Na Albert Kawogo
VIONGOZI wa Chama cha Mapinduzi (CCM), kuanzia Mwenyekiti wake, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Hussein Ali Mwinyi, Makamu wa CCM, Stephen Wassira na Mgombea Mwenza, Dkt. Emmanuel Nchimbi wamekuwa wakijinasibu kuwa CCM itapata Ushindi wa Kishindo.
Pembeni yao kuna Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa chama hicho, Kennan Kihongosi ambaye katika mikutano mbalimbali ya kampeni inayoendelea, neno lake kuu ni CCM Itashinda kwa Kishindo na kudumisha amani.
Kihongosi amechukua nafasi ya CPA Amos Makalla ambaye kwa sasa ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha.
Pamoja na kwamba kila mmoja yuko kwenye harakati za kampeni, lakini Chagizo la Ushindi wa Kishindo hufanywa na kila kada lakini kazi ya kuweka karaha, kejeli kuelekea ushindi huo ni kama ameachiwa Kihongosi kwenye mikutano ya chama hicho aliyoifanya kuinadi Ilani ya Uchaguzi.
Mwingine ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM, John Mongella ambaye naye amekuwa akiutangazia umma kuwa CCM itashinda kwa kishindo.
Siku moja baada ya kuteuliwa, Wassira naye akasema kuwa CCM haina mpango mwingine zaidi ya kukamata dola na kupata ushindi wa kishindo.
Makala hii inaangazia baadhi ya maeneo kati ya mengi ambayo Rais Samia ameyapa jeuri CCM kujinasibu kupata ushindi wa kishindo katika Uchaguzi Mkuu 2025.
Hiyo pekee hasa ni pale Wabunge au viongozi wanaposema, hawana deni na Rais Samia kwa kuwa kila walichotaka ametimiza zaidi ni katika majimbo.
MTAJI WA WANACHAMA
Kati ya vitu ambavyo CCM inajidai navyo hasa, ni mtaji wa wanachama wa chama hicho, ambao kwa sasa wamefikia zaidi ya milioni 13, wapo wapenzi na mashabiki wanaokikubali Chama cha Mapinduzi.
Mfano mzuri ni katika mikutano ya kampeni ya wagombea wa CCM, Samia Suluhu Hassan na Mgombea Mwenza, Dkt. Emmanuel Nchimbi.
Hao huwezi kusema ni wanachama moja kwa moja, kuna wapenzi na mashabiki ambao huwaelezi kitu kuhusu CCM.
Mfano mzuri ambao CCM imejitengenezea mazingira mazuri ya ushindi wa kishindo, ni halaiki iliyojitokeza katika maeneo machache ya kampeni kama; Dar es Salaam, Morogoro Mjini, Kibaigwa, Kondoa, Songwe, Tunduma, Mbeya Mjini, Mbarali, Uyole, Makambako, Mufindi, Iringa Mjini, kampeni zote za Kigoma na sasa Zanzibar.
Kwa upande wa Mgombea Mwenza, Dkt. Emmanuel Nchimbi, ameivuruga mikoa ya Kanda ya Ziwa kabla ya kuingia Kanda ya Kaskazini.
Kwa upande mwingine, uhakika upo kwa hao wanachama milioni 13 ambao pekee ni wale waliosajiliwa kidigiti, sasa kuna kuna hawa nao wanaounga mkono juhudi lakini pia kuna wale kutoka vyama vingine.
Kuna lile kundi la aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana (UVCCM), Jokate Mwegelo, wanaojiita First Time Voters, hao ndio usiseme.
Ni kundi la vijana ambalo Jokate na wenzake, hawana budi kupewa mauwa yao kwa ubunifu wao na hata kuwahamasisha vijana hao. Walifanya uzinduzi wao Mei 24, 2025.
Kundi hili ni la vijana ambao ndio kwanza wameingia miaka 18 na wana nafasi ya kupiga kura kwani pamoja na harakati hizo, walikuwa na kazi moja ya kujiandikisha.
Makamu wa Mwenyekiti wa CCM, Stephen Wassira anasema: Kwa mtaji wa wanachama waliowasajili, CCM ina nguvu ya kuendelea kushika madaraka na kuleta maendeleo endelevu kwa Watanzania.
