Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye hafla ya kupokea Ripoti ya Tume ya Rais ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, 2025, Ikulu Jijini Dar es Salaam, tarehe 23 Aprili, 2026.
TUME ya Uchunguzi wa Matukio ya Uvunjifu Amani Oktoba, 2025 imesema baadhi ya wanasiasa na wanaharakati walitumia changamoto za wananchi kuwashawisha na kuwachochoea kushiriki ghasia kabla na wakati wa uchaguzi mkuu.
Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Othman Chande ameeleza hayo leo Jumatano Aprili 23, 2026 akitoa matokeo ya ripoti hiyo mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan, Ikulu Dar es Salaam.
“Ushahidi umeonyesha baadhi ya wanaharakati na wanasiasa walitumia changamoto za wananchi zilizotokana na vyanzo mbalimbali kama fursa ya kuhamasisha wananchi kushiriki katika ghasia hizo,”
“Tathimini ya Tume imebaini vichocheo mahsusi vilivyohamasisha ari ya kufanya ghasia kabla na baada ya uchaguzi mkuu,” amesema Jaji Chande.
Amesema vichocheo hivyo vimewekwa katika makundi matatu; mitandao ya kijamii, akisema kwa mujibu wa mashahidi waliofika mbele ya Tume walieleza kuwa mitandao yao ilitumika kabla na baada ya uchauguzi mkuu kuwa mitandao yao ilitumika kwa kiwango kikubwa.
“Aidha waliibuka wabuni mada kwenye mitandao ‘content creator’ ikiwemo kuhamasisha wananchi wasishiriki uchaguzi mkuu au kuhakikisha haufanyiki,” amesema.
Katika hatua nyingine, Jaji Chande amesema, vifo vilivyotokana na ghasia za uchaguzi huo ni 518, ambapo wanaume ni 490, sawa na asilimia 94.6 na wanawake ni 28, sawa na asilimia 5.4 na vingi kati vya vifo hivyo vilikuwa sio vya kawaida (unnatural).
Amesema, Mkoa wa Dar es Salaam ulikuwa na vifo vingi zaidi, ukiwa na vifo 182, ikifuatiwa na Mkoa wa Mwanza vifo 90; Mbeya vifo 80; na Mkoa wa Arusha vifo 53.
Kati ya vifo hivyo 518, ishirini na moja (21) vilikua vya watoto. Katika kundi hilo, 15 walikuwa watoto wenye umri kati ya miaka 15 – 17, wanne (4) walikuwa na umri kati ya miaka 7 – 10, na wawili (2) umri chini ya miaka mitano.
“Vifo 502 sawa na asilimia 96.9 vilikuwa vya raia (civilians), na 16 sawa na asilimia 3.1 vilikuwa vya maafisa na askari wa vyombo vya ulinzi na usalama.”
“Kati ya watu 518 waliofariki, 373 walifikishwa hospitali wakiwa wamefariki, majeruhi 121 walifariki wakati wakiwa wanapatiwa matibabu, na maiti 24 hakuna taarifa kutoka vituo vya kutolea huduma za afya. Kati ya Maiti 518, maiti 480 sawa na asilimia 92.7 zilitambuliwa na kuchukuliwa na ndugu na familia,” amesema Jaji Chande.