BALOZI wa Tanzania nchini Sweden, Mobhare Matinyi, amefanya ziara katika makao makuu ya kampuni za Ericsson na Siemens Energy za Sweden kujadiliana kuhusu kuongeza uwekezaji na kuendelea kuleta teknolojia zao nchini.
Balozi Matinyi aliitembelea kampuni ya Ericsson Septemba, 2, 2025, jijini Stockholm na kuzungumza na viongozi na wataalam wao wakiongozwa na Mkurugenzi wa Sera za Serikali na Uhamasishaji, Ola Bergstorm.
Septemba 3, Balozi Matinyi alizitembelea ofisi za Siemens Energy mjini Finspang na kupokelewa na Afisa Mtendaji Mkuu wake, Gunnar Wik, akiwa na timu yake ya menejimenti na wataalam.
Kampuni ya Ericsson ilieleza na kuonesha kwa vitendo mapinduzi ya teknolojia ya mtandao wa intaneti wa 5G unavyotumika kwa pamoja na Akili Unde (AI) kutoa huduma za kitaalam kwenye sekta mbalimbali.
Mhandisi wa Ericsson Jon Gamble alisema nchini Sweden wanatumia teknolojia hiyo kwenye huduma za magari ya wagonjwa, zimamoto na polisi, na pia kwenye kilimo, elimu, afya, na uendeshaji wa miundombinu ya reli, bandari, viwanja vya ndege, usafirishaji umeme na uchimbaji madini.
Ericsson pia iko tayari kuisambaza tekinolojia ya 5G nchini kote ambako mtandao huu haujafika kwa kushirikiana na kampuni za simu Tanzania.
Nayo kampuni ya Siemens Energy ilionesha teknolojia yake kutengeneza mitambo ya kufua umeme kwa kutumia gesi ambayo pia inatumika nchini katika kituo cha kufua umeme cha Ubungo, jijini Dar es Salaam.
Kampuni ya Siemens imesema inataka kuendelea kushirikiana na Tanzania katika uzalishaji wa umeme kwa kutumia gesi katika miradi ya kimkakati ya Kinyerezi, Mkuranga, Somanga, Dodoma na Mtwara.
Sambamba na ziara hiyo, Balozi Matinyi pia alizungumza na wataalam 12 wa Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (Tanesco) waliopo Siemens kupata mafunzo maalum ya uendeshaji wa mitambo ya kufua umeme kwa njia ya gesi kuanzia Agosti 24 hadi Septemba 13, 2025.
Balozi Matinyi aliwataka wataalam hao kujifunza kwa bidii teknolojia hiyo kwani taifa linawategemea wao tu katika kujihakikishia usalama wa nishati.
Ziara hizo mbili ni kielelezo cha uhusiano mzuri wa kidiplomasia uliopo kati ya Tanzania na Sweden, hususan katika utekelezaji wa diplomasia ya uchumi kwa manufaa ya pande zote mbili.