Mbeto: Tutekeleze wajibu ili tupate haki

0

Na Iddy Mkwama

KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis amesema, kila mmoja ana wajibu wa kutimiza wajibu wake kabla ya kudai haki.

Mbeto alisema hayo kwenye mahojiano maalumu hivi karibuni akiwa Kisiwani Pemba, wakati akijibu madai yanayotolewa na viongozi wa ACT Wazalendo kwenye mikutano yao ya kampeni za uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 29, 2025.

“Kuna vitu vitatu ambavyo vinatakiwa kuzingatiwa, wajibu, haki na amani, ili upate haki ni lazima utekeleze wajibu. Wajibu wetu kama raia, tunatakiwa kutii sheria,” alisema.

Mbeto alisema, baraza la wawakilishi limetunga sheria ambayo kila mmoja anapaswa kuifuata, “naomba nitoe elimu kidogo, kazi ya baraza la wawakilishi ni kutunga sheria, kazi ya mahakama ni kuitafsiri sheria, kazi ya serikali ni kuisimamia sheria itekelezwe.”

Alisema, moja ya mambo ambayo viongozi wa ACT wanayalalamikia, ni suala la upigaji wa kura ya mapema kwa watumishi wa tume ya uchaguzi ambao wamepangiwa kufanya majukumu yao mbali na vituo walivyojiandikisha kupiga kura.

Mwenezi huyo alisema, ukiwasikiliza ACT wanavyolalamika ni kama sheria hiyo imepitishwa hivikaribuni na Rais Dkt. Hussein Mwinyi, wakati ilitungwa mwaka 2018 wakati huo akiwa mbunge.

“Hawa jamaa wanalalamika kuhusu kura ya mapema, ukisoma sheria namba 4 ya mwaka 2018, wakati huo hata Hussein Mwinyi hayupo, yeye aliingia 2020, hii ni sheria ya uchaguzi ibara ya 82 ilisema kutakuwa na kura ya mapema, imetungwa na baraza la wawakilishi,” alisema Mbeto.

Alisema, sheria haiwezi kuondolewa kienyeji, badala yake kuna taratibu zinatakiwa kufuatwa “Hussein Mwinyi kaikuta, unataka aiondoshe, kwani yeye ndo anaondosha sheria? Kama kuna sheria haipo sawa, mnatakiwa wawakilishi wenu wapeleke muswada wa kutaka mabadiliko, hawakufanya hivyo.”

Mbali na hilo, alisema kuna mahakama ya katiba ambayo inatafsiri kama kuna sheria inakwenda kinyume na katiba, sheria hiyo inaweza ikafutwa, “waulizeni waliwahi kupeleka muswada wa mabadiliko ya sheria hiyo au kufungua shauri kwenye mahakama ya katiba? Kwa maana hiyo wanawadanganya watu.”

“Hata Maalim Seif aliwahi kusema, hawa maafisa wa tume ni aidha waruhusiwe kupiga kura kwenye vituo vyao au wapewe fursa ya kupiga kura mapema, hii kuwapa fursa ya kupiga kura wanapofanyia shughuli zao ilikataliwa kwasababu hawamo kwenye daftari la kupiga kura la eneo lile”

“Kwa maana hiyo yule anayetoka kule kwenda kwenye kituo alichojiandikisha, aruhusiwe ili siku ya pili atulie kwenye majukumu yao, kosa liko wapi? Bahati nzuri, kwenye kila kituo kuna mawakala wa kila chama, tunagombana kwenye kitu gani? Wakala ndiye msimamizi wa kura zetu kwenye kila kituo,” alisema.

Mbeto alisisitiza “ukitekeleza wajibu utapata haki, usipotekeleza wajibu, hauwezi kupata haki, hautaki kutimiza wajibu unataka haki, ndio matatizo yanatokea.”

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here