari ya kwanza ya Dar es Salaam ambayo historia ya maendeleo yake ilianza rasmi mwaka 1961. Bandari hii imekuwa lango kuu la biashara la Tanzania na moja ya bandari muhimu zaidi katika kutoa mchango wa maendeleo ya Tanzania.
Bandari hii, inasaidia kupokea mizigo ya nchi jirani zisizo na bandari kama Zambia, Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Malawi, Uganda na Zimbabwe. Pia, hushughulikia takribani asilimia 95 ya biashara ya Kimataifa ya Tanzania. Pamoja na yote hayo; hii sio bandari ninayotaka kuizungumzia hapa leo.

Naifahamu bandari ya pili ya Dar es Salaam. Baada ya uhuru wa Tanganyika mwaka 1961, Bandari ya Dar es Salaam iliendelea kuendeshwa chini ya taasisi za kikanda za East African Railways and Harbours Corporation, kabla ya kuhamishiwa East African Harbours Corporation mwaka 1969. Bandari hii iliendelea kutumika kama chombo muhimu cha kuunganisha uchumi wa Taifa na masoko ya Kimataifa.
Ukuaji wa biashara ya nje na kuongezeka kwa matumizi ya reli ya kati kuliongeza umuhimu wa bandari hii kama kitovu cha usafirishaji wa bidhaa za ndani na za nchi jirani. Hii si bandari ninayotaka kuizungumzia sana leo.
Naikumbuka vema bandari ya tatu ya Dar es Salaam iliyokuja baada ya kuanzishwa kwa Tanzania Harbours Authority. Inaelezwa kuwa baada ya kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 1977, Tanzania iliunda Tanzania Harbours Authority (THA) kusimamia bandari zake zote. Hii ilikuwa hatua muhimu katika kuimarisha usimamizi wa Bandari nchini.
Katika kipindi hiki, kwenye bandari ya tatu ya Dar es Salaam miradi kadhaa ya maendeleo ilitekelezwa kwa mfano;Mwaka 1977, ujenzi wa gati namba 9, 10 na 11 ulikamilika. Mwaka 1988, magati hayo yalibadilishwa kuwa kituo cha makasha (container terminal) chenye uwezo wa kuhudumia hadi TEUs 250,000 kwa mwaka.

Mwaka 1989, kituo cha kuhifadhi na kushughulikia nafaka (grain terminal) kilikamilishwa. Mwaka 1998, njia ya kuingilia meli bandarini ilipanuliwa na kuchimbwa zaidi ili kuruhusu meli kubwa kuingia saa 24 kwa siku. Maboresho hayo yaliongeza uwezo wa bandari kupokea meli kubwa na kushughulikia mizigo kwa ufanisi zaidi. Bado sitaki kuizungumzia zaidi bandari hii ya tatu.
Naifahamu na nimeuona ufanisi wa bandari mpya ya nne iliyoanza kazi mwaka 2000. Ni kipindi hiki Mageuzi na Ushirikiano na Sekta Binafsi yalianza na kuimarika. Mfano mwaka huo wa 2000 ndio mwaka ambao shughuli za kituo cha makasha zilikodishwa kwa kampuni ya Tanzania International Container Terminal Services (TICTS), hatua ililenga kuongeza ufanisi wa huduma za bandari.
Sitaki kwenda mbali zaidi kuichambua bandari hii ya nne kwani sio nia ya makala hii. Naifahamu kidogo sana bandari ya tano ya Dar es Salaam nitajaribu kuielezea kadri ninavyofahamu. Mwaka 2004, serikali ilianzisha Tanzania Ports Authority (TPA) kupitia sheria ya bandari na. 17 ya mwaka 2004 kuchukua nafasi ya THA. TPA ilipewa jukumu la kuendeleza, kusimamia na kuendesha bandari zote za Tanzania Bara.
Katika kipindi hiki, Bandari ya tano ya Dar es Salaam ilikuwa kitovu kikuu cha biashara kwa Tanzania na nchi za ukanda wa Afrika Mashariki na Kati Naifahamu zaidi bandari nyingine ya sita ya Dar es Salaam. Bandari hii kama bandari nyingine tano zilizopita ilianzia mwaka 2015.

