Dkt. Migiro: CCM itaendelea kuimarisha maendeleo ya Taifa

0

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Asha Rose Migiro, amesema CCM itaendelea kuonesha mshikamano wa kisiasa na kijamii kwa wananchi katika kusimamia utekelezaji wa sera na ilani zake ili kuimarisha maendeleo ya taifa.

Dkt. Migiro amesema hayo Mjini Unguja wakati akiwahutubia wanaCCM katika mapokezi ya kumkaribisha Zanzibar mara baada ya uteuzi wake, huko katika uwanja wa Afisi kuu za Chama cha Mapinduzi (CCM) Kisiwandui.

Amesema, utekelezaji wa Ilani ya CCM umeendelea kuleta matokeo chanya katika nyanja mbalimbali za kijamii na kiuchumi, ikiwemo huduma za afya, elimu, miundombinu na kilimo kwani mafanikio hayo ndiyo msingi wa chama kuelekea uchaguzi mkuu.

Aidha, amesema ni heshima kubwa kwa chama hicho kumpa nafasi ya uongozi wa juu, huku akisisitiza dhamira yake ya kuendeleza utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa lengo la kuimarisha maendeleo ya taifa na ustawi wa wananchi.

“Tunafahamu kuwa Chama Cha Mapinduzi kimeaminiwa kwa miaka mingi na wananchi, hivyo ni wakati wa kuendelea kuinadi Ilani ya CCM na kuhakikisha tunasimamia maendeleo ya taifa letu moja lenye mshikamano, usawa na amani kwa manufaa ya wote,” Dkt. Migiro.

Amesisitiza kuwa uteuzi wake ni ishara ya usawa wa kijinsia na mshikamano ndani ya CCM, akibainisha kuwa kuchaguliwa kwa mwanamke kushika wadhifa huo wa juu ni hatua kubwa ya kuendeleza sera za usawa, mshirikiano na umoja katika chama.

Sambamba na hayo, amewataka wanachama na wananchi wa Zanzibar kujitayarisha kwa uzinduzi wa kampeni rasmi za chama utakaofanyika Septemba 13, 2025, kwa mujibu wa utaratibu uliopangwa.

Akitumia nafasi hiyo kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya chama hicho kwa kumteua na kuthibitisha jina lake kushika nafasi hiyo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here