AMANI NA UTULIVU
Katika mikutano yake ya kampeni, Dkt. Samia na mwenzake wa Zanzibar wamekuwa wakihubiri amani, umoja na utulivu. Hii ni kete nyingine muhimu ambayo CCM inatamba nayo, kudumisha amani, umoja na utulivu kwa kila Mtanzania.
Dkt.Nchimbi naye haachi kuwaambia Watanzania kudumisha amani, umoja na mshikamano.
Hilo halina ubishi, Watanzania wana imani kubwa na Rais Samia katika kudumisha amani ya taifa, kwani tangu aingie madarakani, amani imetamalaki. Watanzania wanatakiwa waelewe kwamba amani ya Tanzania ikivurugiga, hakuna Tanzania nyingine.
Huduma mbalimbali zitasimama kama afya, elimu, miradi ya maendeleo, uzalishaji mali, uchumi kuporomoka, hakuna biashara inayofanyika na hakuna kinachoendelea kwa kuwa taifa limevurugika.
Watanzania wanataka maisha yao ya kawaida bila kuhofia usalama wao na wasiwasi wa kesho yao, kutembea kwa amani, kufanya kila unachoweza kufanya bila kuvunja sheria.
Mengi yanaonekana Mataifa ya wenzetu ikiwemo mataifa jirani, kila siku ni vurugu, mara biashara hazifanyiki, kutangazwa hali za hatari na zaidi ya yote tunasikia amri za kutotembea usiku. Tanzania hata ukikesha unatembea, rukhsa.
Rais Samia, katika mikutano yake ya kampeni karibu siku zote tangu ilipozinduliwa Agosti 28, 2025 amekuwa akiwasisitiza Watanzania kutokubaliana na kauli za wapinzani za kutaka kuvuruga amani kwani amani ikivurugika hakuna Tanzania nyingine hivyo, tudumishe amani, umoja na mshikamano wa Taifa.
Kimsingi, hii itabaki kuwa kete muhimu ambayo mbali na Rais kuisisitiza, viongozi wote wa juu wa chama na Serikali na wenyewe wamekuwa wakihimiza wananchi kuidumisha amani waliyotuachia waasisi wa taifa letu, Hayati Julius Nyerere na Hayati Abeid Amani Karume.
Watanzania wanataka amani, tofauti na wanasiasa wengine wanaohamasisha maandamano na kukinukisha.
DIRA YA TAIFA 2050
Kati ya Tume mbalimbali alizounda Dkt. Samia, ni pamoja na Tume ya Kuratibu maoni ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ambayo imekamilisha kazi yake na kutengeneza dira ambayo ameizindua Julai 17, 2025 mjini Dodoma.
Umuhimu wa kete hii kuelekea uchaguzi, ni kwamba; Rais ameona Taifa haliwezi kwenda bila kuwa na Dira ya Maendeleo.
Kwa msingi huo, Watanzania wana picha ya mwelekeo wa taifa lao wanalotaka liwe katika ngazi mbalimbali za kijamii, kielimu, afya, nishati, miundombinu, kiutamaduni na mambo mengi sanjari na mabadiliko ya sayansi na teknolojia.
Rais Samia angeweza kutengeneza mazingira yake anayotaka kwa Tanzania kwa kuwa ana uwezo wa kufanya hivyo, lakini si mwenye tamaa, si mbinafsi amewashirikisha Watanzania wa kada zote kupitia Tume hii iliyoongozwa na Prof. Kitila Mkumbo, Dkt. Asharose Migiro na wengine.
Lengo la mpango huu ni Watanzania wenyewe kuamua Tanzania Waitakayo katika miaka 25 ijayo ambayo inatakiwa kurandana na Ilani za uchaguzi za vyama.
Ukiangalia sehemu kubwa ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi CCM ya 2025-2030, haiachani na Dira ya Taifa ya Maendeleo na kwamba kile ambacho Watanzania wanataka ndicho hicho kilichomo kwenye Ilani ya CCM ambayo Rais Samia ameizindua Mei 30, 2025 mjini Dodoma na anatekeleza.
