Na Albert Kawogo, Bagamoyo
SAFARI ya Subira Khamis Mgalu mgombea Ubunge wa Bagamoyo kwa tiketi ya CCM kuanza kuinadi ilani ya Chama cha Mapinduzi ya 2025-2030 inaanza rasmi kesho, pale kipenga cha uzinduzi wa kampeni kitakapopulizwa.
Uzinduzi huo utakaoanza alasiri ya kesho Jumatano Septemba 17, 2025 kwenye viunga vya uwanja wa shule ya Msingi Majengo, Bagamoyo utatangulizwa na ‘bashraf’ ya matembezi ya hiari ya CCM asubuhi kutoka ofisi za Chama hicho hadi shule ya Majengo.
Katibu wa Siasa Uenezi na Mafunzo wa CCM Bagamoyo Ramadhan Lukanga amesema, uzinduzi wa kampeni hizo utafanywa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida Martha Mlata huku akisindikizwa na wageni wengine mbalimbali makada wakongwe wa CCM wakiwemo Sophia Simba na Hawa Ghasia
Lukanga amewataja Wasanii watakaomsindikiza Subira kwenye uzinduzi wa mbio hizo za kampeni kuwa ni J Kombat, Peter Msechu, Siza Mazongela na Amadai.
Pia, Katibu huyo amesema kuwa pamoja na burudani mbalimbali za siku hiyo muhimu pia kutakuwa na tamasha la bodaboda (Bodaboda Festival) litakalosimamisha kwa muda mji mkongwe wa Bagamoyo kuashiria kuwa CCM imedhamiria ushindi wa kishindo wa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Subira Khamis Mgalu na madiwani wote.
Mgombea wa Ubunge CCM Bagamoyo Mgalu anaingia rasmi katika harakati za kusaka kura za ushindi kwa Chama cha Mapinduzi baada ya ushindi wa kishindo baada ya kuwabwaga wagombea wengine wanne kwenye kura za maoni mapema mwezi Agosti mwaka huu.