Nchimbi atua Rukwa na Ilani mkononi

0

Na Iddy Mkwama

MGOMBEA Mwenza wa kiti cha urais kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi amesema, chama kinaangalia mahitaji ya wananchi hasa huduma za jamii pamoja na kuukuza uchumi wa wananchi na zaidi ni vijana.

Dkt. Nchimbi amesema katika miaka mitano iliyopita Serikali imewekeza katika nyanja mbalimbali kama sekta ya afya, elimu, miundombinu ya barabara za lami mjini na Vijijini kutoka Kilomita 39.4 hadi 46.5 pamoja na sekta ya uvuvi.

Akiinadi Ilani ya Uchaguzi Septemba 9, 2025, Wilayani Sumbawanga, Mkoani Rukwa, Dkt.Nchimbi amesema, malengo ya CCM ni kuboresha maisha ya Watanzania na kuwa na Taifa lenye kujitegemea.

Akizungumzia maendeleo yaliyofanywa na Rais Samia amesema amefanya mengi ikiwemo uboreshaji wa Bandari ya Kasanga, Uwanja wa Ndege, sanjari na kutoa mikopo kwa makundi maalumu.

Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi amesema chama kimejipanga kusimamia na kuimarisha huduma za afya kwa akina mama wajawazito na watoto ili kudhibiti na kumaliza vifo vya akina mama wakati wa uzazi kutoka asilimia 9 hadi 4.

Amesema, watapunguza udumavu kwa watoto wa chini ya miaka mitanona kuongeza huduma za lishe kwa makundi yanayoathirika zaidi ikiwa ni pamoja na watoto, wajawazito na vijana balehe.

“Licha ya mkoa wa Rukwa kulima mazao ya chakula na biashara lakini changamoto ya udumavu ni kwa asilimia 49.8 sasa tutahakikisha tunapunguza tatizo,” amesema Dkt. Nchimbi.

Kwa upande wake Mwenyekiti mstaafu wa mkoa wa Rukwa ambaye ameambatana na mgombea mwenza wa Urais Hamis Ally amesema, Chama cha Mapinduzi kina mikakati ya kudhibiti ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto, wasichana, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu.

Akimkaribisha mgombea mwenza wa urais Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Rukwa Siraf Maufi amesema, wataimarisha huduma za ustawi kwa wazee ikiwamo huduma za afya matunzo na ushirikishwaji katika maamuzi na shughuli mbalimbali za maendeleo.

Nao baadhi ya wananchi na wanachama waliojitokeza kusikiliza sera za CCM akiwemo Agnes lyoba amesema, anawaomba wagombea kutimiza yale ambayo wanaahidi ili waendelee kuaminika. “Niombe tu wagombea kutimiza ahadi zenu tunatamani kuona utekelezaji wake.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here