Mbali na Tume ya kuratibu maoni ya Dira ya Taifa, Rais Samia ameunda Tume mbalimbali kwa masuala ya kisiasa, kijamii, Haki Jinai na mengine mengi. Hii yote ni Watanzania kusikilizwa.
FEDHA ZA MAENDELEO
Dkt.Samia amewarahisishia wabunge na madiwani kazi za kujinadi kwa nguvu katika kampeni zinazoendelea, kwani kila anayesimama, ni kwamba wamepata fedha, wamekamilisha shule, hospitali na mengine.
Wengine hudiriki kusema kuwa walikuwa na shule nne sasa ziko 10, walikuwa na vituo vya afya vitatu sasa 10, kila jambo limeongezeka kwa kiasi kikubwa. Hiyo yote ni kutokana na fedha za miradi ya maendeleo mbalimbali kupelekwa kunakohusika na kutengeneza mazingira ya ushindi wa kishindo.
Dkt.Samia ni muumini wa mambo kwenda mbele ndio maana amediriki kutoa fedha nyingi katika maeneo mbalimbali ikiwemo miradi ya kimkakati ili kusiwe na mikwamo na ndiyo inayombeba sasa na wabunge kiasi cha kujaza mikutano yake wananchi wakitaka kumpa ahsante.
Kabla ya kampeni na sasa, kila wizara ikiwemo zile za kisekta, zimeelezea mafanikio ya Awamu ya Sita na zaidi ni kuongezwa fedha kukwamua miradi waliyoianzisha kufikia hatua za ukamilishwaji, katikati au hatua za awali kwa ajili ya wananchi.
Hapa ndipo CCM inajiandaa kuvuna kura kama zilivyo fedha nyingi kutumwa kila wizara kwa ajili ya wananchi kama maji, kilimo au afya. Wananchi ambao hawakuwa na taarifa, sasa wanapata taarifa kwa uwingi wao, lakini pia wameona matokeo na si maneno.
Kwa kuwathamini wananchi, Serikali inaendelea kutenga fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo na ndiyo maana Dkt. Samia amekuwa akisema Watanzania wakiwapa ridhaa hadi 2025-2030 atawafanyia makubwa.
Hapa peke yake, CCM imepiga bao kwa maana ya kwamba fedha nyingi zimetengwa kwa ajili ya miradi inayogusa wananchi kuelekea 2025-2030.
Mfano mzuri, katika miaka minne ya Rais Samia, bajeti ya afya imeongezeka hadi kufikia Shilingi trilioni 1.618 kwa mwaka 2025/2026 kutoka Shilingi bilioni 33.195 za mwaka wa fedha 2020/2021.
HUDUMA ZA JAMII
Hapa ndipo panaangaliwa zaidi kwa kuwa mambo mengi yanayomgusa mwananchi moja kwa moja yanapatikana katika eneo hili.
Utekelezaji wa Ilani 2020/2025 wa Rais Samia alipoingia ofisini, alianza kwa kukazia eneo la maji kwa kuongeza bajeti pamoja na kuanzisha Kampeni ya Kumtua Mama Ndoo ambayo sasa imefikia pazuri.
Kwa asilimia kubwa, Rais Samia amewafuta machozi akina mama na wengi wanasema sasa ndoa zao zimeimarika. Hapa Rais amewagusa akina mama kwa sehemu kubwa na bado anaendelea kukamilisha miradi mbalimbali ya maji.
Rais Samia anaanzisha gridi ya taifa ya maji itakayounganishwa na miradi mikubwa ya maji kutoka Ziwa Victoria, Tanganyika na Ziwa Nyasa, mpango ni kufikisha maji asilimia 70.9 wakazi wa vijijini wawe wanapata maji wakati asilimia 90 katika maeneo ya mijini, sasa kwa vijijini imeongezeka hadi kufikia asilimia 79.6 wakati mijini imefikia asilimia hiyo 90.
Kura za CCM hazina mjadala hapa kwani malengo ni kukamilishwa kwa miradi 1,633 ya usambazaji maji mijini na vijijini na kufikia wananchi 12,547,526 pamoja na ukamilishaji wa vituo 107,819 na maunganisho katika kaya 196,160.