Ili iweze kwenda na mahitaji ya sasa bandari hii ya sita ilifanyiwa upanuzi na uboreshaji Mkubwa na kuwa tofauti kabisa na zile bandari tano. Ni katika kipindi hiki Serikali ya Tanzania ilianza kutekeleza miradi mikubwa ya kisasa ya kuboresha bandari ili kuongeza ushindani wake dhidi ya bandari nyingine za ukanda kama Mombasa na Durban.
Maboresho makubwa yalijumuisha: Ujenzi na ukarabati wa magati mapya. Kuongeza kina cha bandari ili kupokea meli kubwa zaidi. Kuboresha mifumo ya kidijitali ya ushughulikiaji mizigo. Kuongeza maeneo ya kuhifadhi makasha na mizigo mingine. Kuimarisha miundombinu ya reli na barabara inayounganisha bandari na maeneo ya ndani ya nchi.
Kwa sasa, bandari ina urefu wa gati wa takribani mita 2,600 na zaidi ya magati 12 ya maji marefu. Ina uwezo wa kuhudumia mamilioni ya tani za mizigo kwa mwaka na inaendelea kuwa lango kuu la biashara kwa Tanzania na nchi nyingi za bara.
Hapa nitakujulisha ninavyoifahamu bandari ya saba ya Dar es Salaam. Hii sasa ndio ninayotaka kuizungumzia leo. Naifahamu vema bandari mpya ya Dar es Salaam iliyoanza kazi rasmi mwaka 2022 na baadae mabadiliko makubwa kuja kuanza kuonekana mwaka 2024 hadi sasa.

Bandari hii Kwa sasa imesimikwa rasmi heshima ya kuwa lango kuu la biashara la Tanzania na nchi jirani huku ikirekodi ukuaji mkubwa wa mizigo, makontena na mapato katika miaka ya 2025 na 2026. Mafanikio haya yananabebwa na uwekezaji katika miundombinu, ushirikiano na sekta binafsi, pamoja na maboresho ya ufanisi wa huduma
Katika kipindi cha Julai 2025 hadi Machi 2026, Bandari ya Dar es Salaam ilihudumia tani milioni 25.07 za mizigo, ikilinganishwa na tani milioni 19.31 katika kipindi kama hicho mwaka uliotangulia. Huu ni ukuaji wa karibu asilimia 30.
Hii ndio bandari ya Dar es Salaam ambayo rekodi mpya ya makontena yaliyoshughulikiwa katika mfumo wa bandari yalifikia TEUs 1,005,529 kati ya Julai 2025 na Machi 2026, ongezeko la asilimia 20.88 kutoka TEUs 831,866 za mwaka uliopita. Aidha, kati ya Julai 2025 na Aprili 2026, zaidi ya makontena milioni 1.08 yalihudumiwa, ongezeko la asilimia 25.
Naifahamu bandari ya saba ya Dar es Salaam ambayo mizigo ya ‘transit’ inayokwenda nchi zisizo na bandari kama Zambia, Rwanda, Burundi, Uganda, Malawi na DRC ilifikia tani milioni 10.93 katika kipindi cha Julai 2025 hadi Machi 2026, ikiwa ni ongezeko la asilimia 32.64. Hii inaonyesha kuimarika kwa nafasi ya Tanzania kama kitovu cha usafirishaji katika Afrika Mashariki.

Baada ya maboresho ya miundombinu kupitia Mradi wa Dar es Salaam Maritime Gateway, kina cha lango la kuingilia meli kiliongezwa na vifaa vipya vya kisasa vikawekwa. Hali hii imepunguza muda wa meli kukaa bandarini kutoka wastani wa siku 10 hadi takribani siku 3.
Kwenye bandari hii mapato ya forodha yanayokusanywa yaliongezeka kutoka shilingi trilioni 7.33 mwaka 2020/21 hadi trilioni 11.07 mwaka 2024/25, yakichangiwa na kuongezeka kwa shehena na uboreshaji wa huduma. Wakati huo huo, TPA ilikusanya mapato ya zaidi ya shilingi bilioni 718.99 kufikia Machi 2026.
Naifahamu bandari ya Dar es ambayo Mwezi Mei 2026, kituo cha makontena cha TEAGTL kilivunja rekodi kwa kuhudumia TEUs 85,243 ndani ya mwezi mmoja, kiwango cha juu zaidi kuwahi kufikiwa katika historia ya kituo hicho.
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania TPA Plasduce Mkeli Mbossa anasema mafanikio ya bandari ya Dar es Salaam yanahusishwa na uwekezaji mkubwa katika miundombinu, matumizi ya teknolojia na maboresho ya mifumo ya uendeshaji.
Mbossa anasema uwekezaji huo kuwa ni katika vifaa vya kisasa vya kuhudumia mizigo pamoja na mageuzi ya kiutendaji yanayolenga kupunguza muda wa meli kusubiri na kuhudumiwa bandarini.