WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Ridhiwani Kikwete amesema, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anaendelea kupeleka furaha na neema kwa watumishi umma nchini.
Waziri Kikwete alisema hayo kwenye mkutano wa Maafisa Tawala na Rasilimali Watu, uliofanyika kwenye Ukumbi wa AICC na kuweka wazi kwamba, yapo maamuzi mbalimbali yamefanywa na Serikali ya Awamu ya Sita katika kuhakikisha maslahi ya Watumishi wa umma nchini yanaboreshwa.
Kikwete alitaja baadhi ya maamuzi hayo kuwa ni, kupandisha madaraja watumishi 219,042 ambayo ni hatua ya kihistoria katika kuimarisha utumishi wa umma nchini na hatua hiyo imepata ridhaa ya Rais Dkt. Samia.
Maamuzi mengine ni ongezeko la mishahara ya watumishi wa umma (2025): +35.1% , Ongezeko la kima cha chini sekta binafsi (2025/26): +33.4% , ambapo Sekta mbalimbali zitanufaika na maboresho hayo ikiwemo afya, elimu, kilimo, mawasiliano, usafirishaji, nishati, viwanda, biashara, hoteli, michezo, uvuvi, baharini, madini, utamaduni n.k.
“Matokeo haya kitakwimu zinaonyesha kasi ya mageuzi ya kiutumishi chini ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ambayo inaonyesha uongozi wa kimkakati unaoweka mbele ustawi wa watumishi na ufanisi wa taasisi za umma,” alisema Waziri Kikwete.
Aidha, Waziri Kikwete alitumia nafasi hiyo kuwakumbusha watendaji hao kutekeleza wajibu wao na kama ambavyo Serikali inapeleka furaha na neema kwao, nao wapeleke furaha hiyo na neema kwa Watanzania.