‘Changamkieni fursa zilizopo katika uchumi wa buluu’

0

WADAU wa maendeleo wametakiwa kuchangamkia fursa zilizopo katika uchumi wa buluu na kutoa mapendekezo yatakayosaidia Serikali na sekta binafsi kuchukua hatua zitakazochangia kukuza pato la taifa kupitia sekta hiyo.

Wito huo umetolewa na Naibu Katibu Mkuu (Muungano) Ofisi ya Makamu wa Rais Abdallah Hassan Mitawi wakati akifungua Kongamano la Uchumi wa Buluu jijini Dar es salaam leo Septemba 10, 2025.

Amesema kuwa Serikali imedhamiria kutumia fursa za rasilimali za bahari kwa maendeleo endelevu katika kukuza uchumi sanjari na kupanua wigo wa ajira nchini.

Pia, Mitawi amesema kuwa vijana, wanawake na wadau wa sekta binafsi wana nafasi kubwa katika kuchangia uchumi wa buluu hivyo wanapaswa kupewa kipaumbele katika sera, mafunzo na uwezeshaji wa kifedha ili waweze kushiriki kikamilifu na kwa tija.

Ameongeza kuwa ushirikiano kati ya nchi jirani na taasisi za kimataifa ni muhimu kwani bahari haina mipaka hivyo mafanikio katika sekta hii yanahitaji mshikamano wa kitaifa, kikanda na kimataifa.

Aidha, amesisitiza kuwa uchumi wa buluu ni eneo lenye fursa kubwa ambazo hazijatumika na zikitumika ipasavyo zitakuwa ni uti wa mgongo wa mageuzi ya maendeleo ya taifa kutokana na kuwepo kwa maeneo makubwa ya vyanzo vya maji.

”Sote tunatambua kuwa uchumi wa buluu unapatikana kupitia mito, bahari, maziwa, misitu na ardhi oevu nchini ambayo yakitumika ipasavyo yataongeza ajira, kukuza biashara, kuimarisha usalama wa chakula hivyo kuboresha maisha ya wananchi,” amesema Mitawi.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Mkurugenzi wa Miundombinu ya Uchukuzi Shomari Shomari ameelezea nafasi kubwa ya sekta ya usafirishaji na maboresho ya miundombinu ya bandari katika kuimarisha uchumi wa buluu.

Amebainisha kuwa miradi mikubwa ya kisasa ya reli, maboresho ya bandari na udhibiti wa usafiri na usalama wa majini ni nyenzo muhimu katika kufungua fursa za uchumi wa buluu ikiwemo kukuza biashara na ajira kwa Watanzania

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here