Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mussa Azzan Zungu.
Na Mwandishi Wetu
SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mussa Azzan Zungu amesema, bunge litaendelea kutekeleza wajibu wake kwa weledi na uwazi ili kuwaletea Watanzania maendeleo kwa maslahi ya Taifa.
Akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam, Julai 1, 2026, Spika Zungu alisema, bunge linapoelekea kuadhimisha miaka 100 ya kuanzishwa kwake, limeendelea kuimarika katika majukumu yake ya kuishauri na kuisimamia Serikali katika kipindi chote cha historia.
“Niwahikikishie, bunge tunaendelea kusimamia ustawi wa wananchi, tukio hili haliishii kusheherekea tu, bali kuthibitisha kujitoa kwetu kujenga mustakabali imara wa nchi. Bunge litaendelea kutekeleza wajibu wake kwa weledi na uwazi ili kuwaletea wananchi maendeleo kwa maslahi ya Taifa letu,” alisema Spika.
Spika Zungu alitumia nafasi hiyo kutaja mafanikio yaliyopatikana hadi kufika bunge la 13, ambapo ni pamoja na kuongezeka kwa wingi wa wawakilishi na demokrasia bunge, kuimarika kwa shughuli za Kamati za bunge katika kusimamia Seerikali.
Mafanikio mengine ni kuimarika kwa diplomasia za Kibunge, kuongezeka kwa mifumo wa Kidigitali katika shughuli za bunge na kuendelea kwa maboresho ya miundombinu na mazingira ya bunge.
“Mafanikio haya yamesaidia kuongeza hadhi ya bunge na kuongeza tija ya majukumu ya bunge. Bunge limeendelea kuimarika katika kutekeleza majukumu yake ya kuishauri na kuisimamia Serikali kwa kipindi chote cha historia,” alisisitiza Spika Zungu.
Aidha, Spika Zungu alisema, Tanzania inaendelea kufanya vizuri kwa kutoa uwakilishi bungeni kwa makundi mbalimbali; wanawake, vijana na wenye ulemavu, ambapo uwakilishi wa makundi hayo umeongezeka kwa kiwango cha juu.
Alisema, kwasasa uwakilishi wa wanawake bungeni ni asilimia 40%, ambapo kuna chama cha wanawake wabunge ambacho lengo lake ni kuwaongezea uwezo wabunge hao, uwakilishi wa vijana umefikia wabunge 72 na sasa kimeanzishwa chama cha wabunge vijana Tanzania, huku wabunge wenye ulemavu wakiongezeka na kufikia 11.
Awali, akizungumzia kuhusu sherehe za maadhimisho ya miaka 100 ya bunge, Spika Zungu alisema, mwaka huu unaweka alama muhimu katika historia ya Taifa kutokana na kutimia kwa karne moja tangu kuanzishwa kwa mhimili huo ambao umeendelea kuwa nguzo ya demokrasia nchini kupitia majukumu yake ya kutunga sheria, kuwakilisha wananchi na kuisimamia Serikali.
Alisema, maadhimisho hayo yataongozwa na kaulimbiu isemayo “Miaka 100 ya Bunge: Historia Yetu, Dira Yetu,” yakilenga kutoa fursa ya kutafakari historia ya Bunge, kuthamini mchango wa viongozi waliowahi kulitumikia kwa nyakati mbalimbali, pamoja na kuweka mwelekeo wa maendeleo ya mhimili huo kwa karne ijayo.
Spika alisema, maadhimisho hayo yataonesha safari ya miaka 100 ya maendeleo ya Bunge la Tanzania, tangu kuanzishwa kwa Baraza la Kutunga Sheria mwaka 1926 wakati Tanganyika ikiwa chini ya utawala wa kikoloni wa Uingereza, hadi kufikia Bunge la 13 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Katika mkutano huo, Spika Zungu amevitaka vyombo vya habari kushiriki kikamilifu kuelimisha na kuhabarisha umma kuhusu maadhimisho hayo ili historia ya Bunge la Tanzania iendelee kuhifadhiwa na kufahamika kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
“Ninyi wanahabari ni wadau muhimu katika kuandika historia ya Taifa letu. Tunatarajia ushiriki wenu mkubwa kuhakikisha Watanzania na dunia kwa ujumla wanafahamu historia ya miaka 100 ya Bunge letu,” alisisitiza Spika Zungu.
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilianza mara baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Kabla ya hapo palikuwa na Baraza la Kutunga Sheria (LEGCO) na Bunge la Tanganyika.
Machi 19, 1926 wakati Tanganyika ikiwa chini ya utawala wa Waingereza, Bunge la Uingereza lilipitisha Sheria iliyoitwa The Tanganyika (Legislative Council) Order in Council, 1926 kwa lengo la kuanzisha Baraza la Kutunga Sheria la Tanganyika (The Legislative Council of Tanganyika Territory – LEGCO). Baraza hilo lilizinduliwa rasmi Mjini Dar es Salaam Disemba 7, 1926.