MGOMBEA wa nafasi ya Rais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Chama Cha Mapinduzi kitaendelea kuhubiri na kudumisha amani, umoja na mshikamano miongoni mwa Wazanzibari bila ubaguzi wa aina yoyote.
Akizungumza Oktoba 15, 2025, katika mkutano wake na makundi ya wajane, wafuasi wa imani ya Rastafarian, jamii ya Wahindu na Ismailia, uliofanyika katika Ukumbi wa Idrissa Abdulwakil, Kikwajuni, Mkoa wa Mjini Magharibi Dkt. Mwinyi amesema kuwa asili ya mtu si kigezo cha kubaguliwa, na kwamba CCM inawatambua wananchi wote kuwa Wazanzibari halisi, bila kujali chimbuko lao.
Aidha, Dkt. Mwinyi amewahimiza wanajamii hao kuendelea kukiamini Chama Cha Mapinduzi, akibainisha kuwa ndicho chama pekee kilichoonesha uthabiti katika kulinda amani na utulivu wa nchi tangu kuasisiwa kwake.
Halikadhalika, Dkt.Mwinyi amewahakikishia wajane kuwa Serikali inaandaa sheria kali dhidi ya wazazi wanaotelekeza watoto wao, akisisitiza kuwa katika awamu ijayo, hatua madhubuti zitachukuliwa kuhakikisha haki za watoto na malezi bora zinalindwa ipasavyo.
Kuhusu mipango ya kiuchumi, Dkt. Mwinyi amebainisha kuwa Serikali itahakikisha hakuna kundi litakaloachwa nyuma katika utekelezaji wa programu za uwezeshaji wananchi kiuchumi.
Alisema Serikali inaandaa mikakati ya kuyafikia makundi yote ambayo bado hayajafaidika, ili kuyapatia mikopo nafuu na fursa za kujikwamua na umaskini.
Vilevile, Dkt. Mwinyi amewataka wananchi wote, wakiwemo wanachama wa makundi hayo, kujitoa kwa wingi siku ya kupiga kura Oktoba 29, 2025, akiwahakikishia kuwa amani, usalama na utulivu vitakuwepo wakati wote wa uchaguzi.
Wawakilishi wa makundi hayo wamempongeza Rais Dkt. Mwinyi kwa kuwajumuisha na kuwathamini katika kampeni zake, wakisema hatua hiyo inaonesha dhamira yake ya kweli ya kujenga Zanzibar ya usawa na maendeleo.
Wameahidi kumpa ushirikiano na kumchagua tena ili aendelee kuongoza Zanzibar katika safari ya maendeleo endelevu.