Uwanja wa Ndege wa Kisasa kufungua Utalii hifadhi ya Taifa ya Nyerere

0

UWANJA wa Ndege wa kisasa unaotarajiwa kukamilika Oktoba mwaka huu, ni miongoni mwa uwekezaji wa kimageuzi unaoendelea kufanywa na Serikali kuifungua sekta adhimu ya utalii.

Akishuhudia kuendelea kukamilika kwa Uwanja wa Ndege wa kisasa unaojengwa kwenye eneo la Mtemere kwenye Hifadhi ya Taifa ya Nyerere, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi, amesema uwanja huo utafungua “Serengeti” mpya hapa nchini ambayo ni Hifadhi ya Nyerere.

“Hifadhi hii ipo dakika 35 kwa ndege kutoka Dar lakini inaunganishwa na Barabara kadhaa ikiwemo ile ya Kisarawe-kutokea Dar es Salaam; Bigwa-Kisaki kama mtu anatokea Morogoro lakini pia inayopitiwa na treni ya Tazara kwa stesheni ya Vuga.

“Uwanja huu utakaokuwa na urefu wa km 1.8 kwa ile barabara ya ndege pekee lakini na barabara nyingine za akiba pia utakuwa na chumba cha kisasa cha kuongozea ndege, majengo ya kuondoka na kuwasili abiri yenye huduma za kisasa, ofisi na maegesho ya magari,” alisema Dkt. Abbasi akiwahimiza wakandarasi kuhakikisha mwezi ujao tabaka gumu la kwenye njia ya kuruka na kutua ndege kukamilika.

Utalii umeongezeka kwa kiasi kikubwa katika Hifadhi ya Nyerere kutoka wastani wa watalii 15,000 tu kwa mwaka 2021 hadi watalii 47,000 mwaka jana 2024.

Ikishinda Tuzo ya Eneo Lenye Mwonekano Munawari Afrika (Africa’s Leading Scenic National Park 2025) wakati wa Tuto za Utalii za Dunia-Kanda ya Afrika na Bahari ya Hindi, Hifadhi ya Nyerere inazidi kufahamika kwa mandhari zake adhimu, makumi ya wanyama, mito kama Mto Rufiji na sehemu kubwa chini ya Mto ikitengeneza maziwa mengi yanayotokana na mienendo ya kijiografia lakini eneo la juu likiwa na bwawa kubwa lenye upana wa km 30 na urefu wa km 100; sehemu ya Mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Mwalimu Nyerere.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here