RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amewakaribisha wawekezaji na wafanyabiashara kutoka nchi za Kiarabu kuwekeza Zanzibar, akisisitiza kuwa Zanzibar ina mazingira bora ya uwekezaji na fursa nyingi katika sekta za utalii, uchumi wa buluu, mafuta na gesi, uvuvi, utalii wa mikutano , pamoja na maendeleo ya Bandari Jumuishi ya Mangapwani.
Rais Dkt. Mwinyi ametoa wito huo leo, Juni 5, 2026, Ikulu Zanzibar, alipokutana na Mabalozi wa nchi za Kiarabu wanaoziwakilisha nchi zao nchini Tanzania waliofika kumpongeza kwa mafanikio ya maendeleo yanayopatikana Zanzibar chini ya uongozi wake.
Aidha, amezishukuru nchi hizo kwa kuendelea kuimarisha ushirikiano na Zanzibar kupitia misaada na uwekezaji katika sekta za elimu, afya na miundombinu, huku akiomba kuongezwa kwa ushirikiano katika nyanja za teknolojia ya kidigitali na mafunzo kwa vijana wa Zanzibar.
Mabalozi waliofika Ikulu ni pamoja na :
01.Mhe. Ahmada El Badaoui (Comoro)
02.Mhe. Sharif Abdelhamid Ismail (Misri)
03.Mhe. Yahya Ahmed Okesh (Saudi Arabia)
04.Mhe. Mohamed Abdala Abdelhameed (Sudan)
05.Mhe. Ghalib Zemane (Algeria)
06.Mhe. Salam Abuu Sharara (Palestina)
07.Acram Fayz Alhada, Kaimu Balozi wa Syria
08.Ahmad Sale Al Umar, Kaimu Balozi wa Yemen
09.Abdulla Saeed Al Naimi, Kaimu Balozi wa Qatar
10.Abdillatif Abdullah Hilowle, Kaimu Balozi wa Somalia
11.Ezzeddin Bahri, Kaimu Balozi wa Libya.
Kwa niaba ya Mabalozi hao, Balozi wa Saudi Arabia nchini Tanzania, Mhe. Yahya Ahmed Okesh, alimpongeza Rais Dkt. Mwinyi kwa uongozi wake ulioleta mafanikio makubwa katika maendeleo ya miundombinu, uchumi na sekta ya utalii, hatua inayozidi kuiimarisha Zanzibar kama kitovu cha uwekezaji na utalii katika ukanda wa Afrika Mashariki.