RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema kuna umuhimu mkubwa kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kuimarisha ushirikiano katika nyanja ya diplomasia ya uchumi, biashara na uwekezaji.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, Julai 6, 2026, alipokutana na Balozi mpya wa Tanzania nchini Uganda, Balozi Meja Jenerali Marco Elisha Gaguti, aliyefika Ikulu Zanzibar kwa ajili ya kuaga kabla ya kuelekea katika kituo chake cha kazi.
Rais Dkt. Mwinyi amesema ni wakati muafaka kwa nchi za Afrika Mashariki kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji, kwa lengo la kunufaika na fursa mbalimbali za kiuchumi zilizopo katika mataifa hayo.
Ameeleza kuwa uhusiano mzuri baina ya mataifa hayo ni msingi muhimu wa kukuza uchumi na kuimarisha ustawi wa wananchi.
Aidha, Rais Dkt. Mwinyi amemsisitiza Balozi Marco kutumia nafasi yake kuzitangaza fursa za uwekezaji na vivutio vya utalii vilivyopo Tanzania, ikiwemo Zanzibar, nchini Uganda, hususan kwa makampuni, wafanyabiashara na wawekezaji wakubwa, ili waweze kuja kuwekeza nchini.
Rais Dkt. Mwinyi amemhakikishia Balozi Marco ushirikiano mkubwa katika utekelezaji wa majukumu yake mapya ya kibalozi, huku akimshauri kuchukua juhudi maalum za kuwashawishi na kuwaunganisha wafanyabiashara na wawekezaji wa Uganda kutumia fursa zilizopo kuwekeza Tanzania.
Kwa upande wake, Balozi Meja Jenerali Marco Elisha Gaguti amemhakikishia Rais Dkt. Mwinyi kuwa atafanya kila linalowezekana kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi, kwa kuzingatia miongozo na maelekezo aliyopokea, sambamba na kuendeleza kimkakati diplomasia ya uchumi baina ya Tanzania na Uganda.