Katika mkutano wake Songwe na Njombe, Dkt. Samia amesema mpango wa Serikali ni kuzalisha umeme wa aina nyingi, upepo, joto ardhi, jua na maji ili kukabiliana na matatizo ya umeme.
Umeme na wenyewe umekuwa mpango mzima kwani hata ile katikakatika imepungua kutokana na kukamilika ujenzi wa Bwawa la kufua umeme la Mwalimu Nyerere JNHPP lililoko Rufiji mkoa wa Pwani likigharimu Sh 6.558 trilioni na kuzalisha Megawati 2,115.
Ni wazi, kishindo cha kura za CCM ziko maeneo ya vijiji vyote 12,301 ambavyo vimekamilishiwa upatikanaji umeme kupitia mpango wa REA wa upelekaji wa umeme vijijini.
Kwa upande wa barabara, Wakala wa Barabara (TANROADS) wamejenga maelfu ya kilomita za mtandao wa barabara za lami zikiwa zimekamilika huku Kilomita nyingine zinaendelea kujengwa Tanzania.
TARURA na wenyewe wanaendelea na maboresho ya barabara za mlisho maeneo mbalimbali nchini.
Pamoja na kuelezea hapo juu, eneo la afya, linagusa jamii ya watu wengi. Ilani ya CCM kipekee kabisa, imejipambanua kuwa kati ya 2025/2030, Serikali itajenga zahanati 947, vituo vya afya 277, hospitali za halmashauri 57, hospitali za mikoa nne na tatu za kanda na hizo zilizopo sasa zinazoendelea kutoa huduma.
Aidha, huduma za afya kwa wazee, mama na mtoto zimeimarika pamoja na utoaji tiba bure kulingana na aina ya ugonjwa kama kifua kikuu, UKIMWI na mengine.
KILIMO
Rais Samia ameweka fedha za kutosha kuhamasisha vijana kujikita kwenye kilimo na mengine yanayohusiana na kilimo, uvuvi akitoa boti na ufugaji wa kisasa. Bunge limepitisha bajeti ya kilimo kwa mwaka 2025/2026 ya Shilingi Trilioni 1.24.
Aidha, uanzishwaji wa miradi mipya ya kilimo ya ukubwa wa hekta 543,366 yenye thamani ya Shilingi Trilioni 1.18 na ujenzi wa mabwawa makubwa kwa ajili ya umwagiliaji.
Kuanzisha skimu mbalimbali za umwagiliaji ili kuachana na mpango wa kutegemea mvua ambazo mabadiliko ya hali ya hewa hupoteza wakulima mwelekeo.
HAKI
Eneo la utoaji haki na lenyewe limeimarishwa (haki jinai na madai). Rais Samia mwenyewe ni muumini wa haki na amekuwa akihimiza watoa haki kusimamia haki.
Akiwa kwenye mikutano ya kampeni Dar es Salaam, Morogoro, Dodoma, Iringa, Mbeya, Songwe na Njombe pamoja na mambo mengine amejikita kwenye haki.
Uanzishwaji wa Kampeni ya kitaifa ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia ambayo peke yake imefikia watu zaidi ya milioni 2 Tanzania nzima.
MIKOPO
Uwezeshaji wa makundi mbalimbali ya kijamii (vijana, wanawake, walemavu na wenye uhitaji maalumu).
Kwa kutambua tatizo la ajira kwa makundi hayo, Rais Samia ameelekeza mikopo itolewe kwa ajili ya kuwawezesha na Shilingi Bilioni 227.96 zilitengwa kwa Tanzania nzima.
Katika fedha hizo, Shilingi Bilioni 63.67 ni fedha za marejesho, Shilingi Bilioni 63.24 fedha zilizokuwa zimetengwa kwa mikopo na Shilingi Bilioni 101.05 fedha za makisio ya mapato ya ndani kwa mwaka 2024/2025.
Serikali imekuwa ikihamasisha vijana kujiunga katika makundi mbalimbali ya uzalishaji mali ikiwa ni njia rahisi kwa ajili ya kuwapatia fedha hizo. TAMISEMI imeshatoa maelekezo kuwa mikopo hiyo kusimamiwa na kuratibiwa katika ngazi za mikoa, wilaya na kata.
ELIMU
Kwa upande wa elimu, inaanzia ujenzi wa madarasa mapya na sasa ni maghorofa maeneo mengi, uboreshwaji wa shule chakavu na juu ya yote, elimu kutolewa bila malipo kuanzia chekechea hadi kidato cha sita.
Kuanzishwa kwa mafunzo ya amali ikiwemo ujenzi wa vyuo vya VETA 64 kila wilaya, mikopo ya elimu ya juu kuongezwa ikiwemo vyuo vya kati kutoka Shilingi bilioni 731 hadi shilingi bilioni 787.4 zilizotolewa kwa wanafunzi 248,331.
MIRADI YA KIMKAKATI
Kuna ile miradi mikubwa ya kimkakati; Bwawa la kufua umeme la JNHPP, matarajio ni kuzalishwa kwa Megawati 2,115 na hadi sasa ujenzi umekamilika.
Aidha, madaraja mengi kwa sehemu kubwa yamekamilika kuanzia Kigongo-Busisi lililozinduliwa Juni 19,2025, Pangani, Mbambe mkoani Pwani huku safari za treni ya SGR Dar-Moro-Dodoma zinaendelea na sasa mpango ni kufikisha Rwanda na Burundi. Aidha mpango mwingine ni kuitoa reli hiyo hadi Mwanza.
Pia, ujenzi wa viwanja vya ndege, ununuzi wa ndege, barabara huku Dar es Salaam ikiwa katika hatua za mwisho baada ya kufumuliwa na mengi yote kazi inaendelea kwa ajili ya Watanzania.
UWAJIBIKAJI
Katika kipindi cha miaka ya karibuni, Wakati akipokea ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Charles Kicheere, mjini Dodoma, hitimisho la Mbio za Mwenge Rais Samia amepongeza kupungua kwa hati chafu na kupungua kwa kiasi kikubwa miradi ya chini ya kiwango ni kwamba kazi inafanyika.
Hii inaweka imani kwamba, kazi inafanyika hata kimyakimya. Rais Samia amekuwa akisema kila eneo lenye kasoro linaloripotiwa halitaachwa, litamalizwa.
Binafsi amekuwa akisema kuwa yeye si mtu wa kelele, zaidi ni kucheza na kalamu.
UWEKEZAJI
Mwaka huu 2025 peke yake, Kituo cha Uwekezaji kimepanga kusajili miradi 1,500 ambayo kukamilika kwake kutakuwa kimetatua ajira kwa vijana. Tayari miradi 372 imesajiliwa kati ya Januari na Mei 2025
Uwekezaji umeongeza thamani ya uchumi ikiwemo kuvuna kodi, Watanzania kupata ajira na kuimarika kwa teknolojia. Hapo peke yake ni kete muhimu kwa CCM.
Aidha, matokeo ya uwekezaji yameshaanza kuonekana, na mfano mzuri ni Gawio la TPA kwa Serikali lililotokana na uwekezaji wa Kampuni ya DP World kufikia Shilingi bilioni 181.5 kutoka shilingi bilioni 153.9 gawio la awali.
WACHIMBAJI WADOGO
Rais Samia ameahidiwa kura za kutosha za makundi mbalimbali ikiwemo wachimbaji wadogo kupitia Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Wadogo (FEMATA) wakisema ana kura zake kutokana na kuwajali.
MICHEZO
Kila mwanamichezo ni wazi ana kura kwa Rais Samia ikiwa ni shukurani kwa kuziwezesha timu kushiriki michezo mbalimbali.
Simba, Yanga zimefaidika kwa kiasi kikubwa, goli la mama, usafiri wa ndege kwenda na kurudi kwenye mechi zao, timu za taifa kuanzia U-20 hadi wakubwa, timu za wanawake peke yake zitamleta Rais Samia na timu yake kwa kupata ushindi wa kishindo.
Yako mengi, lakini kwa uchache hayo ni mazingira ambayo Dkt. Samia ameyatengeneza kupata kura za kishindo ifikapo Oktoba 29, 2025.